Kibarua kinachomsubiri Profesa Mkenda elimu

Muktasari:

  • Mwishoni mwa wiki iliyopita, Rais Samia Suluhu Hassan alifanya mabadiliko ya baraza la mawaziri, huku akimteua Profesa Adolf Mkenda kuwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Rais Samia Suluhu Hassan alifanya mabadiliko ya baraza la mawaziri, huku akimteua Profesa Adolf Mkenda kuwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia.

Profesa Mkenda anachukua nafasi ya Profesa Joyce Ndalichako, aliyehamishiwa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na wenye Ulemavu. Miaka sita ya kuwa waziri, Ndalichako amepanda milima na mabonde katika safari yake ya kupeleka mbele gurudumu la elimu nchini.

Katika harakati hizo, Profesa Ndalichako ambaye ni msomi bobezi wa elimu hususan fani ya takwimu za elimu, alifanikiwa na kugonga mwamba katika baadhi ya maeneo.

Miongoni mwa mafanikio atakayokumbukwa nayo kwa mujibu wa Dk Malima kutoka Chuo Kikuu cha Tumaini ni namna alivyo makini katika usimamizi wa mitihani.

“Alikuwa anairejesha elimu katika hadhi yake kutokana na usimamizi mzuri, wanafunzi wakawa wanafaulu kwa haki kutokana na kupungua kwa vitendo vya wizi wa mitihani,”anasema.

Ikumbukwe kuwa awali kabla ya kuwa Waziri, Profesa Ndalichako alikuwa Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta).

Kwa mujibu wa mhadhiri wa chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Sabatho Nyamsenda Prof Ndalichako alijizolea umaarufu akiwa Necta kwa jinsi alivyosimamia kwa ufanisi usahihishaji wa mitihani ya taifa kwa ngazi ya sekondari, ambapo matokeo yalidhihirisha kuwa sehemu kubwa ya wahitimu walikuwa hawawezi kufaulu mitihani.

“Kwa hiyo akiwa katibu mtendaji alionyesha udhaifu wa mfumo wa elimu, hasa katika kushuka kwa viwango,’’ alisema na kuongeza kuwa hata hivyo hakuweza kwenda mbali katika kusimamia ufufuaji wa mfumo wa elimu.


Kibarua cha Profesa Mkenda

Wachambuzi na wadau wa elimu, wanaamini Profesa Mkenda anaweza kukabiliana na mzigo mzito wa kubeba hasa katika kuyaweka sawa maeneo ambayo mtangulizi wake anatajwa kutofanya vyema. makala haya yanajaribu kuangazia baadhi ya maeneo ambayo waziri mpya anapaswa kuyavalia njuga kwa minajili ya kuboresha elimu nchini.


Uhuru wa kitaaluma

Nyamsenda, alimuomba Profesa Mkenda kuanza kazi kwa kutilia nguvu suala la uhuru wa kitaaluma (academic freedom).

“Uhuru wa kitaaluma umeshuka kwa kiasi kikubwa sana, kiasi kwamba katika vyuo vikuu hakuna tena mijadala ya kusisimua kuhusu masuala ya msingi ya nchi yetu,”anasema.

Anaongeza: “ Nakumbuka miaka ya hivi karibuni viongozi wa serikali ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) walikuwa na mgogoro na Bodi ya Mikopo. Jawabu la Waziri wa elimu aliyepita lilikuwa ni kuamuru viongozi hao wachukuliwe hatua za kinidhamu. Hii inatengeneza wasomi waoga wasioweza kudai haki zao na wanaowatetemekea watawala,”

Alisema elimu ni lazima izalishe wahitimu wanaoweza kufikiri, kuhoji na kusimamia wanachokiamini. Kwa hiyo, uhuru wa kitaaluma ni suala la kwanza ambalo Profesa Mkenda atapaswa kulisimamia.



Mafunzo kwa walimu

Kwa muda mrefu wadau wa elimu wamekuwa wakitoa kilio cha walimu kutoendelezwa wakiwa kazini. Pamoja na kuwapo kwa semina kadhaa, bado si walimu wote wanaobahatika kuhudhuria masomo, huku lawama zikielekezwa kwa maofisa elimu kata, wilaya na mikoa.

Matokeo yake wanasema hata kunapotokea mabadiliko yakiwamo ya mitalaa, walimu wengi wanashindwa kwenda na mabadiliko hayo kwa kukosa mafunzo ya namna ya kufundisha mitalaa hiyo.

“Ikumbukwe sasa hivi tunatumia mfumo mpya wa mtalaa unaozingatia umahiri wa wanafunzi, lakini kwa bahati mbaya hadi sasa si walimu wengi wenye maarifa nao,”anasema Dk Faraja Kristomus wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Anamuomba Profesa Mkenda, anapoanza kazi, kupigania bajeti ya mafunzo kwa walimu wa shule za msingi na sekondari.


Mabadiliko ya mitalaa

Profesa Ndalichako ameondoka akiacha mezani mchakato wa utekelezaji wa mabadiliko ya mitalaa ili kuendana na maono ya Rais Samia Suluhu Hassan, aliyeagiza mabadiliko ya mitalaa hiyo ili kuwawezesha wahitimu kuwa na ujuzi na stadi za kujitegemea maishani.

Mwalimu mstaafu, Bakari Heri anasema mchakato huo una maana kubwa zaidi hasa kipindi hiki ambacho wahitimu wengi wanamaliza masomo, lakini wanakosa ajira.

‘’Profesa aende pale akijua kuwa mtalaa pamoja na kuambiwa kuwa kwa sasa unaotumika ni ule wa umahiri na ujuzi, lakini kiuhalisia hata hao walimu wenyewe hawaujuia na ndio maana bado shule zinazalisha watu wasio na sifa. Aendelee alipoishia mwenzake ili mwishowe mtalaa alioutaka Rais uanze kufundishwa kwa ufanisi zaidi,’’ anasema.

Kinachotia moyo ni kuwa Profesa Mkenda haanzi sifuri, tayari mtangulizi wake alishajenga msingi wa upatikanaji wa mtalaa mpya, akianza na ukusanyaji wa maoni kutoka kwa wadau mbalimbali.

Novemba 8, Wizara ilifanya kikao na kamati ya kudumu ya Bunge ya huduma na maendeleo ya jamii, kwa lengo la kutoa taarifa ya maendeleo ya kazi ya uboreshaji mitalaa katika ngazi zote za elimu nchini.

Uwasilishwaji wa taarifa hizo ulifanywa na wakuu wa taasisi zinazohusika na mitalaa nchini ambao ni Dk Aneth Komba kutoka Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), ambaye aliwasilisha kwa upande wa mitalaa ya elimumsingi, Dk Adolf Rutayuga kutoka Baraza la Elimu ya Ufundi (NACTE), aliyewasilisha uboreshaji wa mitalaa ya elimu ya ufundi na vyuo vya kati, huku Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) Profesa Charles Kihampa akiwasilisha kuhusu mitalaa ya elimu ya juu.

Awali Juni 18 mwaka 2021, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, iliwakutanisha wadau mbalimbali kwa lengo la kukusanya maoni kuhusu mabadiliko ya mitalaa.


Ajira kwa wahitimu

Unaweza kuhoji ni kwa namna gani Profesa Mkenda anapaswa kubeba mzigo wa ajira kwa Watanzania, hasa kwa kuzingatia uwa kuna wizara maalumu ya ajira.

Anakwenda kusimamia sekta ya elimu yenye uhusiano mkubwa na ajira. Ukweli ni kuwa kwa miaka kadhaa sasa, wahitimu wanaomaliza katika ngazi mbalimbali za elimu wamekuwa wakikosa ajira, kwa sababu wengi wanategemea ajra rasmi za kuajiriwa, huku mfumo wa elimu ukikosolewa kwa kushindwa kuwa na mitalaa inayofundishja ujuzi na stadi za maisha.

Katika andiko lake la ‘Higher Education System and Jobless Graduates in Tanzania la 2016, mwanazuoni Lyata Ndyali anasema mfumo wa elimu wa Tanzania hauzalishi wahitimu wenye stadi na ujuzi wa kazi.

Ndyali katika andiko lake hilo amenukuu maandiko ya kitaaluma ya Mjema (1997), Bugachwa (1991) na Luvanga (1994), yote yanahitimisho kuwa tatizo la ukosefu wa ajira nchini hasa kwa vijana linatokana na mfumo wetu wa elimu usiotilia kuwapo kwa mitalaa inayozalisaha wasomi wemye ujuzi na stadi za kazi.

Ni kwa msingi huo, ujio wa Profesa Mkenda katika wizara hii mama na nyeti kwa maendeleo ya nchi, unatarajiwa kuja na mikakati ya kufumua mfumo mzima wa elimu kama kweli Taifa la Tanzania linataka majawabu ya namna ya kupambana na janga hili la ajira.

Ndyali anahitimisha kwa kusema vyuo vikuu nchini ni lazima vifuatilie mabadiliko na mahitaji ya soko la ajira ili waweze kufikiri upya na kuja na mbinu mpya kulingana na soko la ajira.


Kibarua zaidi

Kwa wadau wengi, elimu ndio sekta mama na nyeti kwa Taifa, Profesa anapaswa kukuna kichwa kwenda kutatua changamoto kama vile kilio cha maslahi duni kutoka kwa watumishi wa sekta hiyo hususan walimu na wahadhiri. Lakini pia ana jukumu zito la kuhakikisha shule za umma zinarudi katika ubora wake wa miaka ya nyuma kitaaluma, hasa baada ya miaka ya karibuni kupigwa kikumbo kikubwa na shule binafsi kwenye matokeo ya mitihani ya kitaifa.