Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kilimanjaro kupunguza idadi ya kaya maskini kwa asimilia 50

Baadhi ya wanufaika wa Mpango wa kunusuru kata maskini (Tasaf) wakiwemo wanafunzi wa  shule ya Msingi Nkeku pamoja na wanufaika wengine wa Kijiji cha Ngumbaro, wilayani Siha. Picha na Janeth Joseph

Muktasari:

  • Mkoa wa Kilimanjaro kupitia mpango wa kunusuru kaya maskini (Tasaf) umelenga kupunguza idadi ya kaya maskini kwa zaidi ya asilimia 50 na kuwa na kaya zenye uwezo baada ya mpango huo kuonesha mafanikio makubwa kwa walengwa.

Siha. Mkoa wa Kilimanjaro kupitia mpango wa kunusuru kaya maskini (Tasaf) umelenga kupunguza idadi ya kaya hizo kwa zaidi ya asilimia 50, hii ni baada ya mpango huo kuonesha mafanikio makubwa kwa walengwa.

Akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Ngumbaro, Wilaya ya Siha, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa huo, Jairy Khanga amesema kwa kipindi cha mwaka 2020/2023 Serikali imetenga Sh23.2 bilioni kwa ajili ya kuzinusuru kaya maskini zipatazo 41,200.

"Mkoa wa Kilimanjaro ni wanufaika wakubwa katika mpango huu wa kunusuru kaya maskini, katika kipindi cha mwaka 2020 hadi 2023 mkoa huu tumeweza kupokea Sh23.2 bilioni kwa ajili ya wanufaika wa mpango huu, na katika kipindi chote hiki walengwa wamenufaika katika nyanja mbalimbali za kijamii,"

Amesema kwa sasa mkoa huo umelenga kupunguza kaya maskini kutokana na jitihada kubwa za mafanikio zilizoonyeshwa kwa walengwa hao ambapo baadhi yao kwasasa ni wajasiriamali wakubwa na wanavipato vikubwa katika familia zao.

"Sisi kama mkoa, lengo letu ni kunusuru kaya maskini, sasa hivi lengo letu ni kwamba tunakwenda kuhakikisha hizi kaya zinapungua kwa asimilia 50 ili kaya zote ziwe na watu wenye uwezo na wanaojiendeleza wenyewe," amesema Khanga.

Mkurugenzi wa Tathmini na Mawasiliano Tasaf, Fariji Mishael amesema mpango wa kunusuru kaya maskini umeonyesha mafanikio makubwa kwa walengwana hali zao zimekuwa ni tofauti na ilivyokuwa mwanzoni.

Amesema sasa hivi walengwa wa mpango huo, wameweza kuzalisha na kuweza kufanya mambo makubwa ya maendeleo ikiwemo kuwapeleka watoto shule kuanzia shule za msingi hadi chuo Kikuu na kwamba sasa wanatakiwa kutoka katika hatua hiyo na kwenda kujiendeleza wenyewe.

"Sasa hivi ukiangalia watu wamefanya maendeleo makubwa, fedha wanazopata kutokana na miradi yao ni kubwa kuliko ile wanayoipata kwenye miradi na kwasababu hiyo hawa wamefanya mambo ya maendeleo ambayo ni makubwa wanatakiwa watoke waje wajiendeleze wenyewe zaidi,"

Aliongeza "Dhana ya kusema kwamba mradi unatakiwa uendelee kuwapa fedha inatakiwa iondoke, waendeleze vile walivyo navyo hivyo watasaidia mbele ya safari ili tupate watu wengine ambao wana uhitaji zaidi kwasababu kile ambacho walitakiwa wakipate kitabaki na kitasaidia wengine,"

Nao baadhi ya wanufaika wa Tasaf katika wilaya ya Siha, wamesema baada ya kuibuliwa na mradi huo wameweza kupata mafanikio makubwa ikiwemo kuanzisha miradi midogo midogo ambayo imeleta mafanikio makubwa kwao pamoja na jamii inayowazunguka.

Mmoja wa wanufaika wa Tasaf katika kijiji cha Ngumbaro, Lilian Lekule, amesema Tasaf imefanya kazi kubwa katika maisha yao hasa kuwaondoa katika umaskini waliokuwa nao kwa kuweza kuanzisha miradi midogo midogo ambayo imewawezesha kujikwamua katika umaskini.

Magdalena Akaro, mnufaika mwingine wa Tasaf Wilaya ya Siha, amesema maisha yake awali yalikuwa duni na wakati mwingine alishindwa kupeleka watoto shule kutokana na ugumu wa maisha aliokuwa nao hivyo kupitia Tasaf alipata fedha na kufuga mifugo ya kisasa ambayo ilimpatia fedha na kuweza kujikwamua kiuchumi.