Kama bado unatumia mifuko ya plastiki hii inakuhusu

Muktasari:

Naibu Waziri  Ofisi ya Makamu wa Rais (muungano na mazingira), Mwita Waitara ameagiza ufanyike msako kuwabaini wanaoendelea kutumia mifuko ya plastiki.

Dar es Salaam. Naibu Waziri  Ofisi ya Makamu wa Rais (muungano na mazingira), Mwita Waitara ameagiza ufanyike msako kuwabaini wanaoendelea kutumia mifuko ya plastiki.

Waitara ametoa agizo hilo leo Alhamisi Machi 4, 2021 alipotembelea  ofisi za Jiji la Dar es Salaam  ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya kukagua mazingira nchini.

Amesema pamoja na Serikali kukataza mifuko hiyo, kuna watu wanaendelea kuitumia.

"Operesheni kubwa ifanyike, hususani Kariakoo ili kuondoa mifuko ya plastiki ambapo wengi wanaitumia kufungashia maji ya kandoro na bidhaa mbalimbali. Mifuko hii inatoka mipakani mwa nchi tena inaingia kiholela na watu hawalipi kodi.”


"Watu hawa wanavunja sheria hivyo wakipatikana washughulikiwe. Serikali ilitoa mwisho wa kutumia lakini bado watu wanaendelea kuitumia. N aagiza Jiji mshughulikie hili, mshirikiane na watu wa NEMC mfanye operesheni kubwa kuondoa mifuko hii," amesema.

Aidha ameagiza kila Kata kuwe na kamati za mazingira ili kuhakikisha suala la uchafuzi wa mazingira linakuwa historia.


Imeandikwa na Tatu Mohamed