Kauli ya Tanroads ujenzi barabara Nachingwea-Masasi
Muktasari:
- Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Mkoa wa Lindi umesema hakuna siasa wala uongo katika ujenzi wa barabara ya Nachingwea kwenda Masasi kwa kiwango cha lami.
Lindi. Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Mkoa wa Lindi umesema hakuna siasa wala uongo katika ujenzi wa barabara ya Nachingwea kwenda Masasi kwa kiwango cha lami.
Hayo yameelezwa leo Jumamosi Septemba 11, 2021 na meneja wa wakala huyo mkoani humo, Ephatar Mlavi katika kikao chake na wanahabari.
Mlavi amesema Serikali imedhamiria kujenga barabara hiyo na imeipa umuhimu mkubwa.
"Kwa hiyo hakuna uongo wala siasa katika ujenzi wa barabara hii inayounganisha wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi na masasi mkoani Mtwara, " amesema.
Amebainisha kuwa upembuzi yakinifu umekamilika kinachosubiriwa ni fedha ili ujenzi uanze na kwamba ujenzi wa barabara ya Nanganga-Ruangwa unaendelea baada ya kuwa na timu mbili moja ikijenga kutoka Nandagala kwenda Ruangwa na timu mbili zinaelekea Nanganga.
Amesema kazi ngumu si kuweka lami bali kuchonga milima na kujaza udongo kwenye mabonde.
"Ujenzi umeanzia katika kijiji cha Nandagala kutokana na mkandarasi kuweka kambi katika kijiji hicho ambacho kipo katikati ya Ruangwa na Nanganga, " ameeleza akigusia matengenezo katika maeneo korofi barabara za Ngongo-Ruangwa, Tingi-Kipatimo eneo la mlima Ngoge na Nangurukuru-Liwale.