Kilio cha uvuvi haramu Ziwa Victoria chatua kwa Waziri Ulega
Muktasari:
Wadau wa sekta ya uvuvi jijini Mwanza wameiomba Serikali kuchukua hatua stahiki kukabiliana na kudhibiti vitendo vya uvuvi haramu vinavyodaiwa kurejea kwa kasi ndani ya Ziwa Victoria.
Mwanza. Wadau wa sekta ya uvuvi jijini Mwanza wameiomba Serikali kuchukua hatua stahiki kukabiliana na kudhibiti vitendo vya uvuvi haramu vinavyodaiwa kurejea kwa kasi ndani ya Ziwa Victoria.
Hiyo ni miongoni mwa hoja zilizotawala mkutano kati ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega na wadau wa sekta ya uvuvi uliofanyika leo Oktoba 4, 2023 eneo la Soko la Kimataifa la Kirumba jijini Mwanza.
Gabriel Magoti, mvuvi na mkazi wa Nyasaka 'B' Manispaa ya Ilemela ndiye aliyeibua hoja hiyo mbele ya Waziri Ulega akisema vitendo hivyo vinatishia kutoweka kwa samaki na mazalia yake ndani ya ziwa hilo iwapo havitadhibitiwa.
‘’Uvuvi haramu umerejea kwa kasi ndani ya Ziwa Victoria…miaka ya nyuma uvuvi haramu ulipodhibitiwa tulikuwa tunapata samaki wakubwa tofauti na sasa. Tusipodhibiti hali hii, samaki watatoweka na vizazi vijavyo viatulaumu kwa kukosa samaki," amesema Magoti
Amesema uthibitisho wa uvuvi haramu ni uwepo wa samaki wadogo katika mialo na masoko ya samaki huku vyombo na mamlaka husika vikionekana kufumbia macho tatizo hilo.
Mvuvi mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Mafwere Nagabona ametaja changamoto nyingine inayoikabili sekta hiyo inayotakiwa kudhibitiwa ni vitendo vya wafanyabiashara kutoka nje ya nchi kwenda moja kwa moja hadi visiwani kununua samaki kinyume cha sheria inayowataka kununua bidhaa hiyo katika masoko rasmi likiwemo Soko la Kimataifa la Kirumba.
"Serikali ifanye uchunguzi…itagundua uwepo wa wafanyabiashara wa nje katika visiwa vya uvuvi kwenye mikoa yote ya Kanda ya Ziwa kuanzia Kagera, Mwanza hadi Mara. Hawa siyo tu wanakiuka sheria, bali pia wanaikosesha Serikali mapato,’’ amesema Mafwere
Ameishauri Serikali kuweka na kutekeleza sheria ikiwemo ya kuwafilisi wavuvi na wafanyabiashara wa nje wanaokiuka sheria kama inavyofanyika katika baadhi ya mataifa jirani.
Kutokana na hoja hizo, Waziri Ulega amemwagiza Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi Nchini, Stephen Lukanga ambaye pia aliyehudhuria mkutano huo kuchukua hatua kudhibiti vitendo vya uvuvi harama na biashara holela ya mazao ya samaki.
shughulikia suala la uvuvi changamoto ya uvuvi haramu nchini ili kulinda na kuokoa mazalia ya samaki na viumbe hai wengine.
Amesema kushindwa kutatua changamoto hiyo hata sita kumuondoa Mkurugenzi huyo pamoja na Maofisa uvuvi wake huku akihakikisha anawafungulia kesi mahakamani.
"Hatuwezi kuendelea kusikiliza maneno yanayojirudia kuhusu uvuvi haramu, Mkurugenzi wa uvuvi na maofisa shughulikieni suala hili,’’ ameagiza Waziri Ulega
Pamoja na uvuvi haramu, Waziri huyo pia amemwagiza Mkurugenzi huyo kwa kushirikiana na vyombo na mamlaka nyingine za Serikali kufuatilia na kudhibiti vitendo vya wafanyabiashara wa nje vya kwenda kununua mazao ya samaki moja kwa moja kwa wavuvi badala ya masoko rasmi.