KESI YA UHAINI 1985:Tamimu auawa, kesi ya wenzake yaanza-2

Tamimu auawa, kesi ya wenzake yaanza-2

Muktasari:

  • Jana tuliona jinsi mambo yalivyokuwa alipofuatwa nyumbani kwake Kinondoni Mkwajuni na wanausalama, kinara wa mapinduzi, Mohamed Tamimu baada ya kuruka ukuta na kutoroka huku wanausalama wakimwandama.

Baada ya mapambano na wanausalama yaliyodumu kwa karibu saa mbili eneo la Leaders Club hadi eneo la Drive In (sasa Ubalozi wa Marekani), Tamimu alizidiwa, akauawa kwa kupigwa risasi.

Pamoja na yeye kuuawa, wenzake waliendelea kukamatwa na baadaye kufikishwa mahakamani.

Kesi yaanza

Kesi ya uhaini iliyowakabili watu 19 wakiwamo wanajeshi 14 ilianza kusikilizwa na Jaji Kiongozi, Nassor Mzavas katika Mahakama Kuu mjini Dar es Salaam Januari 21, 1985.

Washtakiwa hao walisomewa mashtaka manne na upande wa mashtaka uliosimamiwa na timu ya watu wanne wakiongozwa na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Jinai, William Sekule.

Wengine waliokuwa katika timu hiyo ya upande wa mashtaka ni Johnson Mwanyika, Kulwa Massako na George Mlawa.

Washtakiwa katika kesi hiyo pamoja na mawakili wao ni Hatty MaGhee, Kapteni Christopher Kadego na Kapteni Eugene Maganga waliotetewa na Wakili Murtaza Lakha. Washtakiwa wengine ni Suleiman Kamando, Kapteni Vitalis Mapunda na Kapteni Roderic Roberts ambao walitetewa na wakili Thomas Mkude. Washtakiwa Luteni Paschal Chaika, Luteni John Chitunguli na Luteni Mark Mkude walitetewa na wakili Shyam Jadeda.

Mawakili J. T. Tarimo na E. H. Mbuya, kwa pamoja waliwatetea washtakiwa Kapteni Oswald Mbogoro, Kapteni Zacharia Hans Pope na Luteni Badru Kajaje.

Washtakiwa Christopher Ngaiza ambaye hadi alipokamatwa alikuwa mshauri wa Rais, Luteni Gervas Rweyongeza na Luteni Otmar Haule walitetewa na mawakili wawili ambao ni Hussein Muccadam na Mohammed Ismail.

George Banyikwa pamoja na mkewe Zera Banyikwa ambaye alikuwa mwanamke pekee katika kesi hiyo, pamoja na Luteni Nimrod Faraji, walitetewa na Francis Uzanda. Wakili Mahendra Raithatha alimtetea mshtakiwa Livinus Rugaimukamu.

Waliposomewa maelezo ya awali ya mashtaka yao Ijumaa ya Novemba 23, 1984 mbele ya Jaji Anthony Bahati wa Mahakama Kuu, ilidaiwa kwamba katika kipindi cha Januari 10, 1983 washtakiwa hao kwa pamoja wakishirikiana na Pius Mutakubwa Lugangira au ‘Uncle Tom’ na Mohammed Mussa Tamim pamoja na watu wengine wasiofahamika kula njama za kumuua Rais ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu kati ya Juni 1982 na Januari 1983.

Wakati kesi ikiwa katika hatua za awali, Juni 1983 Uncle Tom alitoroka akiwa rumande na kuacha gumzo.

Katika kuiendesha kesi hiyo, walitajwa wazee sita ambao miongoni mwao walichaguliwa wasiozidi wanne kumsaidia jaji katika kuisikiliza kesi hiyo. Wazee hao ni Lawrence Saguti, Jacob Ramadhani, Alhaji Mohamed S. H. Kingalilo, Anna Kirunda, Saidi Ally na Stephen Mlatie.

Wakati akieleza mipango ambayo Mahakama Kuu ya Tanzania ilikuwa inaitayarisha na kujiandaa katika kufanikisha usikilizaji wa kesi hiyo, Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Thomas Mihayo alisema maelezo yote ya yaliyotolewa wakati wa usikilizaji wa kesi yangenaswa moja kwa moja na chombo cha kunasia sauti, Verbatim Tapping Instrument’, kilichoagizwa na Mahakama kutoka nje ya nchi kwa gharama ya Sh400,900.

Mihayo alisema mbali na mitambo muhimu kama hiyo kuwekwa mahakamani ambayo ingeifanya kazi ya kunasa maelezo yote kama ambavyo shughuli za Bunge hufanywa, pia walikuwapo makarani watano wa maandishi ya hati mkato (short hand) ambao pia walihusika na kunakili ushahidi wote uliotolewa.

“Mawakili watetezi walipendekeza kuwa kesi isikilizwe kwa kipindi cha asubuhi tu kwa kuwa ingechukua muda mrefu kusikilizwa, hivyo iwapo ingesikilizwa kwa vipindi viwili, hawangepata fursa ya kushughulikia kazi zao nyingine muhimu.

Ikiwa kama sehemu ya kuimarisha ulinzi wakati wote ambao kesi hiyo ilikuwa inasikilizwa, Msajili wa Mahakama kuu aliweka bayana kuwa Wote ambao wangefika mahakamani kusikiliza kesi hiyo wangepekuliwa.

Mapema kabla kesi haijaanza kusikilizwa, Seukle aliifahamisha mahakama kwamba Uncle Tom ambaye alikuwapo katika orodha ya awali ya washtakiwa 30 na ambaye alitoroka akiwa rumande Juni 1983, aliondoka nchini mwaka 1971 na kwenda kuishi nchini Uganda kwa sababu asingeweza kuishi Tanzania.

Uncle Tom aliacha kazi ya ualimu aliyokuwa akiifanya Kagera na kumfuata baba yake Uganda baada ya kukosana na maofisa wa usalama wa Tanzania.

Wakati Sekule akiieleza mahakama kuhusu Uncle Tom kutoroka rumande, wakili Lakha alisimama na kusema hakuna faida kwa upande wa mashtaka kupoteza muda wa mahakama kwa kutoa maelezo ya historia ya mtu ambaye si miongoni mwa washtakiwa 19 waliokuwa mbele ya mahakama.

Lakha alisema kutoa historia ya Lugangira ambayo haihusiani na ushahidi utakaotolewa mahakamani pia utafanya upande mmoja katika kesi hiyo kunufaika na taarifa hizo.

Hata hivyo, Jaji Kiongozi alisema ni sahihi na hakuna ubaya wowote iwapo maelezo ya historia ya Lugangira yatatolewa mahakamani ila tu alisisitiza lazima historia hiyo isionyeshe wala kutaja uhusiano wowote na washtakiwa 19 waliokuwa mbele ya mahakama.

Kesi ilipoanza kusikilizwa, mwandishi mmoja wa habari wa Tanzania alitajwa mahakamani kuwa alikuwa kiungo cha mawasiliano kati ya shahidi wa kwanza wa upande wa mashtaka na Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa.

Shahidi huyo, Abdallah Shaban Mhando, aliiambia Mahakama kwamba alifanikiwa kuwasiliana na Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa juu ya njama za kuiangusha Serikali na kumuua Rais kupitia kwa mwandishi wa habari wa gazeti la Serikali, Daily News na Sunday News, Charles Kizigha.

Mhando ambaye wakati huo alikuwa dereva wa teksi alieleza hayo wakati akihojiwa na wakili Murtaza Lakha aliyemtetea mshtakiwa wa kwanza, Hatty McGhee, ambaye alitaka kujua jinsi alivyofahamiana na McGhee na ambavyo hatimaye alifanikiwa kuwasiliana na Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa.

Wakili Lakha alipomuuliza Mhando iwapo Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa ambaye alimtaja kuwa jina lake ni Mahiga, ni ndugu yake alikataa kwamba si ndugu yake isipokuwa alimfahamu kupitia kwa rafiki yake.

Alipoulizwa rafiki yake huyo ni nani, Mhando alibabaika kisha akaomba apate ushauri wa Mkurugenzi wa Mashtaka, lakini Lakha alisisitiza kwamba lazima amtaje.

Baadaye alieleza kuwa rafiki yake huyo ambaye alikuwa kiungo chake cha mawasiliano kati yake na Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa ni Kizigha.

Kati ya mwaka 1980 na 1983, aliyekuwa Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa ni Balozi Augustine Mahiga (alizaliwa Jumanne ya Agosti 28, 1945 na kufariki dunia Ijumaa ya Mei 1, 2020).

Baadaye pia aliteuliwa kuwa mwakilishi wa kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Kimataifa akifanya kazi Geneva - Uswisi, ambapo baadaye mwaka 1992 na 1994 aliteuliwa kuwa kiongozi mwakilishi wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR).

Shahidi Mhando alifafanua kuwa pamoja na Kizigha kumsaidia kupiga simu kwa Mahiga, hawakuweza kuonana kwa muda waliokubaliana kwa sababu gari lake (Mhando) liliharibika na hivyo akashindwa kufika sehemu waliyokubaliana kukutana.

Aliongeza kwamba baada ya kushindwa kumwona Mahiga siku hiyo, ilimchukua tena muda kuonana naye kwa sababu Ijumaa, Desemba 17, 1982 alilazimika kusafiri kwenda Harare, Zimbabwe, kwa muda wa majuma mawili.

Kesho tutaendelaa na ushahidi uliotolewa na Abdallah Mhando na mahojiano kati yake na Wakili Murtaza Lakha. Je, alisema nini kwenye ushahidi huo? Tukutane toleo lijalo.