Kheri James awataka wananchi kupuuza taarifa za vitisho

Mwenyekiti wa UVCCM- Taifa,  Kheri James (aliyekaa kwenye kigoda) akivalishwa vazi la heshima la kabila la Wahehe na  mzee wa Kihehe, Hilary Kisonga baada ya kukaribishwa wilayani Mufindi mkoani Iringa. Picha na Mary Sanyiwa

Muktasari:

Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM), Kheri James amewakata Watanzania kupuuza taarifa  za vitisho zinazotolewa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu ugonjwa wa Covid19 na kuzua taharuki.

Mufindi.  Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM), Kheri James amewakata Watanzania kupuuza taarifa  za vitisho zinazotolewa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu ugonjwa wa Covid19 na kuzua taharuki.

Ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Machi 4, 2021 wilayani Mufindi Mkoa wa Iringa wakati akizungumza na mabaraza na jumuiya za chama hicho.

Amesema baadhi ya watu wanapotosha kuwa hali ni mbaya kuhusu maambukizi ya ugonjwa huo, “hata  Rais Magufuli amekuwa akisisitiza watu kuchukua tahadhari  juu ya maradhi mbalimbali ambayo yanaikabili nchini yetu kwa sasa.”

Amesema Watanzania wanapaswa kujua umuhimu wa kujikinga na kuwakinga wengine ili jamii iendelee kuwa salama.

“Sisi tuna umuhimu mkubwa wa kuwalinda wenzetu  na kujilinda wenyewe lakini tunaweza kujilinda  na maradhi  lakini kamwe hatuwezei kujilinda na kifo,” amesema akizitaka taasisi, mashirika na wadau kuwa msaada wa kuwakinga wengine.

Imeandikwa na Mary Sanyiwa