Kesi ya anayedaiwa kughushi vibali Wizara ya Madini yaiva

Watu saba wafikishwa kortini wakidaiwa kujipatia Sh 428milioni mali ya Tanesco

Muktasari:

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imepanga Agosti Mosi, 2022  kumsomea hoja za awali (PH) Anthony Magoe (35) anayekabiliwa na mashtaka sita likiwemo la kughushi vibali vya kusafirisha madini kutoka Wizara ya Madini na kujipatia Sh1.3bilioni kwa njia ya udanganyifu.

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imepanga Agosti Mosi, 2022  kumsomea hoja za awali (PH) Anthony Magoe (35) anayekabiliwa na mashtaka sita likiwemo la kughushi vibali vya kusafirisha madini kutoka Wizara ya Madini na kujipatia Sh1.3bilioni kwa njia ya udanganyifu.

Hiyo ni baada ya upelelezi wa kesi hilo ya jinai namba 74/2022 kukamilika.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Grace Mwanga ameieleza Mahakama hiyo leo Alhamisi Juni 30, 2022, mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Godfrey Isaya, wakati shauri hilo lilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.

Wakili Mwanga baada ya kueleza hayo, hakimu Isaya ameahirisha kesi hiyo hadi Agosti Mosi, atakaposomewa mashtaka.

Kwa mara ya kwanza, mshtakiwa huyo alifikishwa mahakamani Mei 16, 2022 kujibu mashtaka yanayomkabili.

Katika kesi ya msingi, kati ya Januari 18, 2022 na Februari 16, 2022 katika Jiji la Dar es Salaam, Magoe anadaiwa kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kiasi cha  dola za Marekani 602,747, ambazo ni sawa na Sh 1,386, 318,100 kutoka Kampuni ya Macbrusa Pyt  Ltd, kuwa fedha hizo ni kwa ajili ya kuonyesha sampuli za madini, wakati akijua ni uongo.

Februari 9, 2022 katika Jiji hilo, alighushi kibali cha mauzo ya madini chenye namba 11000911 akionyesha kwamba kimetolewa na Wizara ya Madini, wakati akijua ni uongo.

Shtaka la tatu, Januari 19, 2022 alighushi kibali cha mauzo ya sampuli za madini cha tarehe Januari 19, 2022 akionyesha kuwa kimetolewa na Wizara hiyo.

Mshtakiwa pia anadaiwa kughushi maombi ya kibali cha mauzo ya madini nje ya nchi cha Januari 19, 2022 akionyesha kuwa kimetolewa na Wizara ya Madini, wakati akijua kuwa ni uongo.

Shtaka la tano na la sita, Magoe anadaiwa kughushi risiti, akionyesha kuwa risiti hizo zimetolewa na Wizara ya Madini, wakati akijua kuwa ni uongo.

Mshtakiwa yupo nje kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya dhamana, ambayo ni kuwasilisha mahakamani fedha taslimu Sh750 milioni au hati ya mali  isiyohamishika yenye thamani hiyo pamoja na wadhamini yenye barua kutoka Serikali ya Mitaa.