Jinsi wajawazito walivyopambana na corona

Jinsi wajawazito walivyopambana na corona

Muktasari:

Ni jukumu la mjamzito kumlinda mtoto aliyepo tumboni  kwa sababu hutegemea vitu vingi kutoka kwa mama tofauti na anapokuwa amezaliwa.

Ni jukumu la mjamzito kumlinda mtoto aliyepo tumboni  kwa sababu hutegemea vitu vingi kutoka kwa mama tofauti na anapokuwa amezaliwa.

Ugonjwa wa corona ni kati ya magonjwa yaliyowafanya wanawake kuwa makini kuhakikisha hawapati maambukizi lengo likiwa ni kuwalinda watoto.

Kupunguza mizunguko isiyo ya lazima, baadhi kupata hofu ya kwenda kliniki ni kati ya tabia mpya za wanawake zilizoibuka baada ya ugonjwa huo kushika kasi nchini takribani miezi sita iliyopita, wakihofia kupata maambukizi.

 “Nakumbuka Aprili mwaka huu sikuenda kliniki nikihofia ninaweza kupata maambukizi ya corona na hata kwenye  daladala. Nilijitenga ili niwe salama ilikuwa mbaya na siitamani hali ile tena,” alisema Veronica Lucas, mkazi wa Mtoni Kijichi ambaye hivi sasa mwanaye ana umri wa miezi miwili.

Alisema uamuzi aliouchukua kipindi hicho haujutii na ana amini kuwa ndio umemuweka salama.

Wakati  Veronica akieleza hayo, Justina Kitampa alisema kila ilipofika siku ya kwenda kliniki, mawazo yalikuwa hayabanduki kichwani.

“Kila nikijua kesho naenda hospitali na idadi ya wagonjwa ilivyokuwa ikiongezeka kila mara hofu inanijaa na nguvu zinaisha, nikiingia kwenye gari nakosa amani, inakuwa ni safari ya tahadhari sana.”

“Pamoja na hali yangu lakini nilivaa barakoa kwa sababu siamini kama naweza kuwa salama,” alieleza Veronica.

Jackline Sikazwe, akiwa na mimba yake ya kwanza ya miezi nane alisema alitarajia kipindi  hicho kingekuwa cha yeye kuwa karibu na watu anaowapenda lakini badala yake aliishia kuhisi unyanyapaa.

“Mume wangu ni daktari  kipindi hiki nilihitaji ukaribu wake lakini sikuupata, akirudi hataki nimsogelee sababu anahofia kuniambukiza corona, hadi aoge na kubadili nguo zake. Ni kipindi ambacho siwezi kukielezea,” alisema.

Wanawake hao wanawakilisha kundi kubwa la wajawazito waliokuwa wakipitia wakati mgumu, msongo wa mawazo na waliolazimika kuchukua tahadhari kubwa ili kuhakikisha wanakuwa salama wakati wakifuata huduma za afya katika kipindi cha corona.

Licha ya wao kuwa na hofu katika mioyo yao, hospitali zilijipanga kuhakikisha kuwa huduma zote kwa kina mama wajawazito na wanaojifungua zinaendelea kama kawaida, kwa haraka na ubora, zilizoenda sambamba na elimu itakayowaweka salama.

Mwananchi ilitembelea vituo vya afya na kufanya mazungumzo na wahudumu wa kitengo cha kina mama wajawazito ili kujua njia walizotumia kuwalinda huku wakipatiwa huduma bora.

Kwa mujibu wa mtoa huduma za kliniki kwa wajawazito katika moja ya hospitali jijini Dar es Salaam ambaye hakutaka jina litajwe, alisema moja ya njia iliyotumika lakini haikuonekana kuzaa matunda ni kuwashauri kina mama wajawazito kutumia hospitali zilizo karibu na makazi yao.

“Licha ya kuwaambia hivyo hawakuweza  kutekeleza. Wengi walikuwa wakisema hawawezi kwa sababu wamezoea hospitali hiyo na lengo la kufanya hivyo lilikuwa ni kuwapunguzia safari kwa sababu wengine walitokea mbali,” alieleza.

Mbali na hiyo, njia nyingine iliyotumika ilikuwa ni kuwarusha siku za kliniki baadhi ya kina mama ambao wanaonekana kuwa na afya njema na siku zao za kujifungua bado.

“Wengine tuliwapumzisha mwezi mmoja, wengine miwili ila tunampa dawa za kutumia zinazohitajika, hii ilisaidia kupunguza idadi yao katika kliniki zetu,” anasema mhudumu huyo.

Anaongeza kuwa kabla ya corona, hospitali anayofanyia kazi ilikuwa ikihudumia kina mama wajawazito zaidi ya 30 hadi 50, lakini baadaye idadi yao ilishuka hadi kufikia 20 na chini ya hapo.

“Huenda waliamua kutumia hospitali nyingine lakini hofu iliyokuwa imejengeka mioyoni mwao kuhusu coronai nayo ilizorotesha mahudhurio,” alisema 

Mhudumu huyo alibainisha kuwa hata utoaji wa huduma nao ulibadilika, “kina mama hao kulazimika kupita katika meza nyingi na vyumba tofauti, huduma zote zilitolewa katika eneo moja.”

“Hii ilisaidia kuondoa mizunguko na kumlazimisha kukutana na watu tofauti, akiingia katika chumba kimoja anapewa huduma zote akitoka anaondoka nyumbani.”

Kwa sharti la kutoitajwa jina mhudumu wa afya katika hospitali nyingine jijini Dar es Salaam alisema corona iliathiri mahudhurio ya wajawazito kliniki.

Alisema licha ya kuwawekea alama na kuwasisitiza kukaa kwa nafasi, na kutumia vitakasa mikono, bado wengi walikuwa na hofu ya kuhudhuria kliniki.

“Kutoka kina mama 60 kwa siku hadi 30 na pungufu ya hapo au mwingine anajipumzisha mwezi ambao haukumuambia, ukimuuliza anakuambia alikuwa anaumwa lakini kwa sababu tunajua hali halisi tunawaacha,” alisema.

Corona yaacha somo

Wauguzi hawa wanabainisha kuwa uwepo wa virusi vya corona imewasaidia kuona utoaji wa elimu ni suala la msingi kabla ya kuwapatia huduma wajawazito na watu wote walio na mahitaji.

Kupitia elimu ya corona ilikuwa ni rahisi kwao kuunganisha na elimu nyingine kwa kina mama hao ambazo huweza kuwalinda na magonjwa mengine ya kuambukiza.

“Yapo magonjwa mengi ambayo yanahitaji umakini wa kinamama hawa na kukumbushwa kila mara hivyo tunapowafundisha hususani uzingatiwaji wa usafi inakuwa ni fursa kwao kujilinda zaidi,” anaeleza mmoja wa wauguzi wa hospitali hizo.

Alisema corona imeacha somo kwa wanawake kuhusu umuhimu wa kupata chanjo kwa ajili ya kuwalinda watoto na kutambua kuwa endapo watapuuzia, wanaweza kuwafanya watoto kupata magonjwa.

“Hata sisi katika utoaji wa huduma tumejifunza namna ya kuwapa kipaumbele watu wenye mahitaji maalumu si wajawazito tu bali hata walio na magonjwa sugu kama virusi vya ukimwi, kifua kikuu, saratani kuwa ni vyema tujenge utaratibu wa kuwahudumia kwa haraka,” alisema.

Jinsi wajawazito walivyopambana na corona

Baada ya Kujifungua

Kwa mujibu wa wauguzi hao, kina mama walipojifungua na bado wako hospitalini, ndugu walikuwa hawaruhusiwi kumshika mtoto mchanga au hata kuwasogelea.

“Hawakuingia wodini, iliwekwa sehemu maalumu ambayo mama aliyejifungua huweza kusimama na wakapeana maagizo na kuelewana ili kuhakikisha kuwa afya ya mama na mtoto inakuwa salama,” anasema.

Licha ya uwepo wa virusi vya corona nchini na baadhi ya kina mama kushindwa kuhudhuria kliniki, takwimu zinaonyesha kuwa idadi ya wajawazito wanaohudhuria kliniki imeongezeka.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya, ongezeko hilo limechangiwa na kuimarishwa kwa ubora wa huduma za kliniki kwa wajawazito.

Hayo yamebainishwa kupitia taarifa ya Hali ya Huduma ya Afya ya Uzazi na Mtoto nchini Tanzania mwaka 2015/16 hadi 2019/20, iliyotolewa na aliyekuwa waziri wa wizara hiyo, Ummy Mwalimu kwa Wadau na Watoa Huduma za Afya Agosti 19, 2020.

Pia, kiwango cha wanawake wa wajawazito wanaojifungua kwenye vituo vya kutolea huduma kimeongezeka kutoka akina mama milioni 1.226 mwaka 2015 mpaka akinamama milioni 1.801 Juni 2020.

“Uboreshwaji huu pia umechangia kuongeza idadi ya wajawazito wanaoanza kliniki kabla ya majuma 12 kutoka 268,342 mwaka 2015/2016 hadi kufikia 738,006 Juni 2020,”

Hadithi hii iliungwa mkono na Kanuni ya WanaData Initiative ya Afrika, Twaweza na Kituo cha Pulitzer juu ya Kuripoti Majanga