Kasi watoto wanaozaliwa utumbo nje yawa tishio

Mfano wa mdoli mwenye utumbo nje. Picha na Mgongo Kaitira

Mwanza. Watoto 43 kati ya 290 waliozaliwa wakiwa na utumbo nje wamepona baada ya kupatiwa matibabu katika Kanda ya Ziwa ndani ya kipindi cha miaka miwili.

Hayo yalielezwa Agosti 3, 2023 na Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando, Fabian Massaga, wakati akitoa takwimu za tatizo hilo na kusema watoto waliofariki dunia ni 247 sawa na asilimia 85 ya watoto hao.

Alisema vifo hivyo vimetokea katika kipindi cha kuanzia mwaka 2021 hadi 2023.

Dk Massaga alisema takwimu za Kanda ya Ziwa zinaonyesha kuanzia mwaka 2020 kurudi nyuma, watoto waliozaliwa na tatizo hilo, kitaalumu Gastroschisis walikuwa wakifariki dunia, hivyo kusababisha uwepo wa idadi kubwa ya vifo vya watoto.

Akizungumza wakati wa maadhimisho ya siku ya watoto waliozaliwa utumbo ukiwa nje, alisema tatizo hilo ni changamoto ya kidunia, akitoa takwimu kuwa katika kila vizazi 4,000, mtoto mmoja huzaliwa akiwa na tatizo hilo.

"Napenda kutoa rai kwa wajawazito ambao wana umri chini ya miaka 21, kuhudhuria kliniki na kufanya kipimo cha ultrasound ili kubaini tatizo hili kwa mtoto na kuwa na mpango wa matibabu kabla mtoto hajazaliwa," alisema Dk Massaga na kuongeza;

“Wahudumu wa afya mnapokutana na mtoto mwenye changamoto hii wasiliana haraka na Hospitali ya Bugando ili kupata mwongozo sahihi wa jinsi ya kuwahudumia kabla ya kuwasafirisha kuwaleta hapa kwa ajili ya matibabu zaidi."

Mkuu wa Idara ya Watoto Bugando, Dk Neema Kayange alisema watoto hao hupatwa na changamoto hiyo baada ya kutokea hitilafu za kimaumbile wakati wa ukuaji wa mtoto tumboni.

Alisema hakuna utafiti rasmi uliofanyika uliotaja chanzo cha tatizo hilo, badala yake aliwataka wajawazito kufanya kipimo cha ultrasound mapema ili kubaini iwapo mtoto ana tatizo hilo ili ajifungulie katika hospitali inayotoa huduma kwa watoto hao, ikiwemo Bugando kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa. Pia, alisema Bugando inajipanga kufanya utafiti utakaosaidia kubaini chanzo cha tatizo hilo, huku akiwataka wataalamu kutoka idara hiyo kuendelea kufanya ukusanyaji wa taarifa za wazazi waliojifungua watoto wenye tatizo hilo.

"Ni kweli wanaweza kuishi endapo miongozo ya matibabu yao inafuatwa. Watoto walio hapa ni ushuhuda kuwa kweli hawa watoto wanaweza kuishi. Hawa ni baadhi ya watoto ambao tuliwatibu hapa BMC na Mungu amewaponya," alisema Dk Kayange.

Alitaja changamoto za kuwahudumia watoto hao kuwa ni ukosefu wa mifuko ya kufunika sehemu ya utumbo iliyotoka nje, jambo linalosababisha wengine kufariki dunia wakiwa chini ya uangalizi wa madaktari.

“Bado tuna changamoto ya mifuko maalumu ya kuwafunikia sehemu ya utumbo ambayo inakuwa nje. Mifuko hiyo inaagizwa kutoka nje ya nchi kwa sababu nchini hatuna wataalamu wa kuzalisha. Tunaamini tukipata mtu wa kutuletea atatusaidia kuokoa maisha ya watoto wengi zaidi," alisema. Mbali na hilo, Dk Kayange alisema japo haijabainika chanzo, lakini mikoa ya Kanda ya Ziwa inaonekana kuwa na idadi kubwa ya watoto wanaozaliwa utumbo ukiwa nje.

Mkazi wa Bukoba mkoani Kagera, Zainabu Ally alisema alipojifungua mtoto wake, Jumanne Denis na kubaini utumbo uko nje aliamini atakufa, lakini juhudi za madaktari wa Bugando zimesababisha apone tatizo hilo.

"Muda mfupi baada ya kujifungua madaktari walinishauri kumuwahisha Bugando, lakini sikuamini kama ataishi. Namshukuru Mungu na Hospitali ya Bugando leo namuona mtoto wangu akiwa hai anacheza vizuri bila shida," alisema Zainabu.

Naye Mkazi wa Shinyanga, John Jibalo alisema baada ya mkewe kujifungua mtoto mwenye tatizo hilo alishtuka hadi alipofikishwa Bugando na kutibiwa tatizo hilo, ndipo matumaini ya kumuona akiishi yaliporejea.