Kajisajili Basata kwa Sh45,000 ushiriki tamasha Wasafi

Kajisajili Basata kwa Sh45,000 ushiriki tamasha Wasafi

Muktasari:

  • Msanii wa muziki Tanzania, Naseeb Abdul maarufu Diamond Platnumz amesema wasanii watakaoshiriki tamasha la Tumekiwasha linaloandaliwa na Wasafi Media lazima wawe wamesajiliwa na Baraza la Sanaa la Taifa (Basata).

Dar es Salaam. Msanii wa muziki Tanzania, Naseeb Abdul maarufu Diamond Platnumz amesema wasanii watakaoshiriki tamasha la Tumekiwasha linaloandaliwa na Wasafi Media lazima wawe wamesajiliwa na Baraza la Sanaa la Taifa (Basata).

Ili msanii aweze kujisajili Basata anatakiwa kulipia Sh45,000 fedha ambayo baraza hilo limesema kila msanii anaweza kuimudu.

Mkali huyo wa wimbo wa Waah aliomshirikisha msanii wa DRC Congo, Koffi Olomide ameeleza hayo leo Jumanne Januari 19, 2021 katika mkutano wake na waandishi wa habari.

Tamasha hilo litafanyika Januari 30, 2021 jijini Dar es Salaam katika uwanja wa Uhuru kuanzia saa sita mchana.

"Agizo hili tumepewa na Basata wenyewe. Wamesema msanii yoyote ambaye hajasajiliwa asipande jukwaani. Sisi hatupo tayari kuona tunafungiwa tamasha kwa sababu ya mtu mmoja,” amesema Diamond.

Amebainisha kuwa msanii ambaye hajasajiliwa kwa sababu ya kushindwa kumudu gharama za usajili, anaruhusiwa kufanya mazungumzo na Wasafi na watamlipia gharama hizo na kumkata kwenye malipo ya kutumbuiza katika tamasha hilo.

Akizungumza na Mwananchi Digital, ofisa sanaa mwandamizi wa baraza hilo, Abel Ndaga amesema gharama za msanii kujisajili ni Sh45,000 na kwamba haiwezi kuwa sababu  ya kushindwa kujisajili.

"Sh5,000 unalipia fomu, Sh20,000 unalipia gharama za usajili na Sh20,000 inayobaki ni malipo ya kibali cha kufanya sanaa ambacho utakuwa unalipia kila mwaka. Kwa hiyo mtu akijisajili leo Januari 19 atalipia tena mwakani siku kama ya leo,” amesema.

Diamond amesema kabla ya tamasha hilo kufanyika, Wasafi watafanya kongamano na wasanii kwa ajili ya kuwakutanisha na wataalamu wa sekta ya burudani na sanaa nchini kwa lengo la kupewa elimu namna ya kuwa msanii bora na mwenye ushawishi sokoni.