JKT wawaita vijana wengine

Muktasari:

  • Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) limeongeza majina ya vijana wengine waliomaliza kidato cha sita wanaotakiwa kujiunga na mafunzo kwa mujibu wa sheria  mwaka 2022.

Dodoma. Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) limeongeza majina ya vijana wengine waliomaliza kidato cha sita wanaotakiwa kujiunga na mafunzo kwa mujibu wa sheria  mwaka 2022.

Wito huo umetolewa na mkuu wa JKT, Meja Jenerali Rajabu Mabele Jumatano Juni 22, 2022 na kutakiwa kuripoti katika kambi mbalimbali zilizopo karibu na wanapoishi kuanzia jana hadi Juni 25,2022.

Akizungumzia kuhusu wito huo mkuu wa tawi la Utawala wa JKT, Brigedia Jenerali Hassan Mabena amesema vijana hao wanatakiwa kuripoti katika makambi yaliyo jirani isipokuwa kambi ya Makutopora JKT iliyopo mkoani Dodoma, CUJKT iliyopo Kimbiji mkoani Dar es Salaam na Ruvu JKT iliyopo Mlandizi mkoani Pwani.

Brigedia Jenerali Mabena amesema kambi ya Ruvu JKT inapokea wahitimu wenye ulemavu wa kuonekana wa macho kwa kuwa ina miundombinu ya kuwahudumia watu wa jamii hiyo.

“Tunatangaza awamu mbili mpaka tatu ili kuweza kutoa fursa kwasababu hayo mafunzo yanawahusu vijana wote ambao wamemaliza kidato cha sita,” amesema.

Aidha, mkuu wa Jeshi hilo, Meja Jenerali Rajabu Mabele amewataka vijana walioitwa kwa mujibu wa sheria kwa mwaka 2022 ambao hawajaripoti katika makambi waliyopangiwa hadi sasa kuripoti mara moja.

“Anawakaribisha vijana wote walioitwa ili waweze kujiunga na vijana wenzao katika kujifunza uzalendo, umoja wa kitaifa, stadi za kazi, stadi za maisha na utayari wa kulitumikia Taifa,”amesema.