Kilimanjaro kuzifuata kura za Samia hadi hospitalini

Muktasari:

  • Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu amesema katika uchaguzi mkuu wa 2025, watawapelekea karatasi za kupiga kura hata wagonjwa walioko hospitalini katika wilaya ya Rombo, ili wampigie kura Rais Samia Suluhu Hassan

Rombo. Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu amesema katika uchaguzi mkuu wa 2025, watawapelekea karatasi za kupiga kura hata wagonjwa walioko hospitalini katika wilaya ya Rombo, ili wampigie kura Rais Samia Suluhu Hassan.

Mkuu huyo wa mkoa alitoa kauli hiyo jana, mbele ya Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo, wakati alipopata fursa ya kuzungumza wakati katibu mkuu huyo alipotembelea shule ya sekondari ya kata ya Mamsera wilayani Rombo.

Babu alisema katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 wanahitaji Rombo yote iwe ya kijani na 2025 uwe wa mafiga matatu kwa maana ya diwani, mbunge na Rais atokane na CCM na hata aliyeko hospitali, atapelekewa karatasi ya kura.

“Haiwezekani Rais akaleta fedha kwa ajili ya kuwasaidia wananchi halafu wanatokea watu wa ovyo, wanatengeneza vitu vya ovyo, halafu sisi tuvikubali,” alisema mkuu huyo wa mkoa ambaye aliripoti mkoani humo juzi.

“Utaratibu wa Mkoa wa Kilimanjaro sasa chini ya uongozi wangu, ukifanya ovyo maana yake hutufai, unatuharibia chama chetu na sisi tunataka 2024 kijani itawale Rombo na 2025 uwe wa mafiga matatu

“Hata aliyeko hospitali, tutampelekea karatasi ya kura ampigie Mama Samia Suluhu Hassan. Ndugu zangu tumuombee Mungu sana Rais, anafanya kazi kubwa, Rais halali, analeta fedha nyingi kwenye hospitali, maji, barabara. Sisi ni wajibu wetu viongozi kusimamia wananchi wapate huduma bora,” alisisitiza.

“Lakini pia sitaki kusikia mtu ameibiwa au amenyang’anywa mali zake, Chama cha Mapinduzi kinataka wananchi wafanye biashara zao kwa uhuru ilimradi wasivunje sheria na kodi ya Serikali walipe ili maendeleo yawafikie. Ile tabia ya kutolipa kodi pia iishe, lipeni kodi Serikali ilete maendeleo,” alisema mkuu huyo wa mkoa.

Chongolo na ardhi

Katika hotuba yake, Katibu mkuu wa CCM, Chongolo aliziagiza Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na Wizara ya Ardhi kuweka kipaumbele cha kupima maeneo yote ya umma na kuhakikisha yanakuwa na hati miliki.

Chongolo alisema ni lazima maeneo yote ya Serikali nchi nzima yawe na hati miliki ili kuepusha migogoro isiyo ya lazima na kusema hata shule hiyo ya Mamsera wamenunua eneo hilo kutoka kwa wananchi, lakini hawajapima na kuwa na hati.

“Itatokea siku moja kuwa na watoto watakaokuja kusema kihamba chetu kinafika mpaka hapa na kwa sababu hela alichukua baba na hayupo, watoto na wajukuu wataanzisha mgogoro utakaosumbua watu watakaokuwepo,” alisema Chongolo. Alisema ni lazima Tamisemi waweke programu ya kupima maeneo yote ya umma na kuweka malengo kwa kila mkurugenzi na katibu tawala wa mkoa kuhakikisha kwa kipindi fulani wanayatambua maeneo yote ya umma.

“Wizara ya Tamisemi na Ardhi, ni lazima sasa muweke kipaumbele cha kupima maeneo ya huduma nchi nzima, tuwe na hati za maeneo hayo ili yasiingiliwe wala kuwa na migogoro isiyo na lazima,” alisema.