Jina la mrithi wa Maalim Seif tayari

DC Ubungo ataka utaratibu kwa wafanyabiashara stendi ya Magufuli

Muktasari:

  • Uongozi wa ACT-Wazalendo, umesema umekamilisha mchakato wa kumpata mwanachama atakayemrithi Maalim Seif Sharif Hamad kwenye nafasi ya umakamu wa kwanza wa rais wa Zanzibar. Kinachosubiriwa ni Dk Mwinyi kufanya uteuzi huo.

Dar es Salaam. Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amesema chama hicho kimeshapendekeza jina la mwanachama atakayemrithi  Maalim Seif Sharif Hamad umakamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.

Maalim Seif alifariki dunia Februari 17 mwaka huu wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), alikokuwa akipatiwa matibabu tangu Februari 9, mwaka huu.

Zitto ambaye aliwahi kuwa mbunge kwa miaka 15 ameeleza hayo jana  Jumamosi Februari 27,2021 wakati wa hitma ya kumuombea Maalim Seif katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini hapa.

Katika maelezo yake, Zitto alisema kilichobaki ni kusubiri uteuzi utakaofanywa na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi kwa mujibu wa Katiba.

“Bahati nzuri, Maalim Seif alikuwa ni kiongozi. Alijua kuna siku Mungu atamchukua kwa sababu sisi sote lazima turejee kwa  Mungu kama tulivyoambiwa katika mafunzo ya dini.

“Kwa hiyo aliacha maelekezo ya nini kitokee iwapo atatangulia mbele ya haki. Namshukuru Mungu kwamba viongozi wa chama wamefuata yale maelekezo yake kwa namna ambayo alivyotuelekeza sasa umebaki wajibu wa Dk Mwinyi kuyatekeleza hayo,” alisema Zitto.

Zitto amesema chama hicho kinaamini mwanachama aliyependekezwa ana uwezo wa  kusimamia maridhiano na haki za Wazanzibari kama ambavyo Maalim Seif alivyokuwa akifanya.

“Tunawaomba muendelee kutuombea dua ili tusitoke kwenye mstari, tuendelee kupigania demokrasia, haki na kuhakikisha kuwa nchi yetu inaendelea kuwa ya amani ili iweze kupata maendeleo ya watu."alisema Zitto.