Kina Uhuru, Raila wasaka mlango mwingine wa BBI

Kina Uhuru, Raila wasaka mlango mwingine wa BBI

Muktasari:

  • Baada ya kukwama mara mbili kortini kuhusu mpango wa kubadili baadhi ya vifungu vya Katiba ya Kenya, kundi Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM, Raila Odinga limeanza kusaka mlango mwingine wa kupenya.

Nairobi, Kenya. Baada ya kukwama mara mbili kortini kuhusu mpango wa kubadili baadhi ya vifungu vya Katiba ya Kenya, kundi Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM, Raila Odinga limeanza kusaka mlango mwingine wa kupenya.

Hata hivyo, mpango huo pia wa kutumia Bunge, unaosukumwa na baadhi ya wabunge waliowasilisha miswada mitatu huenda zikagonga mwamba.

Hii ni baada ya watu walio karibu na Naibu Rais William Ruto, wakiongozwa na Mbunge wa Garissa Mjini, Aden Duale kumuomba Spika wa Bunge la Kitaifa, Justin Muturi asitishe mijadala ya miswada mitatu inayolenga kubadili vipengele kadhaa vya Katiba.

Moja ya miswada hiyo ni wa Marekebisho ya Katiba unaodhaminiwa na Kamati ya Bunge Kuhusu Utekelezaji wa Katiba (CIOC) chini ya uenyekiti wa Mbunge wa Ndaragua Jeremiah Kioni, unapendekeza kumruhusu Rais kuteua baadhi ya mawaziri kutoka bungeni.

Kwa sasa katiba ya Kenya inataka mawaziri wateuliwe nje ya Bunge.

Muswada huo unapendekeza magavana pia waruhusiwe kuteua baadhi ya mawaziri kutoka katika mabunge ya kaunti.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Kenya, muswada huo umejaa mapendekezo sawa na yale yaliyomo katika muswada mwingine ambao umedhaminiwa na Mbunge wa Mugirango Magharibi, Vincent Kemosi ambao unapendekeza Rais ateue mawaziri wote miongoni mwa wabunge waliochaguliwa.

Kemosi pia anapendekeza viti vya ubunge vitakavyoshindaniwa na wanawake pekee viongezwe kutoka 47 hadi 136.

Anasema lengo la mapendekezo hayo ni kufanikisha hitaji la vipengele vya 47 na 81 vya katiba kuhusu usawa wa kijinsia, kwamba angalau theluthi moja ya wabunge wanafaa kutoka jinsia tofauti.

Muswada mwingine wa marekebisho ya Katiba uliodhaminiwa na Kamati ya CIOC unapendekeza kuwa vyama vya kisiasa viteue waliogombea urais na wagombea wenza katika Bunge la Kitaifa au Seneti kuwa wajumbe maalumu.

Duale ambaye ni mmoja wa watu wa karibu na Ruto, anasema kwa kuwa mapendekezo makuu katika miswada hiyo mitatu yanashabihiana na yale yaliyomo kwenye muswada wa BBI uliozimwa na Mahakama ya Rufaa na Mahakama Kuu, hivyo haipaswi kujadiliwa na kuamuliwa bungeni.

“Bunge likiendelea kujadili miswada hiyo, litakuwa linakwenda kinyume na maamuzi ya Mahakama Kuu na ile ya Mahakama Rufaa. Hii ni kwa sababu maamuzi yaliyotolewa na mahakama hizo yalieleza wazi kwamba marekebisho ya Katiba yanayolenga kugeuza muundo wa kitengo cha utawala, sharti yafanywe kupitia Baraza la Wawakilishi,” anasema mbunge huyo wa Garissa Mjini.

Anasema kitendo cha kupendekeza kuwa baadhi ya mawaziri wateuliwe kutoka miongoni mwa wabunge, miswada hiyo itakuwa inabadili muundo wa kitengo cha utawala na hivyo kutoa nafasi kwa Rais kuingilia utendakazi wa Bunge.

“Hatua kama hii itafanya bunge kuwa sehemu ya kitengo cha Serikali Kuu na hivyo kupoteza uhuru wake. Wakenya hawafai kurejeshwa katika enzi ambapo Bunge lilidhibitiwa na Ikulu ya Rais. “Tutapinga vikali njama hii ya kupenyeza mapendekezo ya BBI kupitia mlango wa nyuma,” Duale, kiongozi wa zamani wa walio wengi bungeni alinukuliwa na gazeti la Taifa Leo.

“Mahakama ya Rufaa ilisema waziwazi katika uamuzi wake Agosti 20, 2021 kwamba marekebisho yoyote ya Katiba yanayoathiri muundo wa utawala sharti yafanywe kupitia baraza la wawakilishi, (yaani Constituent Assembly). Majaji sababu wa mahakama hiyo waliamua kuwa Bunge halina mamlaka kama hiyo,” anaeleza huku akifananisha jaribio la Bunge kufufua BBI kama “kupoteza wakati”.

Lakini Kioni anapuzia pingamizi dhidi ya miswada yake akisema hiyo ni sawa na kuingilia mamlaka na utendakazi wa Bunge.

“Miswada hii ya marekebisho ya Katiba ilitayarishwa na kuwasilishwa bungeni mapema mwaka wa 2019 kabla ya kuundwa kwa mswada wa BBI. Kwa hivyo, Bunge haliwezi kuzuiwa kuijadili na kuipigia kura kwa sababu ina baadhi ya vipengele vilivyoko katika BBI, ilhali haikutayarishwa chini ya muktadha wa mpango huo,” anasema mbunge huyo.