Jumuiya za kusaidiana zaanza kusajiliwa

Muktasari:
- Umuhimu wa kusajili vikundi hivi ni kwa wanachama wenyewe kupata uhalali wa kikundi chao kisheria.
Dar es Salaam. Ofisi ya Msajili wa Jumuiya, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, imetangaza kuanza usajili wa jumuiya zote zisizo za kidini nchini, huku ikiwaonya wanaoendesha shughuli zao ndani ya jumuiya hizo bila kujisajili.
Usajili tayari umeanza kwa Mkoa wa Dar es Salaam leo Aprili 2, 2024 hadi Aprili 10 na utafanyika kwenye ofisi za wakuu wa wilaya kwa mikoa yote nchini.
Ratiba ya usajili kwa mkoa wa Dar es Salaam, itaanzia Wilaya ya Kigamboni Aprili 2- 3, Temeke Aprili 4-5, Ubungo Aprili 6-7 Kinondoni Aprili 8-9 na Ilala Aprili 9-10 na baadaye utaratibu huo kuendelea kwa mikoa mingine.
Jumuiya zinazotajwa ni zinazohusisha umoja wa watu kuzikana, kusaidiana kwenye shida na raha, jumiya ya wamiliki wa nyumba, umoja wa watu wanaoishi kwenye makazi.
Wengine ni jumuiya za kitamaduni, kikabila, kanda, jumuiya za kitaaluma, umoja wa waandishi wa habari, madaktari wahandisi, wahitimu wa shule na vyuo na mafundi na walioanzisha umoja wao wa kusaidiana kupitia kundi la WhatsApp.
Hayo yalielezwa leo Aprili 2, 2024 na Msajili wa Jumuiya Emmenuel Kihampa wakati akizungumza na waandishi wa habari akisisitiza sifa moja wapo ya jumuiya ni kuwa na idadi ya watu 10 na kuendelea.
“Umuhimu wa kusajili vikundi hivi ni kwa wanachama wenyewe kupata uhalali wa kikundi chao kisheria, kwa mujibu wa kifungu cha 40 ya sheria namba 3 ya mwaka 2019 ni sharti la lazima kusajili kusanyiko au vyama vyote vinavyopaswa kusajiliwa kisheria,”amesema Kihampa.
Kihampa ametaja sababu nyingine ya usajili wa jumuiya hizo ni kulinda mali na fedha za wanachama zinazotolewa kwenye vikundi husika.
Hii ni kutokana baadhi ya watu kuwa na tabia ya kutokomea na mali au fedha za vyama hivyo kwenye jamii.
“Pia, kuhakikisha chama kinalindwa kwa misingi ya utawala bora na kulinda haki ya wanachama wake, lengo lingine tupate takwimu sahihi za vyama vilivyopo hapa nchini,”amesema.
Jambo lingine alilotaja ni kuwezesha Serikali kuweka mikakati ya kuvifikia vyama hivyo na kuwasaidia kuongeza tija na uzalishaji na kufikia maendeleo.
Amesema kupitia usajili wa vikundi hivyo, itachochea umoja na mshikamano kwenye jamii pamoja na kudumisha mila na desturi ya Watanzania hasa katika kipindi hiki ambacho kuna mmomonyoko wa maadili.
“Ili kikundi kisajiliwe, wahusika wanapaswa kuwa na barua ya mkuu wa wilaya ya eneo analotokea, orodha ya watu 10 waanzilishi wa vikundi hivyo na wasifu zao pamoja na picha na namba za simu za viongozi wa vikundi hivyo pamoja na katiba ya kikundi,”amesema.
Kihampa ametaja utaratibu mwingine ni kuwasilisha maombi ya usajili kwa ofisi ya mkuu wa wilaya kwa kulipa Sh50, 000 ada ya mwaka 50,000 na ada ya cheti ni Sh100, 000.
“Mpaka Machi mwaka huu, Kihampa alisema tayari wamesajili jumuiya 10,690 tangu mwaka 1995 huku wakifuta jumuiya zisizo hai 1200 na kutangaza zingine 1300 kupitia taarifa ya Serikali,”amesema.
Akizungumzia takwa hilo la kusajili jumuiya Jesca Mollel ambaye ni mwanachama wa jumuiya ya kusaidiana ya Kabila la Kimasai, amesema utaratibu huo ni mzuri kwani utawaongezea imani ya viongozi wao.
“Tuna kundi letu la Enaboishu ambalo linatujumuisha wamasai lengo ni kusaidiana kwenye misiba sherehe na mambo mengine ya kijamii hivyo kwa utaratibu huu wa Serikali ni mzuri kundi letu sasa litadumu,”amesema Jesca.
Kwa upande wake, Edgar Hussein mhitimu wa chuo cha uandishi wa habari Arusha ambaye alianzisha jumuiya kwa njia ya mtandao amesema kujisajili ni njia salama zaidi.
“Tulimaliza chuo mwaka 2019, tukaanzisha kundi kwa njia ya mtandao WhatsApp, tukatengeneza katiba yetu na taratibu zingine zinazopaswa kufuatwa na mwanachama lakini hatukujua utaratibu huu wa kisheria, kama kujisajili ni jambo zuri ila malipo kukamilisha usajili Sh200,000 ni nyingi kwetu,”amesema Hussein.
Machi 26, 2024 Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni akizindua kampeni ya usajili wa jumuiya amesema Serikali inatambua jitihada za jumuiya hizo katika kuleta matokeo chanya ya maendeleo nchini.
“Usajili wa jumuiya hizo utarahisisha utekelezaji wa majukumu, ushirikiano pamoja na uwazi kwa Serikali kuhakiki mapato na matumizi ya jumuiya hizo.... Serikali kupitia wizara tupo tayari katika kushirikiana na kutatua changamoto ili kurahisisha utekelezaji wa majukumu yao,”amesema.
Masauni alizitaka jumuiya hizo kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia kanuni, uwazi na uwajibikaji bila kumomonyoa maadili ya Kitanzania na hiyo ni pamoja na kujisajili zitambulike.