Kanda ya Ziwa kupata intaneti ya satelaiti
Muktasari:
Wakazi wa mikoa ya Kanda ya Ziwa wataanza kupata huduma ya kimtandao kwa njia ya setelaiti baada ya Kampuni ya Konnect kuzindua huduma zake jijini Mwanza.
Mwanza. Wakazi wa mikoa ya Kanda ya Ziwa wataanza kupata huduma ya kimtandao kwa njia ya satelaiti baada ya Kampuni ya Konnect kuzindua huduma zake jijini Mwanza.
Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa huduma hiyo Mei 26, 2023, Mkurugenzi wa Masoko mtandao wa Konnect, Obafemi Agbanrin amewataka wakazi wa Kanda ya Ziwa kutumia mtandao huo kufanya biashara na ujasiriamali kidijitali ili kukuza masoko ndani na nje ya nchi.
Amesema hata wakulima na wavuvi wanaweza kuutumia kupata taarifa mbalimbali kuhusu kilimo cha kisasa, hali ya hewa na uvuvi husiohatarisha mazingira sehemu yoyote walipo.
“Tunaamini kwa dunia ya sasa kila mmoja anahitaji interneti yenye kasi na inayopatikana wakati wote kwa ajili ya shuguli za kiuchumi na hata kwa familia,”amesema
Amesema huduma hiyo inapatikana kwa gharama kuanzia Sh300 hadi Sh18, 000 kwa watakaotumia wifi kulingana na aina ya data huku gharama ya kuunganisha dishi inaanzia Sh60, 000 kwa mwezi.
“Mtandao huu unafika hata zile sehemu ambazo hazina mawasiliano ya kimtandao, ili mradi unatumia connect basi utaweza kufanya kazi zako mtandaoni kwa haraka,”amesema
Mkazi wa jijini Mwanza, Seleman Yahya amesema wajasiriamali wa mtandaoni wamepata mkombozi baada ya malalamiko mengi ya vifurushi vya data vya mitandao ya simu kupanda bei.
Naye Neema Emmanuel amesema mtandao wa data ni muhimu kwakuwa wafanyabiashara akiwemo yeye wanatumia kutangaza biashara zao huku akiwataka Konnect kufika hadi maeneo ya pembezoni.