Kadco kukusanya Sh17 bilioni
Muktasari:
Kampuni ya uendeshaji na uendelezaji wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Kilimanjaro (Kadco) imekusudia kukusanya zaidi ya Sh17.5 bilioni mwaka 2021/22 na kutumia Sh15.5 bilioni kwa ajili ya matumizi ya kawaida pamoja na mishahara ya watumishi.
Hai. Kampuni ya uendeshaji na uendelezaji wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Kilimanjaro (Kadco) imekusudia kukusanya zaidi ya Sh17.5 bilioni mwaka 2021/22 na kutumia Sh15.5 bilioni kwa ajili ya matumizi ya kawaida pamoja na mishahara ya watumishi.
Akizungumza leo Alhamisi Machi 4, 2021 katika ufunguzi wa baraza la wafanyakazi kaimu mkurugenzi wa kampuni hiyo, Christine Mwakatobe amesema kuanzia Julai 2020 hadi Januari 2021, Kadco imekusanya zaidi ya Sh5 bilioni zilizotokana na tozo za maegesho ya ndege na kodi mbalimbali.
Amesema katika kipindi hicho hawakutegemea mfuko wa Serikali kujiendesha.
Amebainisha kuwa mwaka wa fedha 2021/22 wamekadiria kukusanya zaidi ya Sh17.5 bilioni na matumizi na mishahara ya watumishi, watatumia zaidi ya Sh15.5 bilioni.
Amesema katika fedha hizo Kadco imekusudia kuboresha baadhi ya miradi ya maendeleo itakayogharimu Sh1.95 bilioni.
"Ipo miradi ambayo tumenuia kuikamilisha ndani ya miaka mitano ikiwamo kujenga hoteli ya nyota tano pamoja na business complex na kuanzisha mradi wa ufugaji wa nyuki,” amesema.
Akifungua baraza la wafanyakazi wa Kadco mkurugenzi wa utawala na rasilimali watu wizara ya ujenzi na uchukuzi, Lucas kambelenje amesema aliwataka watumishi wasimamia vizuri mapato na matumizi waweze kutoka kwenye kampuni na kuwa taasisi ya umma.