Kidata awaonya wafanyabiashara bidhaa za magendo Bukoba

Muktasari:

  • Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Alphayo Kidata amewataka wafanyabiashara mkoani Kagera wanaojihusisha na biashara ya magendo kuacha mara moja, akionya kuwa watakaobainika watafilisiwa.

Bukoba. Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Alphayo Kidata amewataka wafanyabiashara mkoani Kagera wanaojihusisha na biashara ya Magendo kuacha mara moja, akionya kuwa watakaobainika watafilisiwa.

Kidata ameyasema hayo leo Jumatano Oktoba 20, 2021 Katika mkutano na wafanyabiashara waliopo mkoani humo uliofanyika Katika ukumbi wa mkuu wa Mkoa wa Kagera.

Amesema kuwa kuna baadhi ya wafanyabishara wasio waaminifu ambao wamekuwa wakifanya biashara za magendo ya bidhaa mbalimbali hivyo akawataka kuacha tabia hiyo, kwani inasababisha kupotea kwa mapato ya serikali.

"Wafanyabiashara mtumie mipaka rasmi, mwache kupitia njia za panya kwani biashara za magendo zitasababisha mfilisiwe mali mlizo nazo na hivyo kurudisha nyuma biashara zenu na kusababisha viwanda vya ndani kupunguza ajira za vijana wenu,” amesema Kidata.

Ametaja baadhi ya bidhaa ambazo zimekuwa zikifanywa magendo kuwa ni, vitenge, pombe kali, saruji na mafuta ya kula.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabisha wenye Wiwanda na Kilimo (TCCIA) Mkoa wa Kagera, Ladislaus Gerald amesema biashara ya magendo inamuathiri mfanyabiashara, hivyo akawasisitiza kuachana na biashara hizo.