Kesi ya uhaini 1985: Meja Jenerali Mayunga atoa ushahidi -51

Kesi ya uhaini 1985: Meja Jenerali Mayunga atoa ushahidi -51

Muktasari:

  • Shahidi wa 56 upande wa mashtaka, Meja Jenerali Silasi Mayunga aliiambia Mahakama Kuu kwamba alikutana na Pius Lugangira mara nne na mara tatu kati ya hizo Lugangira alizungumzia nia ya kuiuzia JWTZ vifaa vya mawasiliano ya kijeshi.

Shahidi wa 56 upande wa mashtaka, Meja Jenerali Silasi Mayunga aliiambia Mahakama Kuu kwamba alikutana na Pius Lugangira mara nne na mara tatu kati ya hizo Lugangira alizungumzia nia ya kuiuzia JWTZ vifaa vya mawasiliano ya kijeshi.

Mahakama pia iliambiwa na shahidi wa 55 wa upande wa mashtaka, Meja Deogratias Asanta kwamba alipewa orodha ya maofisa watano wa jeshi waliotakiwa kukamatwa kati ya usiku wa Januari 7 na asubuhi ya Januari 8 mwaka 1983. Maofisa hao ni Luteni Kanali Martin Msami, Kapteni Harry Poppe, Kapteni Zacharia Poppe, Kapteni Roderic Roberts na Kapteni Mapunda.

Akitoa ushahidi wake, Meja Jenerali Mayunga ambaye alikuwa matibu wa CCM Kilimanjaro pia, aliieleza mahakama kwamba wakati wote alipokutana na Lugangira alijua ni raia wa Uganda.

Mayunga alisema walikutana na Lugangira mara ya kwanza mjini Kampala, Uganda kwenye Hoteli ya Nile Mansion mwaka 1979 baada ya vita na alijitambulisha kuwa ni Mganda.

Akiongozwa na Mkurugenzi wa Mashtaka, William Sekule, askari huyo alisema alikutana na Lugangira kwa mara ya pili ofisini kwake, makao makuu ya Jeshi la Wananchi, Mgulani jijini Dar es Salaam. Ilikuwa Agosti 1982.

Alikutana naye tena mara mbili katika Hoteli ya Bushtrekker. Mara zote tatu walizokutana Dar es Salaam, alikuwa ameongozana na mshtakiwa wa tatu, Luteni Eugene Maganga.

Sekule: Unamfahamu Luteni Eugene Maganga?

Mayunga: Ndiyo. Namfahamu.

Sekule: Tangu lini?

Mayunga: Tangu mwaka 1968 wakati anasoma kwenye Sekondari ya Milambo, Tabora.

Sekule: Baada ya hapo?

Mayunga: Baada ya hapo tulimfanyia mpango akajiunga na Jeshi la Wananchi Tanzania.

Sekule: Alifikia cheo gani?

Mayunga: Alifanya vizuri kwenye masomo yake huko Monduli akifikia cheo cha Luteni.

Sekule: Umesema Lugangira alikuja ofisini kwako Agosti 1982. Alikuja peke yake?

Mayunga: Alikuja na Luteni Maganga.

Sekule: Maganga ndiye aliyemtambulisha Lugangira?

Mayunga: Maganga alimtambulisha lakini nilikuwa bado namkumbuka.

Sekule: Lugangira alikuja kukuona kwa madhumuni gani?

Mayunga: Madhumuni yake yalikuwa biashara. Alisema ana vifaa vya mawasiliano ya kijeshi ambavyo alitaka kuviuza Tanzania.

Baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka kumaliza kumwongoza shahidi, Wakili Murtaza Lakhaa aliyewatetea Hatibu Gandhi (Hatty McGhee), Kapteni Christopher Kadego na Luteni Eugene Maganga, alimuuliza iwapo alishangaa kusikia kuwa Maganga alihusika na mpango wa uhaini kwani tangu mwaka 1968 alimjua kuwa ni kijana mtulivu, mwenye nidhamu kubwa na anayeendelea vizuri na Meja Jenerali Mayunga akasema alishangaa sana.

Lakha: Hakuna wakati wowote ambapo Maganga alionyesha tofauti katika vitendo vyake wala kwa siasa za nchi?

Mayunga: Sikuona tofauti yoyote katika vitendo vyake.

Lakha: Maganga alipokuja na Lugangira alimtambulisha kwako kama mfanyabiashara anayetaka kuliuzia Jeshi la Wananchi vifaa vya mawasiliano ya kijeshi?

Mayunga: Jinsi ulivyoona ni kwamba Maganga alimchukulia Lugangira kuwa ni mfanyabiashara?

Lakha: Ndiyo.

Mayunga: Kitendo cha Maganga kumleta Lugangira kwenye makao makuu ya Divisheni ulikiona cha kawaida?

Lakha: Ni jambo la kawaida kabisa. Mara kwa mara wafanyabiashara walikuwa wakija makao makuu ya Divisheni.

Mayunga: Je, kukutana na Lugangira kwenye Hoteli ya Bushtrekker kama mfanyabiashara uliona ni jambo la kawaida?

Lakha: Ni jambo la kawaida na si la kutilia shaka.

Alipoulizwa na Wakili E. Mbuya aliyesaidiana na Wakili T. J. Tarimo kuwatetea Kapteni Dietrich Oswald Mbogoro, Kapteni Zacharia Hans Pope na Luteni Badru Rweyongeza Kajaja kama maofisa wa jeshi wanatakiwa kukamatwa na watu wa vyeo gani, Meja Jenerali Mayunga alisema kwamba hata ofisa wa cheo kidogo anaweza kumkamata ofisa wa cheo cha juu kwa manufaa ya nchi.

Wakili Shyam Jadeja ambaye aliwatetea Luteni Paschal Christian Chaika, Luteni John Chitunguli na Luteni Mark Augustine Mkude, alimwambia shahidi ingawa hapendi kulaghai mtu, hatokuwa amekosea kusema shahidi huyo ni ofisa anayeheshimiwa sana na jeshi pamoja na Taifa, kisha akamuuliza iwapo anafahamu hivyo. Shahidi alisema anafahamu.

Jadeja: Januari 1983 kulikuwa na uvumi kwamba unahusika na njama za kuipindua Serikali lakini hukuhusika, au siyo?

Mayunga: Sikuhusika.

Jadeja: Je, unakumbuka kuwa uliandika taarifa polisi?

Mayunga: Ndiyo. Nakumbuka.

Jadeja: Uliiandikia wapi?

Mayunga: Ofisini kwangu.

Jadeja: Iliandikwa na nani?

Mayunga: Niliandika mwenyewe.

Jadeja: Je, kuna ukweli kwamba ulihusika na njama za kuiangusha Serikali ila ulisafiri nje baada ya kuwaambia wenzako kwamba iwapo watafanikiwa, ukirudi utawaunga mkono?

Mayunga: Hakuna ukweli wowote.

Jadeja: Habari hizo ni upuuzi?

Mayunga: Ni upuuzi na uzushi mtupu.

Jadeja: Lugangira aliwahi kukuambia kuna haja ya kufanya mabadiliko hapa nchini?

Mayunga: Hapana.

Jadeja: Kwako Pius Lugangira alionekana kama mfanyabiashara?

Mayunga: Ndiyo.

Jadeja: Kwa kuwa hakuwahi kuzungumza kupindua nchi, ungeshangaa kusikia Pius Lugangira huko nje anatangaza unaunga mkono mpango wa kupindua nchi?

Mayunga: Ningeshangaa sana.

Wakili aliyemtetea Christopher Pastor Ngaiza, Wakili Hussein Muccadam, alipomuuliza Meja Jenerali Mayunga walikuwa wakizungumza nini na Lugangira katika Hoteli ya Bushtrekker, shahidi alisema walizungumzia biashara.

Muccadam: Sasa unafanya kazi ya kisiasa. Umewahi kuhusika na siasa?

Mayunga: Mimi ni muumini wa chama. Nilikuwa muumini wa Tanu ambayo ilinipeleka kusoma Israel. Chama ndicho kilinijenga kisiasa na kijeshi. Uumini wangu katika chama ulionihamasisha kugombea ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa mwaka 1982.

Muccadam: Kuna mtu yeyote aliyewahi kukushawishi juu ya mapinduzi?

Mayunga: Hakuna aliyewahi.

Muccadam: Kama angetokea ungefanya nini?

Mayunga: Ningemkamata au kutoa ripoti juu yake.

Mzee wa baraza, Lawrence Saguti, alimuuliza shahidi jinsi Pius Lugangira alivyojitambulisha alipokutana naye mara ya kwanza mjini Kampala, Uganda naye akasema alijieleza kuwa ni Mganda.

Saguti: Ulijua kwamba ni mfanyabiashara?

Mayunga: Wakati huo sikujua maana alikuwa na wenzake kwani walikuwa wakija Waganda wengi kutupongeza wakituita wakombozi.

Saguti: Ni wakati gani ulipotambua kwamba Lugangira ni Mtanzania.

Mayunga: Hata mara zote tatu tulizokutana Dar es Salaam nilikuwa namtambua kuwa ni Mganda.

Saguti: Ulimfahamu vipi Maganga?

Mayunga: Nilimfahamu kama rafiki. Alikuwa akiniita kaka yake kutokana na tofauti ya umri wetu.

Alipomaliza kutoa ushahidi wake, Jaji Kiongozi alimuuliza ni vipi asimuulize Maganga jinsi alivyofahamiana na Lugangira kwa kuwa alimfahamu tangu Uganda.

Meja Jenerali Mayunga alisema hakumuuliza Maganga kwa sababu mwingiliano kati ya Tanzania na Uganda ulikuwa mkubwa na hakuwa na wasiwasi na Maganga. Alimwambia Jaji Kiongozi hakumbuki iwapo katika Hoteli ya Bushtrekker, Lugangira alikuja na Maganga au yeye ndiye alikuja na Maganga kwa sababu mara nyingi walikuwa pamoja ila anafikiri mara zote mbili Lugangira ndiye aliyemkuta hapo hotelini.

Aliifafanulia mahakama kwamba hakuwa na ahadi na Lugangira kukutana Bushtrekker isipokuwa Lugangira alikuwa akimfuata hapo kwa sababu ni mahali ambapo (Mayunga) alizoea kwenda.

Itaendelea Kesho