Prime
Jinsi mkaa usiolipiwa ushuru unavyopita ‘njia za panya’ kuingia sokoni
Pikipiki zikiwa zimebeba magunia ya mkaa. Picha na Mtandao
Shinyanga. Wakati ripoti ya ‘The Potential and Optimal Strategies for Charcoal Sub-Sector Development in Tanzania 2019’ ikionyesha asilimia 95 ya mkaa unaozalishwa na kusafirishwa kutoka Shinyanga huingia sokoni kinyume cha sheria, swali kubwa linalozuka ni namna bidhaa hiyo inavyofanikiwa kufika katika masoko ya mijini licha ya uwepo wa vituo vya ukaguzi na mifumo mingine ya udhibiti.
Uchunguzi wa Mwananchi katika vijiji vya Tinde, Samuye, Ishina Bulaindi na maeneo mengine ya jirani umebaini kuwa sehemu ya jibu la kitendawili hicho ipo katika matumizi ya mtandao wa njia zisizo rasmi zinazojulikana kama njia za panya, kusafirisha mkaa kutoka maeneo ya uzalishaji hadi kwenye masoko huku zikikwepa vituo vya ukaguzi wa mazao ya misitu.
Kila alfajiri na jioni katika maeneo hayo, misururu ya baiskeli na pikipiki zilizobeba magunia ya mkaa huanza kuondoka kwenye maeneo ya uzalishaji mara tu giza linapoanza kuingia, zikielekea Shinyanga Mjini na masoko mengine ya karibu.
Tofauti na inavyoweza kudhaniwa, wasafirishaji hao hawatumii barabara kuu ambako kuna vituo vya ukaguzi vya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS).
Badala yake, hutumia njia za porini na mashambani ambazo kwa miaka mingi zimejengeka na kuwa mtandao mbadala wa usafirishaji unaoendesha biashara hiyo sambamba na mfumo rasmi wa udhibiti.
Hata hivyo, kuna baadhi ya maeneo wasafirishaji hao hukatiza kwenye barabara kuu kuelekea manispaa ya Shinyanga mfano eneo la Tinde na Ishina Bulaindi kabla ya kurudi tena kwenye njia za panya kuendelea na msafara wa kupeleka mkaa haramu manispaa ya Shinyanga.
Kinachovutia zaidi ni namna usafirishaji huo unavyofanyika kwa utaratibu unaofanana kila siku. Wakazi wa maeneo hayo wanasema mtiririko wa mkaa umekuwa wa kawaida, unaotabirika na mara nyingi haukatizwi licha ya uwepo wa vituo vya ukaguzi na doria za maofisa wa misitu mara kwa mara.
Kwa mujibu wa Sheria ya Misitu, Sura ya 323, Toleo Lililofanyiwa Marejeo la Mwaka 2023, uvunaji wa mazao ya misitu kwa ajili ya biashara unahitaji kibali kinachotolewa na maofisa wa misitu wenye mamlaka.
Aidha, Kifungu cha 89 cha sheria hiyo kinakataza usafirishaji wa mazao ya misitu yaliyovunwa kinyume cha sheria.
Vilevile, Kanuni za Misitu (marekebisho) za mwaka 2022 zinataka mkaa wote unaosafirishwa kuambatana na hati halali ya usafirishaji (Transit Pass) inayothibitishwa katika vituo rasmi vya ukaguzi vya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS).
Majukumu ya utekelezaji wa sheria hizo yapo mikononi mwa maofisa wa misitu na wahifadhi wa TFS wenye jukumu la kukagua mizigo, kukamata mazao ya misitu yaliyopatikana kinyume cha sheria na kuzuia usafirishaji usioruhusiwa.
Hata hivyo, hali halisi iliyoonekana katika maeneo ya Shinyanga inaonyesha kuwa sehemu kubwa ya usafirishaji wa mkaa bado inafanyika nje ya mfumo huo wa udhibiti.
Wasafirishaji waliozungumza na Mwananchi katika Kata ya Tinde wanasema kukwepa vituo vya ukaguzi si jambo la bahati mbaya bali ni mkakati unaopangwa kwa makusudi.
"Hatuendi karibu na vituo vya ukaguzi kwa sababu bila nyaraka lazima ushikwe," anasema msafirishaji wa mkaa, Dotto Leonard.
Anasema, "Ndiyo maana tunatumia njia za porini ambako hakuna maofisa. Tunafahamu vituo vyote vya ukaguzi, ndiyo maana si rahisi kutukamata."
Katika maeneo ya Samuye, Ishina Bulaindi, Nhelagani na Buhangija, wakazi wanasema baiskeli zinazobeba hadi magunia manne ya mkaa pamoja na pikipiki zinazosafiri kwa makundi zimekuwa uti wa mgongo wa usafirishaji wa bidhaa hiyo kuelekea mijini.
"Huwezi kubeba mzigo wa aina hiyo ukiwa peke yako. Tunaongozana kwa makundi na kusaidiana pale njia inapokuwa na changamoto za kupita au kukutana na maafisa wa TFS," anasema Leonard Dotto, mkazi wa Samuye.
Mbali na kutumia njia zisizo rasmi, muda wa usafirishaji nao hupangwa kwa makini. Baadhi ya wasafirishaji wanasema safari nyingi huanza saa 11 jioni wakati doria za TFS zinapopungua ili kuepuka usumbufu wa kukimbizwa au kukamatwa.
Ingawa mfumo huo umejengwa ili kukwepa kukamatwa, wakati mwingine wasafirishaji hao hukumbana na maofisa wa utekelezaji wa sheria.
"Wakati mwingine wanatufukuza kwa magari hasa maeneo ambayo tunatokeza kwenye barabara kuu," anasema mmoja wa waendesha pikipiki wanaojihusisha na usafirishaji wa mkaa katika Kata ya Tinde bila kutaja majina yake.
Mwenzake waliokuwa wameongozana, aliiambia Mwananchi kuwa, "Ukijaribu kukimbia wanaweza kutumia nguvu zaidi kwa kuku-push ili uanguke na mzigo wako kisha wanashuka na kukukamata."
"Wakikukamata unapoteza kila kitu, kuanzia mkaa hadi pikipiki au baiskeli uliyokuwa unatumia, kuna wengine wanapata hadi vilema japo hakuna mwenzetu ambaye alishawahi kuuawa," anasema.
Licha ya hatari hizo, wengi wao wanasema hali ngumu ya maisha ndiyo inayowasukuma kuendelea na shughuli hiyo.
Mzalishaji wa mkaa, Mponhela Jumanne, anasema wakazi wengi hasa wa kata ya Tinde hawana shughuli mbadala za kuwaingizia kipato ndio maana wamejikita kwenye biashara ya mkaa.
"Maisha yetu yanategemea kukata miti, kuchoma na kuuza mkaa kwa sababu fursa nyingine ni chache. Hata waliojaribu kufuata utaratibu wa vibali wanasema si rahisi kuvipata," anasema.
Mbali na njia za usafirishaji, mtandao huo pia unahusisha maeneo ya kukusanyia mkaa kutoka sehemu mbalimbali kabla ya kupelekwa katika masoko ya mwisho.
Akizungumza katika mahojiano hayo Mwenyekiti wa Kitongoji cha Nyambui, Kata ya Tinde, Masesa Chaula, anasema mkaa kutoka Shinyanga na maeneo jirani ikiwemo Nzega mkoani Tabora hukusanywa kabla ya kuendelea na safari kuelekea masoko makubwa.
Anasema usafirishaji huo kwa kiasi kikubwa hutegemea makubaliano yasiyo rasmi yanayoamua mzigo unaweza kuendelea kwa umbali gani.
"Wafanyabiashara hununua mkaa na wanapofika geti la Usanda, (kata ya Wilaya ya Shinyanga Vijijini katika Mkoa wa Shinyanga) hulipa takribani Sh4,000 kwa kila gunia na kuruhusiwa kuendelea na safari kuelekea Shinyanga," anasema.
Kwa mujibu wake, mfumo huo huacha taswira ya uwepo wa udhibiti wakati sehemu kubwa ya usafirishaji haijapitia uhakiki kamili unaotakiwa na sheria.
Chaula pia anaeleza wasiwasi wake kuhusu ushirikishwaji mdogo wa viongozi wa vijiji na vitongoji katika kudhibiti biashara hiyo.
"Mara nyingi sisi hatuhusishwi. Tunaona vituo vya ukaguzi lakini mamlaka za misitu hazishirikiani sana na viongozi wa vijiji," alisema.
Aliongeza kuwa licha ya jamii za maeneo hayo kuwa kitovu cha uzalishaji na usafirishaji wa mkaa, hazipati manufaa ya moja kwa moja kutoka katika biashara hiyo.
"Hatupati chochote kutokana na biashara hii," anasema.
Wakati biashara ikiendelea kukua, athari zake kwa mazingira zimeanza kuonekana wazi katika maeneo mengi ya uzalishaji.
"Zamani tulikuwa na miti mingi, lakini sasa maeneo ya wazi yanaongezeka. Joto limeongezeka na hata mvua si za uhakika kama ilivyokuwa zamani na kuna muda mwingine zikija zinakua nyingi isivyo kawaida," anasema mkazi wa eneo hilo, Rebeka Hamduni.
Naye Rajabu Njige anasema ukataji miti unaathiri hata shughuli za kilimo.
"Miti inapotea kwa sababu mkaa umekuwa biashara kubwa. Hata hali ya udongo imeanza kubadilika, siku hizi hatupati mazao mengi na bora ukilinganisha na miaka kumi nyuma," anasema.
Walichokisema TFS
Kwa upande wake, Ofisa Misitu wa Wilaya ya Shinyanga na Mhifadhi Mwandamizi, Fabian Balere, anasema TFS inaendelea kufanya operesheni za ukaguzi, kutumia mifumo ya kidijitali na kuimarisha vituo vya ukaguzi ili kudhibiti usafirishaji wa mazao ya misitu.
Alikiri kuwa pamoja na jitihada hizo, bado kuna ukiukwaji wa taratibu za uvunaji na usafirishaji.
"Ukiukwaji wa taratibu za uvunaji na usafirishaji bado unaendelea kujitokeza, hasa katika usafirishaji wa mazao ya misitu," anasema.
Balere anasema Shinyanga pia ni njia ya kupitisha mazao ya misitu yanayotoka maeneo mengine, jambo linalofanya kazi ya udhibiti kuwa na changamoto zaidi.
Anasema maofisa wa TFS wana wajibu wa kukagua nyaraka, kuhakiki hati za usafirishaji na kuchukua hatua dhidi ya mizigo inayobainika kuwa haramu, ikiwemo kuikamata.
Hata hivyo, anakiri kuwa njia zisizo rasmi zinazotumiwa na wasafirishaji zimeendelea kuwa changamoto ya ufanisi wa vituo vya ukaguzi.
"Ingawa tuna vituo vya ukaguzi na mifumo ya udhibiti, bado kuna usafirishaji unaofanyika nje ya njia rasmi tunazozifuatilia," anasema.
Anaongeza kuwa TFS itaendelea na kampeni za uhamasishaji pamoja na operesheni za utekelezaji wa sheria, lakini kuendelea kwa ukiukwaji huo kunaonyesha kuwa changamoto iliyopo si ya kiutendaji pekee bali inahitaji ushirikiano mpana wa wadau wote katika mnyororo wa biashara ya mkaa.
“Ni jambo ambalo tunapigana nalo usiku na mchana kulimaliza na hali inaendelea kuimarika kila siku,” anasema.