Kikwete kumshirikisha Lionel Messi kampeni kusaidia watoto njiti nchini
Dar es Salaam. Kama ulikuwa hufahamu, mchezaji mpira maarufu duniani, Lionel Messi naye alizaliwa mtoto njiti.
Mtoto njiti ni yule alitezaliwa kabla ya wakati kufikisha wiki 37 za mimba kama inavyotakiwa kwa mama mjauzito.
Siri ya Messi kuwa naye alipitia changmoto hiyo imetobolewa leo Ijumaa Novemba 17, 2023 na Rais Mstaafu wa Awamu ya nne, Jakaya Kikwete, alipokuwa akizindua kampeni maalum ya utoaji huduma kwa watoto njiti nchini iliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Katikati ya hotuba yake kwa washiriki waliohudhuria halfla hiyo alimtambulisha Doris Mollel ambaye ni Mkurugenzi wa taasisi ya Doris Mollel na kueleza namna ambavyo amekuwa akiwapambania watoto hao ikiwemo kugawa vifaa kwenye hospitali na kutoa mafunzo kwa watumishi wanaowahudumia vichanga kwa kipindi cha miaka kumi sasa.
"Simama Doris wakuone, geuka wakuone vizuri. Huyu kwa muda sasa amekuwa akiwapambania vichanga hao njiti kuhakikisha wanapata huduma zilizo bora na kuweza kukua kama watoto wengine,” amesema Kikwete na kuongeza:
“Alishaniomba kumsaidia mambo mbalimbali katika kampeni yake hiyo lakini kubwa nina deni kwake la kumkutanisha na Lionel Messi ambaye naye alizaliwa njiti kama mlikuwa hamjui na nitahakikisha nafanya hivyo."
Akizungumzia kuhusu kampeni ya utoaji huduma kwa watoto njiti, Kikwete amesema kunahitajika hatua za haraka kwa kuwa tatizo hilo ni kubwa hapa nchini ambapo hali inaonyesha kila mwaka Watoto 250,000 hadi 300,000 hupoteza maisha.
"Idadi hii ya watoto ni wengi sana maana kama kila mwaka watanzania tunaongezeka milioni mbili kwa mwaka ni wazi kuwa kuna watoto hao njiti zaidi ya 300,000 wanazaliwa ni wengi mno,"amesema Kikwete.
Kwa upande wake Doris alisema ahadi hiyo ni kubwa kwake ukizingatia Mercy ana mashabiki wengi duniani hivyo ujumbe wa kuwapambania watoto hao utafika vilivyo kwa jamii.
Amesema mbali na Messi mwingine anayetamani kuungana naye katika harakati hizo ni mwanamuziki Mariah Carey ambaye yeye alizaa watoto pacha njiti.
"Ukiacha wasanii hao Messi na Mariah, pia hapa nchini nimekuwa nikishirikiana kwa karibu na mwanasoka wetu Samatta na mwanamuziki Ali Kiba.
"Hawa mara kwa mara wamekuwa wakiandaa mashindano ya mpira yanayolenga kukusanya fedha za kusaidia mahitaji mbalimbali katika hospitali zetu," amesema Doris.
Awali Naibu Katibu Mkuu, Dk Grace Maghembe amesema kutokana na tatizo la kuzaliwa kwa watoto njiti amewaomba kujua serikali ina mipango katika kupunguza tatizo hilo na kwa kuanzia ni kuwa na vituo h visivyopungua 350 nchini vinavyotoa huduma kwa watoto hao (yaani hospitali za wilaya na vituo vya afya kimkakati) na hii itakuwa ni pamoja na kwa hospitali binafsi.
Wakizungumzia hilo baadhi ya wadau akiwemo Mkurugenzi wa Taasisi ya Afya Ifakara, Dk Honorati Masanja alisema kama taasisi ya Utafiti wataendelea kufanya taiti zitakaweza kutoa majibu ya utekelezaji wa afua mbalimbali kwa kuonyesha ushahidi nini kinaweza kufanya kazi katika kuboresha afya ya mama na mtoto.
Kuhusu mpango huo alisema unaenda kuongeza chachu na kama nchi inapaswak ukimbia ili kuweza kufikia vifo 12 kati ya vizazi hai 1000 ifikapo 2025.