KCBL yajipanga kukuza mtaji kufikia Sh15 bilioni
Meneja Mkuu wa KCBL, Godfrey Ng'ura wakati akizungumza katika moja ya tukio la benki hiyo. Picha na mtandao
Muktasari:
- Benki ya Ushirika ya Kilimanjaro (KCBL) imejipanga kushirikiana na wadau pamoja na vyama vya ushirika nchini, kuhakikisha mtaji wake unakuwa hadi kufikia Sh15 bilioni ili kufikia lengo la kuwa benki ya kitaifa ifikapo mwezi Juni mwaka huu.
Moshi. Benki ya Ushirika ya Kilimanjaro (KCBL) imejipanga kushirikiana na wadau pamoja na vyama vya ushirika nchini, kuhakikisha mtaji wake unakuwa hadi kufikia Sh15 bilioni ili kufikia lengo la kuwa benki ya kitaifa ifikapo mwezi Juni mwaka huu.
Hayo yamebainishwa na Meneja Mkuu wa KCBL, Godfrey Ng'ura wakati akizungumza kwenye mkutano uliowakutanisha waandishi wa habari na wadau mbalimbali uliokuwa na lengo la kuekezea mafanikio yaliyopatikana jatika kipindi cha miaka miwili.
Ng'ura amesema Benki hiyo ambayo kwa sasa ina mtaji wa Sh5.2 bilioni inahitaji Sh9.8 bilioni hadi kufikia mwezi Juni mwaka huu ili kuweza kutangazwa kuwa Benki ya Taifa ya Ushirika.
"Katika mchakato huu wa kuwa na benki ya Taifa ya ushirika, benki ya KCBL inashirikiana na Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC), Benki ya CRDB, Sccult, TFC na vyama vya ushirika nchini, kuanzisha benki ya Taifa ya ushirika kupitia KCBL kwa kufanya mageuzi ya kimfumo na uendeshaji," amesema.
"Tunategemea kuupata mtaji ifikapo mwezi Juni mwaka huu kwani ili kuwa benki ya ushirika ya Taifa, tuna upungufu wa mtaji wa Sh9.8 bilioni na tunatarajia tutazipata kutoka kwa wadau, watu binafsi na vyama vya ushirika na kufikia lengo la kuwa benki ya ushirika ya Taifa mwezi juni mwaka huu," amesema.
Akitaja mafanikio ya benki hiyo, Ng'ura amesema wameweza kuongeza akaunti mpya zinazofanya miamala ya wateja kufikia 21,000 mwaka 2022 kutoka akauti 15,000 za mwaka 2021 huku mtaji wa wanahisa ukifikia Sh4.4 bilioni mwaka 2022 kutoka Sh2.7 bilioni mwaka 2021.
Aidha amesema faida ya benki baada ya kodi imeongezeka kwa asilimia 12, kutoka Sh293 milioni mwaka 2021 hadi kufikia Sh327 milioni mwaka 2022, huku mali za benki zikikua kutoka Sh8.4 bilioni mwaka 2021 hadi kufikia Sh11 bilioni mwaka 2022.
Akizungumza mrajisi wa vyama vya ushirika nchini, Dk Benson Ndiege amesema benki ya ushirika ni moja ya eneo ambalo liliathirika na ubadhirifu na kuisababishia kuyumba na kwamba kwa sasa vyombo vya dola vinaendelea na kazi yake ili kuhakikisha wote waliohusika wanaendelea kuchukuliwa hatua za kisheria.
“Pamoja na changamoto za kibiashara, lakini benki hi hapo nyuma ilikuwa na watu ambao hawana weledi na hiki ndicho kilichoifikisha benki hii hapa Pamoja na changamoto ya wizi na ubadhirifu na katika mageuzi ambayo tunayafanya tunaangalia kitu gani tufanye ili benki hii iendelee kuchanja mbuga kimafaniikio,” alisema Dk Ndiege.
Ameongeza kuwa, “Tunatakiwa tuwe na watendaji ambao kweli wanaweza kutusaidia katika benki hii na suala la uadilifu ilikuwa ni changamoto hapo awali. Niwaahidi kama kuna wale walioshiriki kuua benki hii wakati ule, sasa vyombo vya dola vinaendelea na kazi yake na kama ulichukua hata senti moja utairudisha kwa sababu ilikuwa ni mali ya wanaushirika au mtu fulani aliyekuwa amewekeza katika benki,” amesisitiza.
“Nitumie nafasi hii kupongeza menejimenti hii ya sasa ya KCBL kwa jinsi wanavyofanya kazi kwa uwazi, uadilifu na hakuna mtu yeyote ambaye anaweza kuuliza maana taarifa zote zipo. Mikakati mingine ambayo tunaiangalia ni kuendelea kuipanua hii benki iwe na wigo mkubwa wa kibiashara,”amesema.