Kagaigai ‘awaka’ Sh3.2 milioni kununua bastola

Muktasari:

  • Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Stephen Kagaigai ameagiza wahusika walioidhinisha malipo ya Sh3.2 milioni kwa ajili ya ununuzi wa bastola ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi kuzirejesha.


Moshi. Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Stephen Kagaigai ameagiza wahusika walioidhinisha malipo ya Sh3.2 milioni kwa ajili ya ununuzi wa bastola ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi kuzirejesha.

Alisema taratibu za ununuzi wa silaha hiyo zilikiukwa.

Kagaigai alisema hayo jana, alipozungumza katika kikao cha baraza la madiwani wilayani hapa.

“Tangu mwaka jana sioni jitihada ambazo zimefanyika, menejimenti ifuatilie hizi fedha zirudi, vinginevyo mimi nimeandika ni ubadhirifu kwa kuidhinisha matumizi ambayo sio sahihi,” alisema Kagaigai.

“Haiwezekani mwaka mzima hamjafuatilia fedha na bastola ziko huko, hamtendei haki fedha za wananchi.”

Akizungumzia suala hilo, aliyekuwa meya wa manispaa hiyo ambaye ni Diwani wa Bomambuzi, Juma Raibu alisema suala la ununuzi wa bastola lilikiukwa na haiwezekani inunuliwe kwa matumizi ya mtu binafsi.

“Tuliliagiza baraza la madiwani lililopita kwamba ununuzi wa bastola ya Sh3.20 milioni iliyokuwa inunuliwe kwa sababu ya mkurugenzi, fedha hizo zirudishwe halmashauri, haiwezekani mkurugenzi wa manispaa kununua bastola kwa fedha za halmashauri,” alisema Raibu.

Akitolea ufafanuzi wa sakata hilo, Naibu Meya wa Manispaa hiyo, Stewart Nkinda alisema fedha za ununuzi wa bastola ya mkurugenzi zilipewa baraka zote na baraza la madiwani.

“Baraza la madiwani lilitoa baraka na pistol (bastola) ya mkurugenzi ikalipiwa fedha, hapa ninachokiona kwenye hoja ya mkaguzi ni namna hizi fedha zilipaswa kurudishwa halmashauri kutoka kwa supplier wa hizo bastola.”