Kamati ya Bunge yaibana halmashauri ya Momba

Muktasari:

Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) imeagiza watumishi wa Wilaya ya Momba mkoani Songwe waliojaza vibaya fomu za madai ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kulipa fedha zilizokataliwa kulipwa na mfuko huo.

Dodoma. Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) imeagiza watumishi wa Wilaya ya Momba mkoani Songwe waliojaza vibaya fomu za madai ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kulipa fedha zilizokataliwa kulipwa na mfuko huo.

Hayo yamesemwa leo Jumatano Oktoba 20 2021 na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Selemani Zedi mara baada ya kupitia hesabu za halmashauri hiyo za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) kwa mwaka unaoishia Juni 30, 2020.

“Kamati imebaini kuna vitendo vya makusudi vya kukosea kujaza karatasi za madai na hivyo kuikosesha halmashauri fedha kwasababu zikiendaa wanakataa kuwalipa fedha,” amesema.

Amesema hata hivyo wamebaini kuwa halmashauri hiyo haijachukua hatua yoyote baada ya kubaini hilo.

Amesema hivyo, kamati hiyo inataka hatua za makusudi za kuwajua na kuwabaini waliokosea makusudi zichukuliwe na kuwalazimisha walipe.

Aidha, amesema taarifa ya CAG imebaini kuwa haikupeleka ipasavyo na kwamba badala ya kupeleka asilimia 40 ya mapato yao ya ndani walipeleka asilimia tano tu.

Naye mjumbe wa kamati hiyo ambaye pia ni Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye amesema Serikali imetekeleza utaratibu wa kutumia force account katika miradi lakini uzoefu unaonyesha kuwa kuna mianya mingi sana ya pesa inapotea.

“Kuna umuhimu kuangalia upya kuweka ukomo ukubwa wa mradi. Kama mradi mkubwa sana tusiruhusu force account,” amesema.

Aidha, amesema hali ni mbaya katika eneo la usimamizi kwenye halmashauri ya Wilaya ya Momba na kushauri kuchukua hatua kuimarisha usimamizi na kuboresha baadhi ya maeneo ya kisheria ili kupata matokeo mazuri.

Kwa upande wake Ofisa Masuhuli ambaye pia ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Songwe Misaile Musa amekiri halmashauri hiyo ina mazingira sio mazuri na inahitaji kusimamiwa kwa karibu.

 “Sisi tumejipanga, tutasimamia na kuleta mabadiliko katika halmashauri zetu zote tano. Maeneo ambayo yanatakiwa kuchukuliwa tutasimamiana kuhakikisha kuwa hatua zinachukuliwa,” amesema.