Kiongozi kikundi cha kigaidi auawa Mali

Kiongozi kikundi cha kigaidi auawa Mali

Muktasari:

  • Kiongozi wa kikundi cha kigaidi cha Kiislamu (Islamic State) katika eneo la Greater Sahara (ISGS), Adnan Abou Walid al-Sahrawi ameuawa katika operesheni ya Jeshi la Ufaransa, huko Menaka Mali.

  

Mali. Kiongozi wa kikundi cha kigaidi cha Kiislamu (Islamic State) katika eneo la Greater Sahara (ISGS), Adnan Abou Walid al-Sahrawi ameuawa katika operesheni ya Jeshi la Ufaransa, huko Menaka Mali.

Al-Sahrawi, ambaye ameuawa mwezi mmoja uliopita, kifo chake kimetangazwa jana na Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, huku akisisitiza kuwa hayo ni mafanikio mengine makubwa katika vita dhidi ya vikundi vya kigaidi huko Sahel.

Waziri anayesimamia vikosi vya jeshi, Florence Parly, alisema al-Sahrawi aliuawa wiki kadhaa zilizopita, lakini walikuwa wakingojea uthibitisho kwamba aliuawa na kifo chake sasa kimethibitishwa.

Parly aliwapongeza maofisa wa jeshi na ujasusi ambao walichangia kwa muda mrefu kuendesha msako dhidi ya al-Sahrawi.

Alisema kifo hicho ni pigo kubwa dhidi ya kundi hilo la kigaidi na kusisitiza kuwa mapambano hayo yanaendelea.

ISGS inalaumiwa kwa kuhusika katika mashambulio mengi ya kigaidi katika eneo la mipakani mwa nchi za Mali, Niger na Burkina Faso.

Kikundi kinachoshirikiana na Al-Qaeda cha GSIM pia kinafanya kazi katika eneo hilo.

Al-Sahrawi amekuwa akidaiwa kuhusika na shambulio la Oktoba 4, 2017 nchini Niger na kusababisha vifo vya wanajeshi wanne wa Marekani na wengine wanne kutoka watu jeshi la Niger.

Kufuatia shambulio hilo, Marekani ilitangaza dau la Dola 5 milioni kwa yeyote atakayefanikisha kukamatwa kwa Sahrawi.

Kundi lake pia linashutumiwa kuwateka wafanyakazi waliokuwa Ufaransa waliokuwa wakitoa misaada huko Sahel na inaaminika bado alikuwa akimshikilia Mmarekani Jeffrey Woodke, ambaye alitekwa nyara huko Niger mwaka 2016.

Pia, aliamuru kufanywa kwa shambulio lililotokea Agosti 2020 huko Niger na kuwashambulia wafanyakazi sita wa NGO wa Ufaransa na wawili kutoka Niger.

Kiongozi huyo mwenye msimamo mkali, Al-Sahrawi alizaliwa katika eneo lenye mabishano la Sahara Magharibi na baadaye alijiunga na Polisario Front.

Baada ya kukaa Algeria, alielekea kaskazini mwa Mali ambako alikuwa mtu muhimu katika kikundi kinachojulikana kama Mujao, kilichodhibiti mji mkubwa wa kaskazini mwa Gao mwaka 2012.

Operesheni ya jeshi iliyoongozwa na Ufaransa mwaka uliofuata iliwaondoa madarakani Waislamu wenye nguvu kutoka Gao na miji mingine ya kaskazini, ingawa makundi hayo baadaye yalikusanyika tena na kufanya mashambulizi.

Jeshi la Ufaransa limekuwa likipambana na watu wenye itikadi kali za Kiislamu katika eneo la Sahel ambapo Ufaransa ilikuwa wakati huo na nguvu ya kikoloni tangu uingiliaji wa 2013 kaskazini mwa Mali.

Juni, Macron alitangaza kwamba operesheni hiyo itapunguzwa na wanajeshi 2,000 kati ya 5,000 watakaoondolewa mwanzoni mwa mwaka ujao.

Habari juu ya kifo cha Al-Sahrawi zinakuja wakati vita ya ulimwengu ya Ufaransa dhidi ya Islamic State ikiwa vichwa vya habari huko Paris.

Mshtakiwa mkuu katika kesi ya mashambulio ya Paris ya mwaka 2015 alisema juzi kwamba mauaji hayo yaliyoratibiwa yalikuwa ya kulipiza kisasi kwa mashambulizi ya angani ya Ufaransa kwa kundi la Islamic State, likisababisha vifo vya watu 130.

Kaskazini mwa Mali ilianguka chini ya udhibiti wa wanajihadi mwaka 2012 hadi walipofukuzwa nje ya miji mwaka 2013.

Lakini Mali, Taifa maskini lenye makabila angalau 20, linaendelea kupigana na mashambulio ya jihadi na vurugu za kijamaa.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Jean-Yves Le Drian alisisitiza jana kuwa hitaji la serikali ni kudhibiti waasi.

“Ni muhimu sana, hasa Niger, wahusika wa serikali kwa haraka kuchukua udhibiti wa maeneo yaliyotelekezwa kwa Dola ya Kiislamu ili kurejesha maisha ya kawaida ya kila siku na huduma muhimu,” Le Drian aliiambia redio ya Ufaransa.