Jinsi wanaodaiwa kumuua kiongozi Chadema walivyojitetea hadi usiku

Jinsi wanaodaiwa kumuua kiongozi Chadema walivyojitetea hadi usiku

Muktasari:

Mahakama kuu kanda ya Mwanza jana Jumatatu Desemba 14, 2020 ililazimika kusikiliza ushahidi wa watuhumiwa wa kesi ya mauaji ya aliyekuwa mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Geita na kanda ya Ziwa,  Alphonce Mawazo hadi saa 2:30 usiku.

Geita. Mahakama kuu kanda ya Mwanza jana Jumatatu Desemba 14, 2020 ililazimika kusikiliza ushahidi wa watuhumiwa wa kesi ya mauaji ya aliyekuwa mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Geita na kanda ya Ziwa, Alphonce Mawazo hadi saa 2:30 usiku.

Mawazo aliyegombea ubunge mwaka 2015 katika jimbo la Busanda aliuawa Novemba 14, 2015 katika mji mdogo wa Katoro wilayani Geita siku moja kabla ya uchaguzi wa udiwani katika kata ya Ludete.

Katika shauri hilo namba tisa la mwaka 2019 watuhumiwa wanne kati ya watano wanaokabiliwa na kesi hiyo wamekutwa na kesi ya kujibu huku mtuhumiwa wa nne,  Habibu Feruzi akiachiwa huru baada ya ushahidi uliotolewa mahakamani hapo kushindwa kuthibitisha kuhusika kwake kwenye mauaji hayo ya kukusudia.


Katika kesi hiyo iliyoanza saa nne asubuhi washtakiwa ni  Alfan Apolnari, Epafra Zakaria, Hashim Sharifu na  Kalulinda Bwire.

Akijitetea mahakamani hapo, Apolnari ambaye ni mchimbaji mdogo wa dhahabu ameieleza mahakama kuwa siku ya tukio alikuwa amelazwa katika zahanati ya Segese iliyopo wilayani Kahama akisumbuliwa na ugonjwa wa kutapika, kuharisha, typhod na malaria.

Mshtakiwa huyo amedai alipokamatwa hakuhojiwa na polisi na wala hakuandika maelezo yoyote mahakamani na kwamba saini iliyopo sio yake hivyo kuiomba mahakama imuachie huru kwakuwa ushahidi uliotolewa dhidi yake ni wa uongo.

Mtuhumiwa amemuomba hakimu kuchunguza kwa makini shauri hilo na mahakama itende haki na isiwaonee wanyonge kwa kuwa upande wa mashtaka wana jambo wanaficha na wanyonge katika kesi hiyo wanatolewa kafara.

Naye Zakaria amedai mahakamani hapo kuwa siku ya tukio alikuwa kwenye semina ya mawakala wa uchaguzi mdogo wa udiwani kata ya Ludete na baadaye alitoka na kwenda kuangalia mechi kati ya timu ya Taifa ya Tanzania iliyocheza dhidi ya Nigeria.

Ameiomba mahakama hiyo kuridhia kielelezo cha ushahidi ambacho ni fomu ya kiapo cha kutunza siri kwenye chumba cha uchaguzi.

Amesema kuwa ushahidi uliotolewa na shahidi wa nne na wa tisa unaomtia hatiani ni wa uongo na kuiomba mahakama kukubali ushahidi alioutoa yeye.

Hakimu mwandamizi mwenye mamlaka ya juu kusikiliza kesi za mauaji, Frank Mahimbali aliahirisha kesi hiyo hadi leo Jumanne Desemba 15, 2020 ambapo washtakiwa Sharifu na Bwire watajitetea.