Kalaghe mwenyekiti mpya Alat Tanga

Muktasari:

Mwenyekiti wa halmashauri ya Wilaya ya Korogwe mkoani  Tanga,   Sadiki Kalaghe amechaguliwa  kuwa mwenyekiti wa Jumuiya ya Serikali za Mitaa (Alat) Mkoa wa Tanga.

Lushoto. Mwenyekiti wa halmashauri ya Wilaya ya Korogwe mkoani  Tanga,   Sadiki Kalaghe amechaguliwa  kuwa mwenyekiti wa Jumuiya ya Serikali za Mitaa (Alat) Mkoa wa Tanga.

Akitangaza matokeo hayo katibu tawala Mkoa wa Tanga, Judica Omari amesema waliowania uenyekiti walikuwa watatu lakini Kalaghe  aliongoza kwa kupata  kura 17, Idrisa Mgaza ambaye ni mwenyekiti ya halmashauri ya Kilindi  kura 13 huku mwenyekiti wa halmashauri ya Wilaya ya Muheza,  Erasto Muhina akipata kura 10.

Nafasi ya makamu mwenyekiti  meya wa Jiji la Tanga, Abdurahman Shiloo aliibuka mshindi kwa kupata kura 32 na kumwangusha mwenyekiti wa Handeni Mji,   Mussa Mkumbati aliyepata kura nne.

Baada ya kutangazwa mshindi Kalaghe amesema moja ya changamoto kubwa kwenye jumuiya hiyo ni uboreshaji wa Serikali za mitaa ikiwemo maslahi ya madiwani.

Amewataka wenyeviti  wa halmashauri  na wakurugenzi  katika  halmashauri  zao  kuhakikisha  wanaongeza kasi ya ukusanyaji mapato pamoja na kulipa  michango  yao  kwa wakati ili  kuipa  uhai jumuiya hiyo .

Makamu mwenyekiti wa halmashauri ya Bumbuli, Hozza Mandia amesema, “tuna imani na mwenyekiti mpya ndio maana tumemchagua  ni mchapa kazi pia ana uzoefu wa kutosha na ni kiongozi mwenye uwezo wa kushirikisha wenzake katika majukumu ya maendeleo.”

Imeandikwa na Raisa Said