Kikwete ataka wasiokubali matokeo uchaguzi Kenya waende kortini
Muktasari:
- Kiongozi wa waangalizi wa Uchaguzi Mkuu wa Kenya kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika Agosti 9, 2022 ambaye ni Rais mstaafu wa Tanzania, Jakaya Kikwete amewataka wagombea ambao hawatakubaliana na matokeo waende mahakamani badala ya kutumia njia nyingine isiyo sahihi.
Dar es Salaam. Kiongozi wa waangalizi wa Uchaguzi Mkuu wa Kenya kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika Agosti 9, 2022 ambaye ni Rais mstaafu wa Tanzania, Jakaya Kikwete amewataka wagombea ambao hawatakubaliana na matokeo waende mahakamani badala ya kutumia njia nyingine isiyo sahihi.
Itakumbukwa kuwa mwaka 2017, Mahakama ya Juu iliyafuta matokeo ya kura ya urais ya uchaguzi huo yalifutwa baada ya kukubaliana na hoja za mgombea urais Raila Odinga kulikuwa na kasoro kwenye ukusanyaji na usafirishaji wa matokeo hayo hadi Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ya Kenya.
Kikwete ametoa kauli hiyo, leo Alhamisi Agosti 11, 2022 wakati akitoa ripoti ya awali juu ya mchakato wa uchaguzi ulivyokuwa hadi hivi sasa ambapo matokeo ya maeneo mbalimbali yamekuwa yakitolewa.
Kikwete amesema kuwa uchaguzi umefanyika kwa amani, utulivu na uwazi zaidi kutokana na maandalizi yaliyofanywa na Taifa hilo pamoja na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).
“Tunawasihi muendeleze amani na utulivu baada ya matokeo kutangazwa, kama mtu atakuwa na pingamizi kuna mwanya wa kisheria hivyo wachukue mkondo huo” amesema
Amesema anaamini matokeo yatakayotangazwa na IEBC ndiyo yatakayoakisi kilichofanyika katika vituo mbalimbali na ndicho Wakenya walichokitaka