Kalonzo awekwa njiapanda

Muktasari:

  • Kiongozi wa chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka yupo njiapanda ndani ya muungano wa vyama vya Azimio la Umoja One Kenya.

Kiongozi wa chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka yupo njiapanda ndani ya muungano wa vyama vya Azimio la Umoja One Kenya.

Kinachomweka njiapanda Kalonzo ni fursa finyu ya yeye kuteuliwa kuwa mgombea mwenza wa urais. Na sasa anatakiwa kuchagua jambo moja kati ya mawili.

Jambo la kwanza lipo ndani ya uwezo wake. Kujitoa Azimio la Umoja One Kenya kama mtu binafsi na kuamua njia yoyote ya kisiasa atakayoona inamfaa, ikiwemo hata kumuunga mkono Naibu Rais, William Ruto, ambaye anawania kuingia Ikulu kwenye Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Agosti 9, mwaka huu.

Uamuzi huo utakuwa kwenda kinyume na msimamo wa chama chake, Wiper, ambacho kimesaini na vyama vingine kuunda Azimio la Umoja One Kenya na kukubaliana kumuunga mkono Raila Odinga kama mgombea urais. Hata hivyo, hakuna sheria yoyote atakayokuwa amevunja.

“Kama mtu binafsi, Kalonzo ana haki zote kumuunga mkono mgonbea yeyote anayemtaka, hata kama atakuwa amekwenda kinyume na msimamo wa chama chake. Itakuwa ni jukumu la chama kumchukulia hatua kama kitaona inafaa,” alisema mwanasheria mbobezi wa Katiba Kenya, Bob Mkangi.

Njia ya pili kwa Kalonzo ni kukishawishi chama chake, Wiper, kiamue kutotambua makubaliano yaliyojenga Azimio la Umoja, kisha chama hicho kiwasilishe jina la Kalonzo kama mgombea urais wao kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Mei 16, mwaka huu.

Hata hivyo, uamuzi huo wa Wiper kumsimamisha Kalonzo kama mgombea urais, utakutana na changamoto za kisheria kwa sababu upo mwongozo kuwa chama chenye mpango wa kujitoa Azimio la Umoja One Kenya kwa ajili ya uchaguzi wa mwaka huu, lazima kiandike notisi ya miezi mitatu.

Hata baada ya kuandika notisi, chombo cha juu cha Azimio la Umoja, ambacho ni Baraza la Vyama vilivyoungana, kitapaswa kufanya mapitio ya sababu za Wiper kujitoa. Baraza hilo linaongozwa na Rais Uhuru Kenyatta akiwa mwenyekiti.

Baada ya Baraza za Azimio chini ya Uhuru kupitia, vilevile sababu za Wiper kujiondoa kwenye muungano huo, zitapitiwa na Msajili wa Vyama vya Siasa Kenya, kabla ya kutoa uamuzi wa mwisho.

Juzi (Jumatano), Msajili wa Vyama vya Siasa Kenya, Ann Nderitu alisema kila chama kinao uhuru wa kujitoa kwenye muungano wa vyama, lakini lazima kiwe na tahadhari ya makubaliano ambayo walisaini.

“Kujitoa na kujiunga, inategemea na masharti ambayo chama kinakuwa kimesaini kwenye muungano wa vyama,” alisema Nderitu.

Hata hivyo, hapo kabla, Msajili huyo wa vyama alivizuia Maendeleo Chap Chap (MCC) cha Gavana wa Machakos, Alfred Mutua na Pamoja African Alliance (PAA) cha Gavana wa Kilifi, kujiondoa Azimio la Umoja One Kenya, na kuvishauri viheshimu makubaliano viliyosaini.

“Sina uhakika na ujazo wa orodha ya wagombea ambao Wiper imewasilisha IEBC,” Mkangi alisema, na kufafanua kuwa majina ambayo Wiper iliyawasilisha IEBC Aprili 9, mwaka huu, kuomba wateuliwa kuwa wagombea wa nafasi mbalimbali kwenye uchaguzi mwaka huu ndiyo itaamua.

Mkangi ambaye alikuwa mmoja wa wajumbe wa kamati maalumu ya wataalamu, iliyoandika Katiba ya Kenya mwaka 2010, alisema kama Aprili 9, mwaka huu Wiper haikuwasilisha jina la Kalonzo kuwa mgombea urais wake, itakuwa vigumu kumsimamisha kwenye Uchaguzi Mkuu Agosti 9.

Aprili 9, mwaka huu ulikuwa ndio ukomo wa vyama vya siasa kukamilisha usajili wa kuungana kuelekea Uchaguzi Mkuu Agosti 9, 2022. Azimio la Umoja One Kenya walikamilisha usajili, Wiper wakiwa ni sehemu ya muungano.

Kumekuwa na maneno kuwa Kalonzo amekuwa akitishia kujitoa na kumuunga mkono Ruto ili kumshinikiza Raila amteue kuwa mgombea mwenza.

Seneta wa Makueni, Mutula Kilonzo Jnr amekanusha taarifa hiyo kuwa Kalonzo amekuwa akitengeneza uvumi wa kujitoa na kumuunga mkono Ruto ili Raila aogope na kumteua kuwa mgombea mwenza. Kilonzo Jnr ni makamu mwenyekiti wa Wiper.

Uvumi huo umekuwa na hoja kwamba kama Raila atamtangaza Kalonzo kuwa mgombea mwenza wake itamsafishia njia Ruto kumweka wazi Musalia Mudavadi kama mshirika wake kwenye uchaguzi mwaka huu.

“Tuhuma zinajenga picha kuwa watu wote wanaotengeneza uvumi huu wanalipwa na Naibu Rais. Kabla ya kujiunga na Azimio la Umoja One Kenya, Kalonzo alikuwa wazi kwa uongozi wa Wiper kuwa hakuwa na mpango wa kushirikiana na Ruto. Kama tutakosana na Azimio, mpango wetu wa pili siku zote umekuwa kumsimamisha Kalonzo kama mgombea urais wetu,” alisema Kilonzo.

Dili la ushirikiano kwa ajili ya uchaguzi mwaka huu, baina ya Wiper na Kenya Kwanza ya Ruto, licha ya kukabiliwa na changamoto za kisheria pale Wiper watakapojitoa Azimio, vilevile ni vita dhidi ya muda, kwani tarehe ya mwisho ya kuwasilisha makubaliano ya ushirika wa uchaguzi ni Mei 8, 2022.

Aprili 9, mwaka huu ilikuwa mwisho wa vyama kupata usajili ili kusimama katika uchaguzi na Mei 8, mwaka huu, ni ukomo wa vyama ambavyo umoja wao haukusajiliwa, kuwasilisha hati ya makubaliano ya ushirikiano, huku kila chama kikisimama kivyake.