Katiba, ukomo urais mwiba

Thursday November 25 2021
katibapic
By Tatu Mohamed
By Peter Elias

Dar es Salaam. Wadau wa utawala bora nchini wamebainisha maeneo matano ambayo Serikali inatakiwa kuyafanyia kazi ili kujiimarisha zaidi huku wakitaka mjadala zaidi katika maeneo hayo uendelezwe.

Hayo yalibainishwa jana jijini Dar es Salaam katika mkutano ulioandaliwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) ukiwa na lengo la kuangalia nafasi ya asasi za kiraia katika mchakato wa masuala ya utawala bora Afrika.

Mkutano huo ulijikita katika kuchambua ripoti ya Mpango wa Kujitathmini Kiutawala Bora Afrika (APRM) ambapo wadau walitoa maoni kuhusu namna ya kuboresha ili kuifanya Tanzania isipoteze sifa yake ya awali.

Ripoti hiyo inabainisha kwamba Tanzania imekuwa ikitajwa kama moja ya nchi za Afrika zinazotekeleza kwa vitendo dhana ya utawala bora, demokrasia, amani na utulivu, hali inayochochea ustawi wa wananchi wake na katika Bara la Afrika.

Hata hivyo, wadau hao walibainisha kwamba miaka ya hivi karibuni, Tanzania imekuwa haifanyi vizuri katika maeneo hayo, jambo ambalo wamesema linahitaji mjadala zaidi ili kuisaidia Serikali kuboresha zaidi.ya mjadala

Hata hivyo, Serikali imetambua umuhimu wa utawala bora na kukaribisha mijadala ya wadau mbalimbali ili kuboresha eneo hilo na kuisaidia Serikali kuona namna nzuri ya kuiwezesha Tanzania kupiga hatua.

Advertisement

Mambo ambayo wanataka yajadiliwe ni pamoja na Muungano, utawala wa kisiasa na masuala ya haki za binadamu, ibara za Katiba zinazozungumzia ukomo wa Rais katika kushika madaraka, kuridhia tamko la Kiafrika la kujiunga na Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na kuanzisha mchakato wa Katiba mpya.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Mkurugenzi wa Kituo cha Taarifa kwa Wananchi (TCIB), Deus Kibamba alisema inafaa kutafakari yale ambayo yaliifanya Tanzania ing’are kwenye ripoti iliyotolewa mwaka 2013, kama bado yanaendelea kuenziwa.

“Tanzania tulitajwa tunafanya vizuri, lakini tunakaribia kuyumba. Inatakiwa tutafakari katika maeneo haya, bado tunafanya vizuri? Kwa sababu tathimini nyingine inakuja, tunaweza kujikuta tunarudi nyuma katika maeneo ambayo tulitajwa kuyafanya vizuri.

“Leo hii, huu mchakato wa Katiba tuliosifiwa nao hakuna chochote kinachofanyika, tunaona watu wameshaanza maneno maneno kuhusu ukomo wa urais, na pia kwenye Mahakama ya Afrika tayari tumeshajitoa,” alisema.

Alisema APRM inapaswa kuwa mwarobaini katika kuweka makubaliano ya wananchi na viongozi.

Kibamba alitoa wito kwa asasi za kiraia, viongozi wa dini na waandishi wa habari kuhamasisa suala la demokrasia kwa kuwa watawala peke yake hawawezi kuidumisha.

“Kwa hiyo mpango huu unakwenda kuweka vidhibiti, watawala watende mambo kulingana na makubaliano kwenye Katiba zao na kwa mujibu wa sheria za nchi hivyo tuendelee kuwakumbusha yale mambo yaliyokuwepo kwenye hiyo ripoti,” alisisitiza.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Anna Henga alisema APRM ni muhimu zaidi kwa sababu ni jambo ambalo linagusa mambo ya utawala bora kwa Afrika nzima .

“Cha muhimu ni kwamba sisi asasi za kiraia tulikuwa hatujasikia muda mrefu sana kuhusu huo mchakato, na ndio maana tukaamua tuufufue.

Ripoti iliyotoka mwaka 2013 ilizinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan wakati huo akiwa Makamu wa Rais, hivyo tunahitaji pia kuchagiza kwa Rais kwa kuwa anaifahamu vizuri hii ripoti,” alisema Henga.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Balozi Mindi Kasiga ambaye anatoka sekretarieti ya APRM iliyo chini ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, alisema ili nchi iwe na maendeleo lazima iwe na utawala bora.

“Ili kuimarisha demokrasia, wakasema tuanzishe mpango wetu, siyo utakaoletwa na wengine. Tanzania ni miongoni mwa nchi za 41 Afrika zilioukubali mpango huo.

“Utawala bora umekuwa ni kizuizi cha cha maendeleo ya bara la Afrika. Tusisubiri kutoka nje au Umoja wa Mataifa utuambie hatuna utawala bora. Afrika tujitathmini wenyewe. Utawala bora hauwezi kufanana na nchi za nje, mfano China ua Marekani. Tufanye juhudi zetu kama Waafrika,” alisema Mindi.

Akizungumzia suala la mchakato wa Katiba mpya, Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria, Profesa Sifuni Mchome alisema suala hilo ni mjadala unaoendelea.

“Changamoto ni kwamba watu wanafikiri kila wanachotaka kitatokea, haiwezi kuwa hivyo. Kundi hili linasema hivi na lingine linasema vile. Kwa hiyo suala hili la Katiba ni mjadala unaoendelea, utakapofika mwisho majibu yatapatikana,” alisema Profesa Mchome.

Naye Naibu Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Hamad Hassan Chande alizungumzia kuhusu mjadala kwenye suala la Muungano akisema ni jambo jema kwa sababu nchi ni ya wananchi wenyewe kwa hiyo kama wanaona kuna changamoto ambazo hazijabainishwa, waziwasilishe.

“Watakuwa wanatusaidia kwa sababu sisi viongozi hatuwezi kuyaona yote lakini wananchi ndiyo wanaweza kuona nini kipo. Kwa hiyo Serikali inawakaribisha wananchi wake kutoa maoni yao kuhusu Muungano,” alisema Chande.


Advertisement