Kanisa kuanzisha kituo cha kuwasaidia vijana

Muktasari:

  • Kanisa la Waadventista wa Sabato Mzizima limejipanga kuanzisha kituo katikati ya Mkoa wa Dar es Salaam ili kuwasaidia vijana kupambana na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa ajira, umaskini na utumiaji wa dawa za kulevya. 

Dar es Salaam. Kanisa la Waadventista wa Sabato Mzizima limejipanga kuanzisha kituo katikati ya Mkoa wa Dar es Salaam ili kuwasaidia vijana kupambana na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa ajira, umaskini na utumiaji wa dawa za kulevya.

Pia, kituo hicho kitashughulika masuala ya afya, kitakuwa na maktaba ya jamii pamoja na huduma mbalimbali za kuwafikia vijana katika jamii.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumanne Aprili 13, 2021 mkurugenzi wa maendeleo ya kanisa jimbo la mashariki kati mwa Tanzania, mchungaji Jonas Singo amesema kwa mujibu wa tafiti mbalimbali, ukosefu wa ajira umesababisha kuongezeka kwa matukio ya uhalifu, matumizi ya dawa za kulevya, mimba zisizotarajiwa pamoja na ongezeko la magonjwa yatokanayo na ngono isiyo salama kwa vijana nchini.

Amesema kwa kuzingatia hayo, kanisa la Waadventista wa Sabato Mzizima linaendesha harambee ili kupata Sh800 milioni zitakazolipia gharama za ununuzi wa eneo na ujenzi. 

"Inakadiriwa kuwa nusu ya wakazi wa Tanzania wana umri chini ya miaka 25, na mmoja kati ya watoto watatu wanaozaliwa huishi mjini na waathirika wakiwa ni vijana na kupelekea ukosefu wa ajira, kuongezeka kwa uhalifu, matumizi ya dawa za kulevya, mimba zisizotarajiwa na magonjwa ya kuambukiza.”

"Itambulike kuwa vigezo vitakavyotumika kwa vijana hawa ni Utanzania tu. Hatutajali dini wala nini, hiki ni kituo kwaajili ya watu wote," amesema.