Jinamizi la ajali nchini...'Wachawi' watajwa

Gari aina ya Coaster iliyokuwa imebeba maiti ikisafirisha kwenda kuzika mkoani Kilimanjaro baada ya kupata ajali iliyoua watu 20 wilayani Korogwe, Tanga.

Dodoma/Rombo. Wakati la ajali za barabarani zikiendelea kugharimu maisha ya watu, wengine kujeruhiwa na au kupata ulemavu wa kudumu, wabunge wametaja sababu zinazochangia hali hiyo ikiwemo rushwa kwa baadhi ya askari wa usalama barabarani.

Pia, kitendo cha wa wanasiasa kuingilia utekelezaji wa sheria ya usalama wa barabarani ni miongoni mwa sababu hizo na hivyo kushauri hatua za makusudi zichukuliwe ili kukomesha hali hiyo.

Wabunge wamebainisha hayo katika kipindi ambacho Taifa limepata msiba kufuatia ajali iliyosababisha vifo vya watu 20, wakiwemo 14 wa familia moja wilayani Rombo, Mkoa wa Kilimanjaro.

Ajali hiyo ilitokea usiku wa Jumamosi, eneo la Magira Gereza, Korogwe, mkoani Tanga baada ya basi dogo abiri aina ya Toyota Coaster lililobeba waombolezaji 26 wanaliokuwa wanasafirisha mwili wa Atanas Mrema kwenda Rombo kwa maziko, kugongana uso kwa uso na Fuso.

Katika ajali hiyo, watu wanane walifariki papo hapo na wengine 12 kufariki kwa nyakati tofauti wakipatiwa huduma hospitalini. Miongoni mwa waliokufa watatu walikuwa wekute dereva pamoja na watatu walikuwa kwenye Fuso, akiwemo dereva.

Wakati mazishi ya marehemu na matibabu kwa majeruhi yakiendelea, jana bungeni Dodoma, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama iliwasilisha ya utekelezaji wa shughuli kwa kipindi cha kati ya Februari 2022 hadi Januari mwaka 2023, ikigusia suala la ajali kwa kiasi kikubwa.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Vita Kawawa alisema kwa kipindi cha Oktoba hadi Desemba, 2022, zilitokea ajali 281 ziliyosababisha vifo ikilinganishwa na 273 zilizoripotiwa katika kipindi kama hicho mwaka 2021, sawa na hilo ni ongezeko la ajali nane (asilimia 2.9).

Katika kipindi hicho mwaka jana idadi ya watu waliopoteza maisha ni 382 ikiongezeka kutoka 367 waliokufa kwa kipindi kama hicho 2021, sawa na asilimia 4.1.


Rushwa inavyochangia

Alisema uchambuzi uliofanywa na kamati ulionyesha kuwa ajali hizo zimekuwa zikichangiwa na baadhi ya askari wa usalama barabarani kujihusisha na rushwa na hivyo kushindwa kutimiza wajibu wao wa kushughulikia makosa ya barabarani.

Vilevile, Kawawa alitaja uhaba wa vitendea kazi kama vile magari ya doria katika barabara kuu, taa za kuongozea magari, vifaa vya kupima mwendokasi, upungufu wa kamera na vipima ulevi.

Jambo jingine, limetajwa kuwa ni “kukosekana kwa utashi wa kisiasa kwa baadhi ya wanasiasa na hivyo kuingilia utekelezaji wa Sheria za Usalama Barabarani.”

Akitolea mfano, Kawawa alitaja matukio ya kuwazuia askari kuwakamata bodaboda au bajaji wanapofanya uvunjifu wa sheria.

Alifafanua kuwa kitendo hicho kinaweza kusababisha madereva wa bodaboda kupata ulemavu wa kudumu na wengine kupoteza maisha kwa na ajali.

Alitumia fursa hiyo kuwataka wanasiasa kuacha kuliingilia Jeshi la Polisi huku akiliomba Bunge kuazimia kwamba “Serikali iendelee kudhibiti uendeshaji mbovu wa madereva wa pikipiki kwa kusimamia ipasavyo sheria”


Ubovu wa miundombinu

Kamati hiyo ya Bunge ilibainisha sababu nyingine inayochangia ajali kuwa ni ubovu wa baadhi ya barabara hali ambayo wakati mwingine husababisha ajali pamoja na hulka za kibinadamu za kuamini kuwa ajali hazina kinga.

Suala la miundombinu mibovu, liliungwa mkono na Balozi wa Usalama Barabarani (RSA), Rama Msangi aliyesema ni miongoni mwa vitu vinavyotakiwa kufanyiwa kazi ikiwemo kuwa na barabara zenye upana wa kutosha.

Msangi mwenye ithibati ya kimataifa ya mambo ya ukaguzi wa miundombinu ya barabara, alisema lazima ziwe pana zinazoruhusu magari mawili kupita pasipo vikwazo, zikiwa na eneo linalogawa barabara katikati yaani mstari unaotambulika, msingi au uzio fulani ambao utamfanya dereva wa upande mmoja asihamie upande mwingine.

“Ajali ya Korogwe dereva asingeweza kuhamia upande mwingine kama kungekuwa na miundombinu rafiki,” alisema Msangi.


Madereva wasio na sifa

Mbunge huyo wa Namtumbo alitaja sababu nyingine ni madereva wengi wasio na sifa kutokana na mfumo wa utoaji leseni za udereva kutoa mwanya kwa wasio na sifa ya kupata leseni.

Kawawa aliliomba Bunge kuzimia Serikali ianze mchakato wa kuutazama upya mfumo uliopo wa utoaji leseni za udereva ili kuwa na mfumo imara ambao utatoa fursa kwa madereva waliokidhi vigezo kupata leseni.

Kuhusu wimbi la magari kufunga ving’ora, Kawawa alisema kamati ilibaini katika siku za karibuni kumeibuka wimbi la magari ya watu, taasisi binafsi na za umma, kufungwa ving’ora na vimulimuli kinyume na utaratibu ilihali wakiwa hawana uelewa wa kutosha kuhusu suala hilo.

Alisema hali hiyo inahatarisha usalama kwa watumiaji wengine wa barabara.

Machi 14 mwaka jana, aliyekuwa Kamanda wa Polisi, Kikosi cha Usalama Barabrani, Wilbroad Mutafungwa lilitangaza kupiga marufuku matumizi ya ving’ora na vimulimuli kwa watumiaji wa magari binafsi bila kibali

Taarifa ya Mutafungwa aliyoitoa wakati huo ilisema kama mtu ana dharura anahitaji kutumia ving’ora anatakiwa kuomba kibali wizara ya mambo ya ndani au Jeshi la Polisi, ambapo ataruhusiwa atasindikizwa kwa kutumia ving’ora.