Kina Zumaridi wakutwa na kesi ya kujibu

Mshtakiwa namba moja kwenye kesi ya jinai namba 10/2022 Diana Bundala maarufu Mfalme Zumaridi na washtakiwa wenzake nane wakiwa ndani ya Mahakama ya Hakimu Mkazi kusikiliza uamuzi wa kesi yao. Zumaridi na wenzake wamekutwa na kesi ya kujibu. Picha na Mgongo Kaitira

Muktasari:

Uamuzi huo umetolewa leo Jumanne, Oktoba 4, 2022 na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Monica Ndyekobora wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutolewa uamuzi iwapo washtakiwa hao wanakesi ya kujibu au laa.

Mwanza. Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mwanza imewakuta na kesi ya kujibu, Diana Bundala maarufu Mfalme Zumaridi na wenzake nane katika mashtaka matatu yanayowakabili.

Washtakiwa katika kesi hiyo ya Jinai namba 12/2022 ni Zumaridi, Amos Kailembo, Isaya John, Isaka Mafuru, Neema Julian, Suzana Simon, Anitha Yesaya, George Maloji na Veronica Emmanuel.

Uamuzi huo umetolewa leo Jumanne Oktoba 4, 2022 na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Monica Ndyekobora wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutolewa uamuzi iwapo washtakiwa hao wanakesi ya kujibu au laa.

Zumaridi na wenzake wanakabiliwa na mashtaka matatu ambayo ni kufanya shambulio la kudhuru mwili, kuzuia askari kutekeleza majukumu yake na kuzuia ofisa wa umma kutekeleza majukumu yake.

Washtakiwa hao wanadaiwa kutenda makosa hayo, Februari 23 mwaka huu nyumbani kwa Zumaridi katika mtaa wa Buguku kata ya Buhongwa jijini Mwanza kinyume na kifungu namba 241, 243 (b) na 114 (a) na (b) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu.

Hakimu Ndyekobora amesema mahakama imewakuta washtakiwa na kesi ya kujibu baada ya upande wa Jamhuri kufunga ushahidi kwa mashahidi 12 na vielelezo 11.

Baada ya kutamka hivyo akawataka mashahidi kusema watajitetea kwa kiapo au bila kiapo ambapo wakili wa Utetezi, Steven Kitale amesimama na kuieleza mahakama kuwa washtakiwa wote watajitetea kwa kiapo.

Baada ya maelezo hayo, Hakimu, Ndyekobora ameahirisha kesi hiyo huku akisema ushahidi wa upande wa utetezi utasikilizwa kwa siku tano mfululizo kuanzia Oktoba 17 mwaka huu.