Jicho letu mahakamani: ‘Kina Zombe wakinyamaza, wakijitetea wana hatia-59

Jicho letu mahakamani: ‘Kina Zombe wakinyamaza, wakijitetea wana hatia-59

Muktasari:

  • Katika sehemu ya 55 hadi 58 ya simulizi hii ya kesi ya mauaji, tuliona mawakili wa washtakiwa wakiwasilisha hoja zao kuishawishi Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, kuwa washtakiwa hawakuwa na kesi ya kujibu kuwataka kusimama kizimbani kujitetea.

Katika sehemu ya 55 hadi 58 ya simulizi hii ya kesi ya mauaji, tuliona mawakili wa washtakiwa wakiwasilisha hoja zao kuishawishi Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, kuwa washtakiwa hawakuwa na kesi ya kujibu kuwataka kusimama kizimbani kujitetea.

Katika ujumla, mawakili wote kwa nyakati tofauti waliieleza Mahakama kuwa upande wa mashtaka ulishindwa kuwasilisha ushahidi mzito wenye kuwagusa washtakiwa kiasi cha kuwalazimu kujitetea, huku wakichambua udhaifu wa ushahidi huo na hivyo wakaiomba Mahakamaa hiyo iwaachie huru.

Hii ni simulizi ya mauaji iliyokuwa ikiwakabili aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi mkoa (RCO) wa Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Abdallah Zombe, Mkuu wa Upelelezi Wilaya (OC-CID) ya Kinondoni, Mrakibu wa Polisi (SP) Christopher Bageni na askari polisi 11.

Washtakiwa walikuwa wakidaiwa kuwaua kwa makusudi wachimba madini watatu kutoka Mahenge wilayani Ulanga mkoani Morogoro, Sabinus Sabinu Chigumbi maarufu kama Jongo, mdogo wake Ephraim Chigumbi na Mathias Lunkombe pamoja na Juma Ndugu, dereva teksi wa Manzese Dar es Salaam, aliyekuwa akiwaendesha.

Walidaiwa kuwapiga risasi katika msitu wa Pande, Mbezi Luis, wilayani Kinondoni, Dar es Salaam, Januari 14, 2006, baada ya kuwatia mbaroni Sinza Palestina, nyumbani kwa mchimbaji mwenzao, walipokuwa wamempelekea mkewe fedha, wakihusishwa na uporaji wa fedha katika gari la kampuni ya Bidco.

Kesi hiyo ilisikilizwa na kuamuriwa na aliyekuwa Jaji Kiongozi, Salum Massati wa Mahakama Kuu, katika masjala ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.

Baada ya mawakili wa utetezi kumaliza kuwasilisha hoja zao za kuishawishi Mahakama iwaone washtakiwa hao hawakuwa na kesi ya kujibu na hivyo iwaachie huru Februari 4, 2009, siku iliyofuata, yaani Februari 5, 2009, upande wa mashtaka nao uliwasilisha hoja zake. Nini ambacho upande wa mashtaka ulikisema? Endelea...


Wakati upande wa utetezi katika hoja zake ulidai ushahidi wa upande wa mashtaka ulikuwa dhaifu na haukuweza kuwagusa washtakiwa kiasi cha kuwalazimu kujitetea, upande wa mashtaka kwa upande wake ulitamba kuwa ulikuwa umetekeleza vema jukumu lake la kuthibitisha mashtaka dhidi ya washtakiwa.

Jopo hilo la waendesha mashtaka katika hoja zake ulikuwa na jukumu la kuionyesha na kuishawishi Mahakama kuwa wameweza kuwasilisha ushahidi mzito na hivyo kujenga kesi dhidi ya washtakiwa, hivyo walikuwa na kesi ya kujibu jambo ambalo lililikuwa ni lazima wapande kizimbani kujibu mashtaka hayo au kujitetea.

Jopo hilo la waendesha mashtaka liliwasilisha hoja hizo kwa zamu, huku wakijaribu kuchambua ushahidi dhidi ya kila mshtakiwa na kuieleza Mahakama kuwa ni kwa namna gani ulikuwa umemgusa kila mshtakiwa.

Alianza kiongozi wa jopo hilo la waendesha mashtaka, Wakili wa kujitegemea kutoka jijini Arusha, Revocatus Mtaki. Katika hoja zake wakili Mtaki alianza kwa kusema, na ninamnukuu:

“Mheshimiwa Jaji na Waungwana Wazee wa Baraza, tumesikiliza hoja za wenzetu mawakili wasomi wa utetezi, nasi sasa tunataka kuionyesha Mahakama yako Tukufu kuwa ushahidi wetu tuliouwasilisha umekidhi matakwa ya kifungu cha 293 (1) cha CPA (Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai).

Kwa ushahidi wa mashahidi 37 pamoja na vielelezo 23 tulivyoviwasilisha mahakamani hapa, tunaamini mshtakiwa wa kwanza mpaka wa 13 wana kesi ya kujibu kwa vifo vya marehemu (watu) wanne.

Tunaamini hata wakinyamaza au wakijitetea kwa ushahidi huu Mahakama itawatia hatiani. Sheria inataka upande wa mashtaka kuthibitisha kwanza, kwamba marehemu (watu) wamekufa vifo visivyo vya kawaida, kwamba ni washtakiwa ndio waliowaua na kuonyesha walifanya hivyo kwa nia ovu ya kuua au kusababisha majeraha.

Katika kuthibitisha vifo kutokuwa vya kawaida, ni wazi kwamba kupitia PW19 (Dk Martin Phillip Mbonde na vielelezo vyake taarifa ya uchunguzi wa chanzo cha vifo zilizowasilishwa hapa mahakamani, wote wanne walipigwa risasi kisogoni na kutokea usoni.

Lakini pia kuna ushahidi wa PW4 (4th Prosecution Witness – Shahidi wa nne upande wa mashtaka) Venance Mchami; PW5, Jane Joseph (mkewe Mchami) na PW17, Emmanuel Ekonga (ambao walishuhudia majeraha wakati walipokwenda kutambua miili ya wachimba madini hao na dereva teksi kabla ya kutiwa mbaroni na askari polisi).

Pia mshtakiwa wa 11 na wa 12 kwa vielelezo (maelezo yao ya maandishi yalipokewa mahakamani kama vielelezo vya ushahidi ambao walieleza wachimba madini hao waliuawa katika Msitu wa Pande, Mbezi Luis wilayani Kinondoni, kwa kupigwa risasi shingoni kwa nyuma) walithibitisha hivyo.

Kuhusu hoja ya Msomi Wakili Magafu (Majura) ya identification (gwaride la utambuzi wa watuhumiwa) kwa madai kuwa askari watuhumiwa (waliohusika tangu tukio la kuwatia mbaroni wachimba madini walikuwa wengi, na kwamba hawakutambuliwa na shahidi.

Ushahidi wa kuwatambua hawa 13 ni mwingi. Kuna PW 24 SSP (Mrakibu Mwandamizi wa Polisi) Sebastian Masinde, aliyekuwa mkuu wa kituo cha Polisi Chuo Kikuu, akiungwa mkono na msaidizi wake PW14 aliwatambua washtakiwa waliotoka kituo cha Polisi Chuo Kikuu.

Hao ni mshtakiwa wa nne, Noel; (sita) Nyangelera; (saba) Emmanuel Mabula; (nane)Felix Sandy Cedrick; (tisa) Michael Shonza na (13), Festus Gwabisabi.

Waliotoka kituo cha Polisi Urafiki, walitambuliwa na PW23, SP (Mrakibu wa Polisi) Juma Ndaki, aliyekuwa mkuu wa kituo hicho (OCS).

PW23 aliwataja mshtakiwa wa tatu ASP (Mrakibu Msaidizi wa Polisi) Ahmed Makelle; wa tano, WP Jane Andrew na wa 10, Abeneth Saro, kuwa ndio waliokwenda kwenye tukio la Bidco (tukio la uporaji fedha katika gari la makusanyo ya mauzo ya bidhaa za kampuni ya Bidco.

SP Ndaki alieleza kuwa alipigiwa simu na ASP Makelle kuwa wamekamata majambazi.

PW2, Benadetha Limbu, PW6 Mjatta Kayamba George na PW7 Hadija Chaka, walieleza jinsi gari la Polisi Urafiki lilivyofika likiwa na askari mwanamke na wawili wanaume na kuunga na gari la Polisi kutoka Chuo Kikuu, ambalo lilitambuliwa na SP Ndaki (lile la Urafiki)

Waliotoka kituo cha Polisi Oysterbay walitambuliwa na PW15, Xavery Kajela, mtunza ghala la silaha Oysterbay kuwa waliokuwa zamu tarehe hiyo ni mshtakiwa wa 12, Rajabu Bakari; 11, Rashidi Lema; Saada, aliowagawia silaha na pia PC Joseph; PC Samson Jackson.

Hakuna ubishi waliongozwa na mshtakiwa wa pili, SP Bageni (aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Kinondoni). PW27 ACP (Kamishna Msaidizi wa Polisi) Maxmilius Ubisimbali na PW30 ACP Mmari ambao walielezwa na mshtakiwa mwenyewe.

Vielelezo D6 taarifa ya uchunguzi wa unyang’anyi washtakiwa wote isipokuwa wa pili walikubali kuwapo na mapambano katika ukuta wa Posta walivyodai.

Kwa ushahidi uliopo haina ubish kuwakamata na kuwasababishia vifo. Haikuwa na haja ya identification parade, kwa sababu washtakiwa wanakubali labda kama wangekataa.

Kuua: PW2 Benadetha, PW6 na PW7 waliwaona marehemu (wachimba madini – kina Jongo) wakikamatwa na kupekuliwa mmoja mmoja, pistol yao ikachukuliwa na washtakiwa pamoja na mfuko mweusi, wakafungwa pingu, wakawekwa ndani ya gari ya Pick-up na kuondoka nao.

Rejea taarifa ya mshtakiwa wa tatu kwa PW23 SSP Ndaki. Ni tukio la Januari 14,2006, jioni kesho yake marehemu (kina Jongo) hawakuonekana hotelini walikofikia. PW1, (mchimbaji madini mwenzao na kina Jongo) Alex Mathew Ngonyani, aliwatafuta kwa simu hakuwapata.

PW4, PW5 waliwatafuta katika vituo vyote vya Polisi hawakuwapata. Kesho yake miili yao ikapatikana Hospitali ya Taifa Muhimbili wamekufa kwa risasi.

Mheshimiwa Jaji, kwa kuwa walikamatwa na washtakiwa na kwa kuwa walikutwa wamefariki wakiwa chini ya ulinzi wa washtakiwa, washtakiwa wanapaswa wasimame waeleze walikufaje au waliwatorokaje mpaka wakapigwa risasi na watu wengine.

Usikose sehemu ya 60 kesho katika mwendelezo wa hoja za upande wa mashtaka kuona namna gani walivyojibu hoja za mawakili wa utetezi katika kuishawishi Mahakama iwaone washtakiwa kuwa wana kesi ya kujibu.