Kishindo cha Fatma Karume baada ya siku 243 kusimamishwa uwakili

Muktasari:

Licha ya Mahakama Kuu kubatilisha uamuzi wa Kamati ya Mawakili kumwondoa katika orodha ya mawakili nchini, Fatma Karume amedai ana mashaka kama atarudishiwa hati yake ya kufanya kazi za uwakili.

Dar es Salaam. Licha ya Mahakama Kuu kubatilisha uamuzi wa Kamati ya Mawakili kumwondoa katika orodha ya mawakili nchini, Fatma Karume amedai ana mashaka kama atarudishiwa hati yake ya kufanya kazi za uwakili.

Fatma, aliyewahi kuwa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), alipewa adhabu ya kufutwa katika orodha ya mawakili Septemba 23, 2020 na Kamati ya Mawakili baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kukiuka maadili ya taaluma hiyo, hivyo kumfanya kukaa siku 243 akitumikia adhabu hiyo.

Hata hivyo, alikata rufaa Mahakama Kuu Masjala Kuu akipinga uamuzi huo.

Mahakama Kuu katika hukumu yake iliyotolewa jana na jopo la majaji watatu lililoongozwa na Jaji Issa Maige akishirikiana na majaji Dk Deo John Nangela na Edwin Kakolaki lilikubaliana na moja ya sababu za rufaa ya Fatma ambayo ilibatilisha mwenendo na uamuzi wa Kamati ya Mawakili.

Katika sababu hiyo pekee ambayo Mahakama Kuu imekubaliana nayo, Fatma kupitia kwa wakili wake, Peter Kibatala alikuwa akidai kamati hiyo haikuwa na mamlaka ya kusikiliza malalamiko yaliyowasilishwa dhidi yake na mjibu rufaa wa kwanza, Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Mahakama hiyo ilisema kamati hiyo ya mawakili kusikiliza na kuamua shauri hilo ilikuwa inakwenda kinyume na amri ya Jaji Kiongozi ambaye katika amri yake ilimsimamisha kwa muda Fatma kusubiri Msajili awasilishe malalamiko dhidi yake katika kamati hiyo.

Hivyo, mahakama hiyo imesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali hakuwa na haki ya kuwasilisha malalamiko hayo, ambayo Jaji Kiongozi alielekeza yawasilishwe katika kamati hiyo na Msajli wa Mahakama Kuu.

Hivyo mahakama hiyo imebatilisha uamzi huo na badala yake imeelekeza Msajili ndio awasilishe malalamiko dhidi ya Fatma katika Kamati ya Maadili.

Akizungumzia uamuzi huo, Fatma alilieleza Mwananchi kuwa mpaka sasa yuko huru na kwamba uamuzi huo wa mahakama inaonyesha aliondolewa uwakili kinyume cha utaratibu, kwa kuwa kamati hiyo haikuwa na mamlaka hayo. Alisema hata amri ya Jaji Kiongozi ya kumsimamisha kwa muda imeshakwisha muda wake, maana kisheria amri kama hiyo haipaswi kukaa zaidi ya miezi sita.

“Ile ilikuwa ni `temporary order’ (amri ya muda). Hakuna `temporary order’ Tanzania inaweza kudumu kwa zaidi ya miezi sita, lakini sasa inaelekea mwaka wa pili na Msajili `haja-file’ (hajawasilisha) hiyo `complains’ (malalamiko), `automatically’ sasa moja kwa moja `order’ ya `kuni-suspend’ (kunisimamisha) haipo tena.

“Lakini sina imani kwamba watanirejeshea practicing certeificate yangu kwa sababu Registrar huyo huyo ndiye aliambiwa awasilishe complains zangu wa Advocate Committee lakini ndiye yeye hajafanya hivyo,” alisema Fatma.

Alisema Mahakama Kuu imeonyesha kulikuwa hakuna haki, haki haikuwa imetendeka kumuondolea uwakili kwa sababu Profesa Kilangi ndiye alikuwa amewasilisha malalamiko hayo mbele ya Jaji Kiongozi, Dk. Eliezer Felesh lakini yeye mwenyewe alikwenda kuyawasilisha katika kamati hiyo.

Awali, wakili Kibatala alilieleza Mwananchi kuwa uamuzi huo ni hatua kubwa kwa Fatma kupata haki yake.