Kazi atakayoifanya Lissu hadharani

Muktasari:

Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu amesema kazi kubwa atakayoifanya baada ya kurejea nchini akitokea Ubelgiji ni kutengeneza nguvu ya umma kwa ajili ya Taifa ili ipatikane Katiba mpya.


Dar es Salaam. Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu amesema kazi kubwa atakayoifanya baada ya kurejea nchini akitokea Ubelgiji ni kutengeneza nguvu ya umma kwa ajili ya Taifa ili ipatikane Katiba mpya.

Lissu ametoa kauli hiyo leo Jumatano, Januari 25, 2023 katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Bulyaga wilayani Temeke ambapo pia ulikuwa kwa ajili ya kumpokea.

"Mwenyekiti wetu na chama chetu tulipata nafasi ya kuzungumza na Rais Samia Suluhu Hassan na akakubali tuzungumzie mambo yetu na mustakbali wa Taifa letu, huko nyuma kwa hayati Magufuli ilishindikanaā€¯ amesema.

Amesema wataendelea na mazungumzo hata yeye amechangia katika mazungumzo yaliyokuwa yanafanyika lakini kinachotakiwa ni kupatikana kwa Katiba mpya.

"Tukiamua tutapata Katiba mpya kabla ya mwaka 2025 na Tume hintapatikana kama Katiba mpya itapatikana,"

Amesema endapo watamsadia Mbowe katika kudai katiba inawezekana lakini kama Watanzania watalegalea haitawezekana.

"Tukijenga shinikizo lenye nguvu kweli tutapata Katiba mpya kabla ya mwaka 2025 na tukipata hiyo tutapata Tume huru ya Uchaguzi, tume haiundwi nje ya Katiba," amesema.

"Tutafute namna ya kuhakikisha wote wanaoumizwa na utaratibu huu, ili tumpe nguvu Mwenyekiti na timu yake ya kwenda kudai kwenye hayo mazungumzo," amesema.