JICHO LETU MAHAKAMANI: Shahidi atoa majibu tata sampuli ya damu (49)

Saturday April 03 2021
SHAHIDIPIC

Aliyekuwa Kamishina Msaidizi wa Polisi, Abdallah Zombe akizungumza na mwanasheria wake, Richard Rwengeza(kushoto) katika Mahakama ya Rufaa, Dar es Salaam jana. Picha ya Maktaba

By James Magai

Jana katika sehemu ya 48 ya mfululizo wa simulizi ya kesi ya mauaji ya wafanyabiashara watatu wa madini na dereva teksi tuliona Mahakama Kuu ikitaa kupokea kielelezo cha picha zilizopigwa eneo la mauaji kwa kuwa uwasilishwaji wake haukufuata utaratibu wa kisheria.

Tuliona pia ndugu wa mshitakiwa wa kwanza na aliyekuwa mkuu wa upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Abdallah Zombe wakiwashutumu waandishi wa habari katika walichodai kumwandika na kumpiga picha ndugu yao kuliko wanavyofanya kwa washitakiwa wengine.

Katika kesi hiyo, Zombe na askari wenzake 12 walishitakiwa kwa kuwaua kwa makusudi wachimba madini kutoka Mahenge mkoani Morogoro ambao ni Sabinus Chigumbi na mdogo wake Ephraim Chigumbi, Mathias Lunkombe pamoja na dereva teksi aliyekuwa akiwaendesha, Juma Ndugu.

Upande wa mashitaka ulidai kuwa askari waliwapiga wafanyabiashara hao risasi shingoni na sehemu mbali mbali za miili yao katika Msitu wa Pande, Mbezi Luis, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam usiku wa Januari 14 mwaka 2006, baada ya kuwatia mbaroni eneo la Sinza Palestina wakihusishwa na uporaji wa fedha katika gari la kampuni ya Bidco. Endelea…

Kikao cha tatu cha usikilizaji wa kesi hiyo kilianza Septemba 22 hadi 26 mwaka 2008 na ndicho upande wa mashitaka ulifunga ushahidi wake. Jumla ya mashahidi watano walitoa ushahidi wao mbele ya mahakama.

Shahidi wa kwanza katika kikao hicho ambaye ni wa 33 katika kesi hiyo alikuwa ni Stafu Sajenti mpelelezi Nickobay Mwakajinga. Huyu alikuwa ofisa wa polisi kutoka makao makuu kitengo cha upelelezi ambaye jukumu lake kubwa lilikuwa kuchora ramani za maeneo ya matukio ya uhalifu mkubwa.

Advertisement

Kwa mujibu wa ushahidi alioutoa Septemba 22 mwaka 2008, alisema Januari 23 mwaka 2006 alikwenda kuchora ramani ya maeneo matatu tofauti ya matukio yaliyokuwa yakihusishwa na mauaji hayo akiambatana na mshtakiwa wa pili, SP Christopher Bageni.

Maeneo hayo ni Sinza C, mahali ambako wachimba madini hao wakiwa pamoja na dereva teksi aliyekuwa akiwaendesha walitiwa mbaroni na washitakiwa.

Eneo lingine alikochora ramani ni Barabara ya Sam Nujoma karibu na lilipokuwa banda la kampuni ya Konoike, mahali lilikotokea tukio la uporaji fedha katika gari la makusanyo ya mauzo ya bidhaa mbalimbali za kampuni ya Bidco ambalo wachimba madini hao walituhumiwa kulishambulia kisha kutokomea na fedha zilizokusanywa siku hiyo.

Pia Sajenti Nickobay alichora ramani ya eneo la ukuta wa Shirika la Posta lililopo Sinza, mahali ambako Jeshi la Polisi lilidai ndipo yalipotokea mapambano ya risasi na wale waliowaita majambazi ambao ni wachimba madini hao na askari polisi yaliyosababisha mauaji ya wachimbaji.

Katika ukuta huo alionyeshwa mashimo manne ambayo yanadaiwa yalitokana na risasi za askari polisi walipokuwa wakikabiliana na waliowaita majambazi na akaonyesha mahali wahanga (marehemu wachimba madini hao) walikoangukia baada ya kupigwa risasi ati wakijaribu kuruka ukura huo.

Mahali hapo alibaini kuwapo kwa madoa manne ya damu. Alichimba kidogo udongo wa maeneo hayo yaliyokuwa na madoa yaliyodaiwa kuwa damu za binadamu, na akauweka katika mfuko wa nailoni na kurudi nao ofisini.

Baada kuonyeshwa eneo hilo, baadaye aliwahoji watu waliokuwa katika gereji pamoja na waliokuwa katika kisima cha kuuza maji, ambavyo vilikuwa jirani na ukuta huo mahali yalikodaiwa kutokea mapambano ya risasi akitaka kujua zaidi kuhusiana na kuwapo kwa tukio la kurushiana risasi.

Hata hivyo, mashahidi hao aliowahoji walisema hawakuwahi kushuhudia mapambano ya namna hiyo wala kusika milio ya risasi mahali hapo.

Februari 22 mwaka 2006 aliitwa tena na Kamishna Msaidizi Mwandamzi wa Polisi (SACP), Sidney Mkumbi aliyekuwa kiongozi wa timu ya polisi ya upelelezi wa tukio la mauaji hayo iliyoundwa na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), kama Tume ya Jaji Mussa Kipenka iliyoundwa na Rais Jakaya Kikwete kuchunguza mauaji hayo ilivyokuwa imeelekeza.

Hivyo SACP Mkumbi alimtaka shahidi huyo, Sajenti Nickobay aambatane na timu hiyo katika maeneo mbalimbali yaliyokuwa yakihusishwa katika tukio la mauaji ya wachimba madini hao, yakiwamo maeneo yale matatu aliyokuwa ameelekezwa na kuonyeshwa na SP Bageni.

Maeneo mengine yalikuwa ni katika Msitu wa Pande uliopo Mbezi Luis wilayani Kinondoni, mahali mauaji hayo yalikofanyika na katika bonde la machimbo ya mchanga Bunju ambako washtakiwa wawili na mwenzao aliyetoroka waliagizwa na SP Bagen ili wampelekee maganda ya risasi zilizotumika huko ukuta wa Posta kwenye mapambano ya askari polisi na waliowaita majambazi.

Wakati wa madodoso (maswali ya udadisi kutoka kwa mawakili wa utetezi), shahidi huyo alikiri kuwa katika maelezo yake aliyoyatoa polisi, hakutaja uwepo wa mshtakiwa wa kwanza (Zombe).

Hivyo alilazimishwa na wakili wa Zombe, Jerome Msemwa kuyawasilisha mahakamani maelezo yake hayo yawe kielelezo cha utetezi.

Hata hivyo, shahidi huyo alikana kwenda eneo la tukio la Msitu wa Pande na Bunju, badala yale alisema kuwa alichokifanya yeye ni kuchora ramani ya maeneo hayo ya uhalifu kutokana na ramani isiyo rasmi iliyochorwa na kukabidhiwa kwake na Stafu Sajenti Moja (shahidi wa 32).

Pia shahidi huyo alikiri kuwa mbali na mafunzo ya msingi ya kozi za upolisi, hakuwa na mafunzo maalumu ya uchoraji ramani isipokuwa kipaji binafsi ndicho kilichomwezesha kutekeleza majukumu aliyokuwa anapangiwa na wakuu wake wa kazi.

Vilevile alikiri kuwa, mbali na SP Bageni aliyemwongoza katika matukio hayo, hakuna mshtakiwa mwingine ambaye alikuwapo wakati wa utembeleaji wa maeneo hayo ya matukio ya uhalifu na kwamba maeneo yote ambayo yeye alihusika kuchora ramani (Pande na Bunju) yalitokana na ramani aliyoichora Sajenti Moja na kukabidhiwa michoro hiyo ambayo haikuwa rasmi ili kuikamilisha.

Lakini, shahidi huyo alikiri kumkabidhi Mkemia Mkuu wa Serikali sampuli za damu alizozichukua eneo la tukio, pale ukuta wa Posta Sinza kwa ajili ya uchunguzi na uchanganuzi wa kitaalamu kama inavyotakiwa ili kukamilisha na kuthibitisha ushahidi huo.

Alibainsha kwamba alikuwa na taarifa kuwa matokeo ya uchunguzi wa Mkemia Mkuu yalionyesha sampuli za damu ile ilikuwa mchanganyiko wa damu ya binadamu na ya mnyama, lakini hakuwahi kuiona taarifa hiyo kwani haikumfikia.

Wakati akiongozwa na mwendesha mashtaka, Wakili Kaishozi kutoa majibu ya ufafanuzi wa hoja zilizokuwa zimeibuliwa, shahidi huyo pamoja na mambo mengine alieleza kuwa ingawa hakuwa na mafunzo maalumu ya uchoraji ramani, uchoraji ni sehemu ya mafunzo ya msingi yanayotolewa chuoni kwa kila askari polisi kumsaidia kwenye shughuli zake atakapokuwa kazini.

Pia shahidi huyo alieleza kuwa ingawa yeye mwenyewe hakwenda katika Msitu wa Pande wala Bunju, lakini shahidi wa 32, Sajenti Moja, aliyekwenda kupiga picha katika maeneo hayo ya matukio, alimwelezea mazingira muhimu ya mahali husika na yeye akakadiria vipimo kwenye ramani aliyoiandaa na kuiwasilisha mahakamani hapo kwa ajili ya ushahidi.

Hivyo alieleza kuwa kutokana na maelezo hayo aliweza kukamilisha ile ramani ya awali aliyokuwa ameichora Sajenti Moja.

Shahidi huyo alisisitiza kuwa kwa uzoefu wake haihitaji kuwepo mtuhumiwa au mshtakiwa wakati wa kuchora ramani ya eneo la tukio la uhalifu.

Akihojiwa na wazee wa baraza, shahidi huyo alieleza kuwa mshtakiwa wa pili, SP Bageni alimweleza kuwa askari waliorushiana risasi na wale waliowaita majambazi walitoka kituo cha Oysterbay.

Kuhusu matone ya damu yaliyokutwa eneo la tukio, alisema yalikuwa yametawanyika kwa wastani wa umbali wa sentimita 30 kutoka moja hadi lingine.


Advertisement