Joe Biden azifuta sera kadhaa za Trump

Thursday January 21 2021
joebiudenpic
By Mwandishi Wetu

Marekani. Rais wa Marekani, Joe Biden ameingia ofisini kwa kasi baada ya kuanza kazi kwa kutengua sera kadhaa muhimu za Rais aliyemaliza muda wake, Donald Trump, saa chache baada ya kuapishwa.

Biden alipishwa jana Jumatano Januari 20, 2021, kuwa Rais wa 46 wa Marekani na tayari ameshasaini maagizo ya watendaji 15 yanayolenga kukabiliana na kusambaa kwa virusi vya corona.

Shughuli ya uapisho wa kiongozi huyo na Makamu wake wa Rais, Kamala Harris, ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwamo Barack Obama, Bill Clinton, George W Bush na aliyekuwa makamu wa Rais wa Trump, Mike Pence.

Trump ambaye bado anaonekana hajakubaliana na ushindi wa Biden, alishangaza wengi baada ya kukataa kuhudhuria hafla hiyo ya mrithi wake na badala yake, aliamua kufanya sherehe zake binafsi katika makazi yake.

Katika hotuba aliyoitoa Biden baada ya kuapishwa, aliahidi kuwa atakuwa Rais wa wote waliompigia kura na ambao hawakumpigia kura.

Alisema ushindi alioupata ni wa kidemokrasia huku akizitaka jamii za kimataifa kuitegemea Marekani mpya.

Advertisement

“Nitailinda Katiba, nitailinda Marekani, nitailinda demokrasia na kwa pamoja, tutaandika historia ya Marekani yenye matumaini na sio uwoga. Marekani yenye umoja na sio utengano, Marekani yenye mwanga na sio giza, tutaandika historia yenye utu, upendo na yenye kuponya maumivu,” amesema Biden.Advertisement