Kaya 15,200 hazina vyoo Mara, zatumia maeneo yasiyo rasmi kujisaidia

Friday November 26 2021
New Content Item (1)

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Ally Hapi akifungua kikao cha kamati ya huduma za afya ya msingi. Picha na Beldina Nyakeke

By Beldina Nyakeke

Musoma. Ofisa afya wa Mkoa wa Mara, Erick Murigi amesema kaya 15,274 kati ya kaya 284,350 zilizopo katika mkoa huo hazina vyoo ikiwa ni sawa asilimia 7.4.

Takwimu hizo zimetolewa leo Novemba 26, 2021 na wakati akiwasilisha taarifa ya hali ya vyoo katika kikao cha kamati ya huduma za afya ya msingi mkoani Mara.

Amesema kuwa kutokana na kaya hizo kutokuwa na vyoo wakazi wa kaya hizo wamekuwa wakitumia maeneo yasiyo rasmi wakati wa kujisaidia ikiwa ni kwenye vyanzo vya maji, ziwani, mitoni na maeneo mengine jambo ambalo linahatarisha maisha ya wakazi wa maeneo hayo.

Amesema kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime Vijijini inaongoza kwa kuwa na idaidi kubwa ya kaya ambazo hazina vyoo na kutaja idadi hiyo kuwa ni 4,080 ikifuatiwa na Rorya yenye kaya 4,050 huku Butiama ikiwa na idadi ndogo ya kaya ambazo hazina vyoo ambayo ni 74.

Amesema kuwa katika kaya hizo zilizopo mkoani mara ni kaya 170,688 zenye vyoo bora huku kaya 98,388 zikiwa na vyoo ambavyo sio bora.

"Tunaposema vyoo bora tunamaajisha ni kile choo chenye mlango, ukuta, paa na pia kinaweza kusafishika vizuri kwahiyo katika Mkoa wa Mara kaya ambazo zina vyoo vyenye sifa hizo ni 170,688" amesema

Advertisement

Awali akifungua kikao hicho, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Ally Hapi alisema kuwa hali ya vyoo mkoani Mara ni mbaya na hivyo kusabbaisha kuwepo kwa magonjwa yanayosababishw ana uchafu.

"Watu wanajisaidia kwenye vyanzo vya maji na watu wangu wa afya wananiambia kuwa kule katika vituo vya kutolea huduma za afya magonjwa yanayosababishwa na uchafu ni mengi kuliko magonjwa ya kawaida hii haikubaliki lazima tutoke na maazimio katika kikao hiki" amesema.

Advertisement