JKCI kuanzia matawi nchini

Muktasari:

  • Mwenyekiti wa Bodi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Profesa William Mahalu amesema umefika wakati wa kuanzisha  matawi ya taasisi hiyo katika Kanda ili kusaidia utoaji wa huduma katika maeneo hayo.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Bodi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Profesa William Mahalu amesema umefika wakati wa kuanzisha  matawi ya taasisi hiyo katika Kanda ili kusaidia utoaji wa huduma katika maeneo hayo.

Amesema hiyo ni ndoto moja iliyobakia kati ya nne alizokuwa nazo tangu kuanzishwa kwa JKCI mwaka 2008.

Ameyasema hayo leo Jumamosi Juni 12, 2021 katika hafla ya uzinduzi wa mtambo wa Cathlab uliounganishwa na mtambo wa Carto 3 (3D & Mapping Electrophysiology System) uliogungwa JKCI.

Profesa Mahalu amesema Tanzania ni kubwa na wakati mwingine ni ngumu kwa mgonjwa wa tatizo la moyo kutoka Mbinga, Muleba, Mbambabay  hadi JKCI mkoani Dar es Salaam.

“Mimi ndoto yangu ni kwamba tuanzishe matawi ya  JKCI katika hospitali zetu za kanda, hii naamini itatusaidia kutupunguzia matatizo mengi, kama mgonjwa wetu mmoja alivyosema, kwa njia hii basi, India itakuwa Imerudi hapa (Tanzania),” amesema Profesa Mahalu.

Akielezea ilivyokuwa kabla ya kuanzishwa JKCI, amesema mwaka 1978 alipokuwa hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) aliona watu wengi wakifariki kutokana na matatizo ya moyo na walioweza walipelekwa nje jambo ambalo lilimfanya kuweka ndoto ya kwanza kuwa operesheni hizo lazima zifanyike Tanzania

“Ikapigwa vita na wengi sana lakini mwisho nilirudi nyumbani na mwaka 2008 tukaanza kufanya operesheni za moyo nchini na tulianza polepole na tunawashukuru  wenzetu wa MOI (Taasisi ya Mifupa) walitupa nafasi tukapanga pale,” amesema Profesa Mahalu

Anasema ndoto ya pili ilikuwa kuifanya JKCI kuwa taasisi kwani waliamini wakijitenga na wengine itakuwa vizuri zaidi huku akimshukuru Rais wa Awamu ya nne, Jakaya Kikwete kuwa alilisikia hilo.

“Baada ya kuanza taasisi sasa  tulianza kazi ya kuhakikisha watu hawaendi nje ya nchi kutibiwa na kuanza kuomba watu kutoka nje waje kushiriki katika upasuaji uliokuwa ukifanyika nchini.”

“Lakini sasa umeonyeshwa ushahidi kuwa operesheni nyingi zinafanywa na wenyeji, ushahidi mkubwa ulikuwa wakati wa Covid-19, operesheni nyingi zilifanyika wakati mipaka imefungwa hata wale waliokuwa wanatusaidia hawakuweza kuja na watanzania wengi wamefaidika nayo,” amesema Profesa Mahalu

Amesema kutokana na kukosekana kwa wataalamu waliamua kuanzisha mafunzo kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Sayansi ya Tiba Muhimbili (Muhas) ili waweze kufundisha madaktari bingwa wa ndani na mara chache inapolazimika wanapelekwa nje ya nchi kwenda kuona wengine wanafanyaje na kupata ujuzi mpya.