Karani wa mahakama adakwa na Takukuru akidaiwa kuomba rushwa ya Sh30,000

Thursday April 08 2021
By Joseph Lyimo

Babati. Karani wa mahakama ya mwanzo Magugu wilayani Babati, Alfred Ntatirwa anashikiliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa madai ya kuomba na kupokea rushwa ya Sh30,000 ili ampatie mwananchi nakala ya hukumu.

Mkuu wa Takukuru mkoani Manyara, Holle Makungu ameyasema hayo leo Alhamisi Aprili 8, 2021  wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Babati.

Makungu amesema karani huyo anadaiwa kufanya makosa hayo Aprili 6, 2021 kinyume na kifungu cha 15 cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa namba 11/2007.

Amesema Ntatirwa anatuhumiwa kuomba rushwa ya Sh30,000 na kukamatwa na maofisa wa Takukuru akiwa amepokea kiasi hicho cha fedha ili atoe nakala ya hukumu ya kesi.

"Mtuhumiwa aliomba fedha hizo ili amsaidie mtu mmoja aliyeomba nakala ya hukumu ya kesi iliyokuwepo mahakama ya mwanzo Magugu ambaye hakuridhika na hukumu hiyo na alitaka kukata rufaa mahakama ya Wilaya," amesema Makungu.

Amesema mtuhumiwa huyo anatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote ili akajibu mashtaka hayo yanayomkabili.

Advertisement

Amewataka wananchi wote kufahamu kuwa hawalazimiki kulipia tozo yoyote inayohusiana na nakala za hukumu na maamuzi ya mahakama ya mwanzo, wilaya, hakimu mkazi au mahakama kuu.


Advertisement