Kesi ya Sabaya kuunguruma wiki moja mfululizo

Muktasari:

  • Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha imepanga kusikiliza mfululizo kwa wiki nzima kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake sita kuanzia Oktoba 18, 2021.

Arusha. Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha imepanga kusikiliza mfululizo kwa wiki nzima kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake sita kuanzia Oktoba 18, 2021.

Hatua hiyo inakuja baada ya leo Oktoba 13, shauri hilo kutajwa mbele ya Hakimu Mkazi Patricia Kisinda, ambapo Jamhuri iliwakilishwa na wakili wa Serikali, Neema Mbwana huku watuhumiwa hao wakiwakilishwa na Wakili Fauzia Mustapha.

Wakili Neema ameieleza mahakama hiyo kuwa shauri hilo lilikuja kwa ajili ya kutajwa kuendelea kusikilizwa na walishakubaliana pande zote hivyo wanaomba tarehe kwa ajili ya kuendelea kusikiliza.

Hakimu Kisinda amesema shauri hilo litaendelea kusikilizwa kwa wiki nzima mfululizo kuanzia Oktoba 18, mwaka huu.

Washitakiwa wengine katika shauri hilo la uhujumu namba 27, 2021, ni pamoja na Enock Mnkeni, Watson Mwahomange, John Aweyo, Sylvester Nyegu, Jackson Macha na Nathan Msuya.

Washitakiwa hao wanakabiliwa na makosa matano likiwemo la kuongoza genge la uhalifu na kosa la utakatishaji fedha ambapo washitakiwa wote saba wanadaiwa kupata Sh90 milioni kutoka kwa mfanyabiashara Fransis Mrosso, huku wakijua kupokea fedha hizo ni zao la kosa la vitendo vya rushwa.

Makosa mengine matatu yanamhusu Sabaya peke yake.