Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kaya maskini 20,000 Tanga zaanza kunufaika na bima ya afya kwa wote

Daktari Jestina Msumari akimhudumia mmoja wa wananchi waliotembelea banda la Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) wakati wa Maonesho ya Biashara yanayoendelea katika viwanja vya Mwahako, jijini Tanga. Picha na Mbonea Herman.

Muktasari:

  • Kaya 7,816 zimeshapatiwa kadi na kuanza kutumia huduma za afya tangu Machi mwaka huu, NHIF yasema awamu ya pili inalenga kaya 1,300 zaidi huku uhakiki wa taarifa ukiendelea.

Tanga. Zaidi ya wananchi 20,000 kutoka kaya maskini mkoani Tanga wameandikishwa na wameanza kunufaika na mpango wa bima ya afya kwa wote unaolenga kuboresha upatikanaji wa matibabu kwa kaya zenye kipato cha chini.

Katika awamu ya kwanza na ya pili ya mpango huo, inalenga kaya zenye kipato cha chini, hatua inayotarajiwa kuboresha afya na ustawi wa jamii.

Kundi hilo linafadhiliwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf), lengo likiwa kupunguza changamoto ya wananchi kushindwa kumudu gharama za matibabu.

Zaidi ya wanufaika 20,000 kutoka kaya 7,816 wameshapatiwa kadi za bima, na wanufaika hao wameanza kutumia huduma hizo tangu Machi mwaka huu.

Akizungumza na Mwananchi, leo Juni 9, 2026 Dk Lawi Kupaza wa Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF), amesema mwitikio wa wananchi ni mkubwa na wengi waliostahili wamepatiwa kadi zao.

Amesema awamu ya pili inalenga kufikia kaya 1,300 zaidi na kwamba kazi ya ugawaji wa kadi unaenda sambamba na uhakiki wa taarifa zao.

“Kuna changamoto ya kuwafikia wanufaika wote kwa wakati. Hii inatokana na ratiba na ukubwa wa eneo la utekelezaji. Hata hivyo, watendaji wa kata na vijiji wanaendelea kusaidia uhamasishaji,” amesema Kupaza.

Ofisa madai wa mfuko huo, Neema Kisinga, ameitaka jamii kujiunga na bima, akisema kuna vifurushi mbalimbali vinavyowezesha kupata huduma kwa gharama nafuu. Hii inasaidia kupunguza mzigo wa kulipa kila unapohitaji matibabu.

Ofisa huyo anatoa mfano wa kifurushi cha Tarangire ambacho kinahusisha matibabu, vipimo na huduma za daktari. Hii ni tofauti na asiye na bima anayelazimika kulipa kila huduma.

Mratibu wa wanufaika wa Tasaf, Joicy Mshimbula, amesema mpango huo unasaidia kaya maskini kupata matibabu.


Ameeleza kuwa watu wengi walikuwa wanashindwa kumudu gharama za hospitali, hali iliyokuwa ikiwaacha wengi bila huduma muhimu.

Amesema baadhi ya wananchi huugua kwa muda mrefu bila matibabu sahihi, na wengine hutumia dawa za maumivu kama paracetamol wakisubiri fedha, hali ambayo huchelewesha tiba na kuongeza madhara ya kiafya.

Mmoja wa wanufaika, Asha Juma, amesema kuwa kukosa bima kunaleta changamoto kubwa wakati wa kuugua. Ameeleza kuwa mara nyingi hulazimika kusubiri fedha ili kuanza matibabu, hali ambayo huathiri afya ya binadamu na kuchelewesha kupona.

“Hata hapa ninapokuambia, ninaumwa malaria na UTI, lakini sina fedha. Nimebaki na karatasi tu. Ninasubiri nipate fedha ndiyo nikanunue dawa na kuanza dozi,” amesema Asha Juma, ambaye anasubiri awamu ya pili ya mpango huo.