Kiongozi wa Mbio za Mwenge atoa maagizo kwa DC Mufindi
Muktasari:
- Kiwanda hicho kinategeneza samani kwa kutumia mabaki ya misitu chenye thamani ya Sh34.8 bil.
Mufindi. Kiongozi wa Mbio Mwenge wa Uhuru Taifa, Abdallah shaib Kaim amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Dk Linda Salekwa kupitia upya mikataba baina ya mwajiri na wafanyakazi wa Kiwanda cha Lush Chanzo Wood Industries kilichopo mjini Mafinga kinachofanya shughuli za utengenezaji wa mbao ngumu ili kujiridhisha na maslahi ambayo wanalipwa wafanyakazi wa kiwanda.
Akitoa agizo hilo, baada ya kukagua na kuweka jiwe la msingi zinazofanywa na kiwanda hicho leo Mei 5, 2023 kiongozi huo amesema wilaya wasimamie na kuhakikisha sheria na taratibu katika taasisi hizo zinafuatwa ili kuwalinda watumishi dhidi ya waajiri wao.
Kiwanda hicho cha kwanza nchi kutengeneza malighafi kwa kutumia mabaki ya miti kilichopo Kata ya Rungemba Mjini Mafinga chenye thamani ya Sh34.8 bilioni huku zaidi ya wananchi 100 watanufaika na kiwanda hicho.
Pia kiongozi huyo amesema licha ya kazi kubwa na nzuri inayofanywa na kiwanda hicho lakini wazingatie suala la usalama wa wafanyakazi kwa kuvaa vifaa ambavyo vitawakinga wafanyakazi wao wakati wa kufanya kazi ili kujiepusha na majanga ambayo wanaweza kuyapata.
"Naelekeza kuwa kuvaa mavazi ambayo kitaaluma yanajulikana lakini pia mvae maski maalumu ambazo zinaweza kulinda usalama wenu ili kujiepusha na majanga ambayo wanaweza kuyapata," amesema.
Kaim ameeleza kuwa kupitia uwekezaji huo umeongeza fursa katika kukuza sekta binafsi na kuongeza pato la taifa sambamba na kutoa ajira kuwa Watanzania ili kukuza pato la mtu mmoja mmoja.
"Nimpongeze mwekezaji huyu kutoka China pamoja na watendaji wote wa Kiwanda cha Lush Chanzo kwa kazi kubwa ambayo wanaendelea kufanya kwa sababu mbio za Mwenge ungefanya kazi ya ukaguzi wa kina ikiwemo mashine za kisasa na aina mbalimbali za bidhaa ambazo zinazalishwa katika kiwanda hicho.
Awali, akisoma risala kwa kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa Meneja msaidizi wa kiwanda hicho Justine Mligo Amesema kuwa kiwanda hicho kikikamilika litakuwa na uwezo wa kuzalisha mita za ujazo 100,000 ambapo kwa sasa kinazalisha mita za ujazo 25,000 za MDF kwa mwaka.
Aidha amesema kuwa lengo la mradi huo kuzalisha mbao ngumu za MDF board kwa ajili ya kutengeneza samani za ndani kwa kutumia mabaki ya mazao ya misitu.
"Mradi huu ni kati ya miradi mikubwa inayosaidia Wilaya kwenye uhifadhi wa mazingira na kupunguza uchafu kwani malighafi ambazo zinatumika ni mabaki yanayotokana na uchakatwaji wa mazao ya misitu," amesema meneja huyo.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Mafinga Mjini, Cosato Chumi amesema kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ameweza mazingira mazuri ya uwekezaji ambayo yanavutia wawekezaji kutoka nje ya nchi.
"Haya ambayo mnayaona ni jitihada za Rais ambazo amezifanya katika kufungua milango ya uwekezaji kwa sababu kama Taifa na Mafinga wananchi wamepata ajira na halmashauri wanapta tozo mbalimbali kupitia uwekezaji huo," amesema.
Hata hivyo Mwenge wa Uhuru umeweza kukimbizwa katika Halmashauri ya Mji Mafinga na kupitia miradi nane ambapo jumla yake thamani ya Sh 38.9 bilioni.