Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kero ya foleni Mbagala yapata suluhu, malori yaondolewa

Muktasari:

  • Bandari Kavu ya Mbagala imepata eneo la maegesho la malori na kutumia mfumo wa namba za foleni, hatua iliyopunguza msongamano na foleni barabara ya Kilwa eneo la Zakhem na kuongeza ufanisi wa huduma kuondoa malalamiko ya madereva.

Dar es Salaam. Bandari kavu ya Mbagala jijini Dar es Salaam imepata eneo la maegesho ya malori katika juhudi za kupunguza msongamano na foleni ya magari iliyokuwa ikijitokeza nje ya bandari hiyo.

Hatua hiyo imekuja baada ya Mwananchi Juni 7, 2026 kuripoti kuhusu maegesho holela ya malori yanayoingia kwenye bandari kavu yanavyochangia foleni jijini Dar es Salaam.

Mfululizo wa habari hizo, ziliangazia athari za kiuchumi na utoaji wa huduma na jinsi ambavyo wananchi wamekuwa wakisota barabarani.

Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) imechukua hatua ya kuondoa malori yaliyoegeshwa barabarani.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumanne, Juni 9,2026, msimamizi wa bandari kavu ya Mbagala Kurasini, Jackson Mkama amesema eneo hilo jipya lililopo umbali wa takribani mita 200 hadi 300 kutoka kituo hicho, bado kuna nafasi ya kutosha ndani ya bandari inayoweza kuhudumia malori mengi zaidi.

Hali ilivyo katika Bandari Kavu ya Mbagala baada ya kuondolewa kwa malori yaliyokuwa yameegeshwa eneo hilo na kuwa kero kwa watumiaji wa barabara ya Kilwa

Amesema hatua hiyo ni sehemu ya maandalizi ya kukabiliana na ongezeko la mizigo linalochochewa na maboresho yanayoendelea kufanywa na Serikali katika sekta ya usafirishaji na bandari.

“Tumepata eneo jingine jirani na hapa lenye uwezo wa kuhifadhi magari zaidi ya 50 hadi 70 kwa wakati mmoja, pia ndani ya bandari tuna eneo la kutosha kwa ajili ya maegesho na shughuli nyingine za upakiaji na upakuaji wa mizigo,” amesema Mkama.

Amesema awali kulikuwa na changamoto ya baadhi ya malori kuegeshwa nje ya bandari wakati wa kusubiri huduma, lakini maboresho yaliyofanyika yameondoa hali hiyo na kuongeza ufanisi wa utoaji huduma.

Mkama amesema bandari hiyo ina mashine na vifaa vya kutosha vinavyoweza kuhudumia hadi makontena 300 kwa siku bila kuathiri shughuli nyingine za uendeshaji.

Amesema kwa sasa malori yanapangwa katika eneo maalumu la maegesho na kufuata utaratibu wa kuandikwa namba ya foleni, jambo linalorahisisha huduma na kuondoa migogoro miongoni mwa madereva.

Hata hivyo, amesema changamoto inayojitokeza kwa sasa ni baadhi ya mawakala na wamiliki wa mizigo kuchelewa kukamilisha taratibu za kuchukua makontena yao, jambo linalosababisha mizigo kukaa kwa muda mrefu kwenye yadi.

“Tunawaomba mawakala kuchukua mizigo yao kwa wakati ili kutoa nafasi kwa makontena mapya yanayoingia kila siku, sisi tumejipanga na tunaendelea kutoa huduma saa 24,” amesema.

Aidha, amesema bandari hiyo imeandaa maeneo maalumu ya kuhifadhi makontena ya muda mrefu bila kuathiri shughuli za kawaida za upokeaji na utoaji mizigo.

Amesema bandari kavu ya Mbagala kwa sasa ina uwezo wa kuhudumia zaidi ya malori 40 kwa wakati mmoja, huku ikiendelea kuimarisha huduma zake ili kuendana na ukuaji wa biashara nchini.

Pia, amesema bandari hiyo inaendelea kuboresha huduma zake sambamba na utekelezaji wa maboresho ya Serikali katika sekta ya usafirishaji, ili kuhakikisha ongezeko la biashara linaendana na uwezo wa kuhudumia mizigo kwa haraka na ufanisi.

Hali ilivyo katika Bandari Kavu ya Mbagala baada ya kuondolewa kwa malori yaliyokuwa yameegeshwa eneo hilo na kuwa kero kwa watumiaji wa barabara ya Kilwa

Dereva wa lori, Maulid Mkambala amesema utaratibu wa sasa umewasaidia kuanzishwa kwa eneo hilo la maegesho kumesaidia kuleta utaratibu tofauti na ilivyokuwa awali.

Amesema zamani madereva walikuwa wakipigiwa simu kwenda kuchukua au kupakia mizigo, lakini walipofika bandarini walikuta magari mengine tayari yameingia mbele yao jambo lililosababisha malalamiko na kupoteza muda.

“Awali tulikuwa tunaitwa kuja kupakia mizigo, lakini ukifika unakuta kuna magari mengine yameshaingia mbele yako, ilikuwa vigumu kujua nani alitangulia kwa sababu hakukuwa na mfumo wa namba au utaratibu maalumu wa kupanga magari,” amesema Mkambala.

Mkazi wa Kongowe anayefanya kazi Ubungo, Frank James amesema barabara hiyo ilikuwa kero kubwa na iliwafanya kuchelewa kufika majumbani mwao.

“Jamani hongereni sana Mwananchi, habari ambayo mliandika naona imezaa matunda huku, leo sijaona lori barabarani, yaani nimetumia muda mchache sana kutoka Ubungo hadi Mbagala,” amesema James.