Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Jiwe la msingi UVCCM lazua taharuki Mwanza

Mwonekano wa jengo lenye Ofisi ya Serikali ya Mtaa wa Bujimile Kata ya Nyamhongolo iliyopo katika Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza huku jiwe la msingi la Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) likiwa limejengwa mbele ya ofisi hiyo. Picha na Anania Kajuni

Muktasari:

  • Jiwe hilo lenye bendera na maandishi, limejengwa mbele ya Ofisi ya Serikali ya Mtaa wa Bujimile Manispaa ya Ilemela jijini Mwanza.

Mwanza. Wakati baadhi ya wakazi wa Mtaa wa Bujimile mkoani hapa wakipinga kuwepo kwa jiwe la msingi la Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) mbele ya ofisi ya serikali ya mtaa huo, chama hicho kimesema wao wamepanga karibu na ofisi hiyo. .

Jiwe hilo lenye bendera na maandishi yaliyoandikwa "Jiwe hili la vijana wa CCM Bujimile limezinduliwa Julai 28, 2024 na Ndugu Calorine Kabula Masanja, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Mwanza" limejengwa mbele ya ofisi ya serikali ya Mtaa wa Bujimile Manispaa ya Ilemela.

Kutokana na uwepo wa jiwe hilo,  Kiongozi wa Chama cha ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe alichapisha picha ya ofisi hiyo katika ukurasa wake wa X Oktoba 31, 2024, ikionesha  jiwe hilo, huku akitaka watendaji wa chama hicho nao kuweka kijiwe chao karibu na ofisi yao.

"CCM wamejenga kijiwe chao mbele ya ofisi ya serikali ya Mtaa wa Bujimile Kata ya Nyamhongolo hapa Ilemela. Nimewaelekeza viongozi wa ACT -Wazalendo wa kata hii,  waanze kujenga ngome ya ACT Wazalendo pembeni ya kijiwe hicho cha CCM kwani ofisi ya mtaa ni raia wote," alisema Zitto.

Akizungumza na Mwananchi, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ilemela, Yusuph Bujiku amesema kutokana na mtaa huo kutokuwa na ofisi umelazimika kupanga katika eneo hilo, ambalo pia zipo ofisi za UVCCM  ili kurahisisha upatikaji wa huduma.

"Ofisi ya Serikali ya Mtaa ya pale Bujimile imepanga pale kwa hiyo wao walipotafuta sehemu ya kupanga wakapata hapo, ambapo jirani yake kuna hilo tawi la chama,  sasa huwezi kumpangia mwenye nyumba kwamba umpangishe nani na yupi usimpangishe," amesema.

Naye Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela, Ummy Wayayu amesema baada ya kufuatilia amebaini pale ilipo wamepanga kwa muda lakini hata hivyo ameelekeza litafutwe eneo lingine.

"Nimefuatilia ile ofisi pale tumepanga kwa hiyo kama na hao wengine wapo pale kama wapangaji sisi hatuwezi kuwazuia na tayari nimeelekeza litafutwe eneo lingine tukapange," amesema Wayayu.

Baadhi ya wananchi waliozungumza na Mwananchi wameonesha kuchukizwa na kitendo hicho,  huku wakiomba jiwe hilo au ofisi moja iondolewe ili kuondoa sintofahamu.

"Mimi nimezoea kuona bendera za chama zinakuwa katika ofisi zao sio kwenye ofisi za Serikali, kwa sababu ile ni ya watu wote bila kujali chama chochote," amesema Elias Juma.

Mkazi wa Mtaa wa Ilamba Kata ya Nyamhongolo, Abdallah Kalori ameshauri uongozi wa chama hicho ngazi ya kata kutoa bendera hiyo mbele ya ofisi hiyo.

"Ukiangalia kwa makini ofisi za Serikali ya Mtaa zinaonekana hazina muda mrefu tangu zimejengwa, lakini hata bendera hiyo ya chama na yenyewe inaonekana haina muda mrefu,  najiuliza kwanini imekuwa hivyo?

“Zaidi nashauri waondoe bendera ya chama hicho katika eneo hilo kwani hizo ofisi hizo zinahudumia wananchi wote bila kujali chama na kibaya zaidi tunaenda kwenye uchaguzi inaweza kuja kuleta shida," amesema Kalori

Mwenyekiti wa ADC Taifa, Shaban Itutu amesema mbali na kukemea tabia hiyo ya kuweka nembo za chama kwenye ofisi za umma, lakini bado utekelezaji umekuwa mgumu hivyo kuzitaka mamlaka husika kusimamia vyema sheria ya vyama vya siasa inayokataza kufanya hivyo.

Akiunga hoja hiyo aliyekuwa mgombea ubunge Jimbo la Misungwi kwa tiketi ya Chadema, Shija Shimbi ameshauri jiwe hilo kuondolewa mbele ya ofisi hiyo au ofisi ihamishwe.

"Mimi nashauri ingehamishwa iwekwe eneo ambalo halitakuwa na mgongano wa namna hiyo kwa sababu ukijenga hivyo inamaanisha mpo pale na nyie ndio mna umiliki kitu ambacho sio sahihi," amesema Shija.

Kwa mujibu wa kifungu cha 11C(3) cha Sheria ya Vyama vya Siasa, Sura ya 258 kinakataza vyama vya siasa kutumia au kuweka nembo, bendera, au alama yoyote ya chama kwenye majengo ya umma au ofisi za serikali.

Lengo ni kuhakikisha kuwa majengo ya umma yanabaki kuwa maeneo yasiyoegemea upande wowote wa kisiasa na yanayohudumia wananchi wote bila ubaguzi wa kisiasa.