Kagame aweka rekodi ya ushindi

Muktasari:

  • Katika uchaguzi wa mwaka 2003 uliofanyika baada ya kutengeneza Katiba iliyoweka ukomo wa mihula miwili ya urais ya miaka saba kila kimoja, Kagame alishinda kwa asilimia 95.1 akiwaangusha wapinzani wake Faustine Twagiramungu aliyepata asilimia 3.6 na Jean Nayinzira aliyeambulia asilimia 1.3.

Rais Paul Kagame wa Rwanda amefanikiwa kutetea kiti chake cha urais baada ya kushinda kwa asilimia 98.6 ya kura zilizopigwa na hivyo kuvunja rekodi ya ushindi aliyoiweka katika chaguzi mbili zilizopita.

Katika uchaguzi wa mwaka 2003 uliofanyika baada ya kutengeneza Katiba iliyoweka ukomo wa mihula miwili ya urais ya miaka saba kila kimoja, Kagame alishinda kwa asilimia 95.1 akiwaangusha wapinzani wake Faustine Twagiramungu aliyepata asilimia 3.6 na Jean Nayinzira aliyeambulia asilimia 1.3.

Aidha, katika uchaguzi wa mwaka 2010 Kagame alitangazwa mshindi baada ya kujizolea asilimia 93.08 akifuatiwa na Jean Damascene Ntawukuriryayo aliyeambulia asilimia 5.15.

Uchaguzi wa mwaka huu umeonyesha kwamba umaarufu wa Kagame ambaye alikuwa makamu wa rais kuanzia 1994 hadi 2000 alipoteuliwa kuwa kaimu rais baada ya Pasteur Bizimungu kujiuzulu kisha kusimamia mabadiliko ya Katiba, unazidi kuongezeka.

Matokeo yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi ya Rwanda jana siku moja baada ya uchaguzi huo, Kagame alishinda kwa asilimia 98.66 na kuwaangusha vibaya washindani wake Phillipe Mpayimana aliyepata asilimia 0.72 na Frank Habineza aliyeambulia asilimia 0.45. Asilimia 80 ya waliojiandikisha walipiga kura.

Taarifa zinasema kwamba raia wa Rwanda waishio nchi za nje pia walipiga kura katika vituo 98 isipokuwa katika nchi mbili jirani za Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo ambako imeelezwa hakukuwa na usalama wa kutosha.

Mabadiliko ya Katiba yaliyopitishwa kwa asilimia 98 mwaka 2015 kuondoa ukomo wa mihula kumwezesha Kagame kuongoza hadi mwaka 2034, kilikuwa kielelezo kwamba Wanyarwanda walikuwa wakimhitaji yeye na siyo Frank Habineza kutoka chama kidogo cha DGP wala mgombea binafsi ambaye hajulikani sana Philippe Mpayimana.