KATIBA MPYA: Tujifunze kutokana na makosa yetu

Rais Jakaya Kikwete (kushoto) na Rais wa Zanzibar, Dk Al Mohamed Shein wakionyesha Katiba inayopendekezwa baada ya kukabidhiwa na Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba Samwel Sitta. Picha na maktaba

Muktasari:

Kuna mjadala mkubwa kuhusu Katiba Mpya. Wanaharakati na vyama vya siasa vya upinzani, lugha yao ya kutaka Taifa lipate Katiba Mpya, ilipazwa barabara. Sasa na CCM wamesema wanataka ingawa mwanzoni walisema kipaumbele chao na Serikali wanayoiongoza ni kuboresha uchumi


Kuna mjadala mkubwa kuhusu Katiba Mpya. Wanaharakati na vyama vya siasa vya upinzani, lugha yao ya kutaka Taifa lipate Katiba Mpya, ilipazwa barabara. Sasa na CCM wamesema wanataka ingawa mwanzoni walisema kipaumbele chao na Serikali wanayoiongoza ni kuboresha uchumi

Swali, lugha yao ni moja? Miaka nane iliyopita, vyama vyote vilikuwa vinataka Katiba Mpya. Wanaharakati hali ladhalika. Hata hivyo ilishindikana kwa sababu kila mmoja alikuwa na aina ya “upya” aliouhitaji ambao ulitofautiana na mwenzake.

Kumbukumbu ya nusu muongo uliopita ni kuharibiwa kwa mchakato wa Katiba Mpya katika hatua ya Bunge Maalumu la Katiba. Chama cha Mapinduzi (CCM) na vyama vya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kwa pamoja wanastahili lawama.

Bunge Maalumu la Katiba, lililoongozwa na aliyekuwa mwenyekiti wake, hayati Samuel Sitta, ndilo ambalo lilisababisha Rais wa Awamu ya Nne, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Jakaya Kikwete aondoke madarakani pasipo kupatikana kwa Katiba mpya.

Hali hiyo imekuwa kinyume na ahadi ya Rais Kikwete ambaye katika hotuba yake ya kuzindua Bunge la 10 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Novemba 2010, aliahidi kuwa muhula wake wa pili, 2010-2015 ungekuwa wa kupatikana kwa Katiba mpya ya Watanzania.

Sababu kuu ya kutopatikana kwa Katiba Mpya ni Ukawa kugoma na kususia vikao vya Bunge la Katiba, kisha waliosalia bungeni, wengi wao wakiwa CCM, walipuuza umuhimu wa maridhiano.

Bunge Maalumu la Katiba mwaka 2014, lilipitisha Katiba Inayopendekezwa. Hata hivyo, imekuwa vigumu kuruhusu mchakato wa kuipigia kura ya maoni, ama ipitishwe au ikataliwe, kutokana na kile kinachoonekana ni aibu kutokana na mazingira yaliyojitokeza bungeni.

Kimsingi, Katiba Inayopendekezwa ilipoteza uhalali mapema kabisa. Kitendo cha wajumbe zaidi ya theluthi moja kususia vikao vya Bunge la Katiba, kilijenga picha kuwa Katiba haiwezi kuwa ya wananchi.

Sababu nambari mbili ni kiburi cha wajumbe waliobakia bungeni. Kitendo cha wao kuamini kuwa wangeweza kuketi na kupitisha Katiba Inayopendekezwa pasipo maridhiano na waliosusa, kilikuwa hakijengi.

Katiba ya wananchi sharti iwe na maridhiano. Kwa maana kwamba Katiba ni vizuri iwe na sura yenye kukubalika na jamii kwa upana wake. Wengi wanaposusa, maana yake hiyo siyo Katiba ya wananchi bali ni Katiba ya kikundi fulani.


Makosa ya Ukawa kwenye Katiba

Bunge la Katiba mwaka 2014 lilithibitisha kuwa wapinzani Tanzania ni waoga, wanadeka na dhaifu ukilinganisha na wenzao wa Kenya. Wakati Ukawa wanasusa Bunge la Katiba, ilikuwa imepita miaka tisa tangu wapinzani Kenya walivyoikataa Katiba iliyokuwa chapuo la watawala.

Mwaka 2005 Kenya walipokuwa wanataka kufanya mabadiliko ya Katiba yao, mchakato uliendeshwa mpaka Bunge la Katiba liliketi. Ndani ya Bunge, sauti ya wajumbe wengi walikuwa upande wa maoni yenye kubeba fikra za aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, marehemu Mwai Kibaki na timu yake.

Kiongozi wa chama cha ODM, Raila Odinga, aliongoza timu ya watu ambao waliikataa katiba hiyo. Akina Raila pamoja na uchache wao hawakususa Bunge la Katiba, walibaki ndani yake, walipambana mpaka mwisho.

Kura za wajumbe wa Bunge la Katiba zilipopigwa, akina Raila walishindwa kutokana na uchache wao. Katiba inayopendekezwa kwa Wakenya ikawekwa hadharani, ikatangazwa tarehe ya kura ya maoni.

Raila na wenzake baada ya kushindwa bungeni, walijielekeza katika kuelimisha umma kuhusu ubaya wa Katiba iliyokuwa inapendekezwa. Matokeo ya kura ya maoni iliyofanyika Novemba 21, 2005, sauti za akina Raila zilisikika na wananchi wa Kenya kwa asilimia 58 waliikataa Katiba hiyo.

Wakati huo Kibaki, wabunge wengi na Serikali kwa upana wake walisimama imara kufanya kampeni wakiwataka wananchi kupiga kura ya “ndiyo”, lakini matokeo yakawa, waliochagua “hapana” walishinda.

Ukawa walipaswa kuonesha ukomavu wa aina hii, kushindana kwa hoja bila kukata tamaa. Mnazidiwa nguvu bungeni kisha mnahamia mtaani kuelimisha wananchi waikatae Katiba Inayopendekezwa. Wao suluhu ikawa kususa vikao vya bunge.

Hali hiyo ndiyo ambayo hufanya wapinzani wa Tanzania waonekane sawa na mtoto anayedeka kwa mama au baba yake wa kambo. Je, ni matarajio kweli mzazi wa kambo anaweza kumdekesha mtoto ambaye si wake? Hutokea wawili kati ya elfu.

Upinzani na chama tawala lazima kuwe na msuguano wa kimawazo, hoja kwa hoja, mikakati kwa mikakati. Lile ambalo chama tawala wataona linawafaa kwa mbinu zao za kubaki madarakani watalitumia tu. Wapinzani wa Tanzania hutaka CCM yenyewe ilegeze kamba kisha wao washinde dola kwa urahisi kabisa.

Mtoto wa kambo huwa hasusi chakula, maana akifanya hivyo ataambulia mkong’oto kisha atashinda au atalala na njaa. Wapinzani wanatakiwa kujielimisha kuwa kuwasusia CCM ni sawa na kuridhia wafanye mambo yao bila bughudha. Wanashika tu ule msemo; ukisusa wenzio tunakula.


Twendeje sasa?

Ya 2014 tumeshayaona na kususa kwa wapinzani. Huu ni mwaka wa nane tangu Katiba Inayopendekezwa ilipopatikana. Je, wenye kutaka Katiba Mpya, wanataka Inayopendekezwa ikapigiwe kura na wananchi?

Kama ilishindikana mwaka 2014 na 2015, inawezekana vipi mwaka 2022. Sababu za kutoiingiza Katiba Inayopendekezwa kwa wananchi ili ipigwe kura mwaka 2014 na 2015, sasa hivi hazipo?

Kwa mtazamo wa kawaida kabisa, ni ndoto ya mchana kuiingiza Katiba Inayopendekezwa ili ipigiwe kura leo. Kwa kuzingatia hoja ya wajumbe wa Bunge la Katiba, zaidi ya theluthi moja kuondoka kwenye vikao.

Pili, imepita miaka nane. Je, Katiba Inayopendekezwa bado haijachezewa kwa kunyofoa vipengele na kuweka vipya? Wanaotunza nyaraka wanaaminika?

Je, tuendelee tulipoishia kwenye rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba? Nayo bado ni salama? Haijanyofolewa baadhi ya mambo?

Rasimu ya Jaji Warioba ilikamilika mwaka 2013. Huu ni mwaka wa tisa. Je, katika kipindi chote hicho, mawazo ya Watanzania yapo vilevile?

Kenya walitengeneza Katiba Mpya mwaka 2010. Mwaka 2018, tayari yakaibuka mawazo ya kufanya mabadiliko ya Katiba kupitia Mpango wa Ujenzi wa Daraja la Maridhiano (BBI). Kama Kenya miaka minane walitaka Katiba ibadilike, je, Tanzania miaka tisa?

Wakati wa Bunge la Katiba, kilichokwamisha ni idadi ya serikali. Kuna waliotaka ziwe tatu, wengine mbili. Kama itaamuliwa rasimu ya Tume ya Warioba ipelekwe bungeni, mtafaruku utakuwa ulele.

Tume ya Warioba ilikusanya maoni yenye kutaka muundo wa serikali uendelee wa sasa wa nusu urais (semi presidential), ndio maana wakapendekeza serikali tatu.

Katika miaka tisa, hakuna mawazo mbadala? Ama kuachana kabisa na semi presidential na kuufuata mfumo wa urais (presidential system), vipi kuhusu serikali ya kibunge (parliamentary democracy).

Vijana wengi ambao hawakuwa na umri wa miaka 18, leo hii ni watu wazima. Wanahitaji kushiriki kutoa maoni ya Katiba wanayoitaka.

Ni kwa mawazo hayo, unaona kuwa kwa hoja nyingi, Katiba mpya inahitaji mchakato uanze upya. Tume ya Katiba iundwe upya, ikusanye maoni kwa uwazi na irahisishe watu kujitokeza kushiriki.