KCMC yahuisha mfumo wa ukusanyaji mapato

Muktasari:
- Hospitali ya KCMC imehuisha makubaliano yanayoifanya Benki ya CRDB, kuwa mtoa huduma za kifedha katika ukusanyaji wa maduhuli hospitalini hapo, ambapo kwa miaka nane, imekusanya Sh52.8 bilioni, huku ikimaliza tatizo la upokeaji wa fedha bandia.
Dar es Salaam. Hospitali ya KCMC imehuisha makubaliano yanayoifanya Benki ya CRDB, kuwa mtoa huduma za kifedha katika ukusanyaji wa maduhuli hospitalini hapo.
Uamuzi huu unafuatiana mafanikio katika mfumo wa ukusanyaji mapato, ambapo kwa miaka nane, imekusanya Sh52.8 bilioni, huku ikimaliza tatizo la upokeaji wa fedha bandia.
Hayo yamebainishwa leo Alhamisi Septemba 21, 2023; na Mkurugenzi Mkuu wa hospitali hiyo, Profesa Gileard Masenga, huku akisema: “Kabla hatujaanza kutumia mfumo wa CRDB, tulikuwa tunakusanya mapato kidogo.”
“Kama mnavyofahamu uendeshaji wa hospitali ni wa gharama kubwa, hivyo usimamizi wa mapato ni kati ya vipaumbele muhimu vya hospitali yoyote. Ndiyo maana leo tupo tena hapa kuuhuisha mkataba wetu ili kuendelea kuwa na ufanisi mkubwa katika ukusanyaji wa mapato yetu,” amesema Profesa Masenga.
Awali, mkurugenzi huyo amesema wahasibu walilazimika kukaa na fedha nyingi jambo lilikuwa ni hatari, na kwamba hiyo ndiyo sababu menejimenti kushawishika kutumia teknolojia ya kisasa na hivyo kuongeza ufanisi katika usimamizi wa mapato.
“Uhusiano wetu hauishii kwenye huduma za benki kwani KCMC ni miongoni mwa wanufaika wa uwekezaji unaofanywa kwa jamii na benki hiyo. CRDB wametujengea eneo la mapumziko na ili kuboresha huduma, mara kadhaa wametusaidia vifaa tiba na kompyuta,” amesema.
Kwa upande wake Boma Raballa ambaye ni Ofisa Mkuu wa Biashara wa benki hiyo, amesema waliingia makubaliano na hospitali hiyo 2014, ubia ulienda sambamba na uzinduzi wa kadi maalumu ya malipo iliyopewa jina “TemboCard KCMC.”
“Katika mwaka wa kwanza tangu kuanza kutumika kwa mfumo huo hospitalini hapo, zaidi ya Sh4.1 bilioni zilikusanywa. Sasa makusanyo ya mwaka yameongezeka ambao kwa 2022, hospitali ilikusanya Sh8.7 bilioni,” amesema.
Kulingana na ofisa huyo, azma ya benki yake ni kuhakikisha inatoa huduma bora na shindani zinazokidhi mahitaji ya wateja wake, na kwamba huduma hizo ni muhimu kwa maendeleo ya taifa.
“Tangu tulipoingia mkataba na Hospitali ya KCMC kuanza kuutumia mfumo wetu mpaka mwaka jana, tumeiwezesha Hospitali ya KCMC kukusanya zaidi ya Sh52.8 bilioni. Hiki ni kiasi kikubwa kukusanywa ndani ya miaka minane na makusanyo yamekuwa yakiongezeka kila mwaka,” amesema Raballa.
Raballa amesema katika kuimarisha ushirikiano na hospitali na pia ili kusogeza karibu zaidi huduma kwa wateja wake mwaka 2020 Benki ya CRDB ilifungua tawi hospitaini hapo.
Amesema tawi hilo linawafaa pia wafanyakazi wa hospitali, wanafunzi wanaojifunza hospitalini hapo, wagonjwa, wafanyabiashra na wananchi kwa ujumla wanaoishi au kupita maeneo ya hospitali.